Tuesday, May 21, 2013

Polisi nchini Uganda wawacharukia wanahabari ili kumlinda Rais Museven.

Polisi nchini Uganda wamefunga ofisi za Monitor Publications Limited (MPL), wachapishaji wa magazeti ya Daily Monitor na vituo vyake vya redio; KFM na Dembe FM.

Taarifa ya kulaani hatua hiyo iliyotolewa jana na Menejimenti ya MPL, ilieleza kwamba zaidi ya polisi 50 wenye silaha wakiwa kwenye sare zao walizingira ofisi za kampuni hiyo zilizoko eneo la Namuwongo, mjini Kampala wakiwa na hati ya upekuzi na kuzuia kuendelea kwa shughuli yoyote mchana kutwa jana.

Katika rabsha hizo, polisi walisema wanahitaji kufanya upekuzi ili kupata nyaraka zilizowezesha kuandikwa kwa habari iliyohusu “Mradi wa Muhoozi”, wenye nia ya kumweka madarakani mtoto wa Rais Yoweri Museveni, Brigedia Jenerali Muhozi.

Nyaraka hizo zilielezwa kwamba zilinaswa ikiwa ni barua iliyoandikwa na Mkuu wa Upelelezi, Jenerali David Tinyefunza kwa Mkuu wa Usalama wa Taifa ikieleza kuwapo kwa mpango wa kuwaua maofisa wote wanaopinga mpango huo.

MPL ni miongoni mwa kampuni za habari zilizoko chini ya mwavuli wa Nation Media Group (NMG), ikiwamo Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Hata hivyo, badala ya kufanya upekuzi kama walivyodai awali, polisi hao walizima umeme na kuzuia kufanyika kwa kazi zote ikiwamo shughuli za maandalizi na uchapaji gazeti na urushaji matangazo kwenye redio.

“Tumeshtushwa na tukio hili, ambalo ni ukiukaji wa wazi wa sheria na kukandamiza haki ya msingi ya Monitor kikatiba. Suala hili tayari liko mahakamani na uongozi unalaani vikali hatua ya polisi kutulazimisha kutaja chanzo cha habari yetu iliyoandikwa,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa MPL, Alex Asiimwe.

Aliongeza kuwa polisi walizuia watu kutoka au kuingia kwenye ofisi hizo, kuamuru kusimamishwa kwa shughuli zote kwa kisingizio cha kufanya upekuzi, kwa suala ambalo tayari linaweza kumalizika mahakamani.

Hadi jana jioni, polisi hao waliendelea kuzingira ofisi za MPL ambapo uongozi ulikuwa ukihangaika kutafuta jinsi ya kuzuia uhalifu huo.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment