Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) unatarajiwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu baada ya
ule wa Dharura wa marekebisho ya Katiba ulipangwa kufanyika Julai 13 mwaka huu.
Tarehe hizo zimepangwa na kikao cha dharura cha
Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika leo (Mei 9 mwaka huu) jijini Dar es
Salaam chini ya uenyekiti wa Rais wake Leodegar Tenga ambacho kupokea rasmi
maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na kupanga
utekelezaji wake.
“Kamati ya Utendaji ya TFF imepokea rasmi barua
ya FIFA na kupanga utekelezaji wake. Tumepokea maagizo ya FIFA yanayotuelekeza
cha kufanya, si TFF wala mtu mwingine yeyote anayeweza kuongeza jambo lingine.
“Maagizo ni undeni Kamati ya Maadili, Kamati ya
Rufani ya Maadili, fanyeni marekebisho ya Katiba, anzeni tena uchaguzi,
waliokuwepo na wengine wapya waruhusiwe. Tumejitahidi kuhakikisha uchaguzi uwe
kabla ya Oktoba 30 mwaka huu kama FIFA
walivyotuagiza,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema kazi kubwa itakuwa ni kutayarisha kanuni
hizo, kwani Kamati za Maadili lazima ziwe na kanuni zake na kuhakikisha kuwa
hakuna mgongano kati ya Kanuni za Nidhamu na Kanuni za Maadili.
Pia Rais Tenga amesema kuna kazi ya kuangalia
jinsi zitakavyoingia katika uchaguzi ambapo maana yake muda wa mchakato wa
uchaguzi utakuwa zaidi ya siku 40 za sasa, hivyo mabadiliko hayo yatagusa
vilevile Kanuni za Uchaguzi.
Kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji, rasmu ya
mwanzo ya Kanuni hizo inatakiwa iwe imetoka kufikia Mei 30 mwaka huu ambapo
itapelekwa FIFA kwa ajili ya kupata mawazo yao kabla ya kuendelea na hatua inayofuata.
Juni 15 mwaka huu Kamati ya Utendaji ya TFF
itakutana kupokea mapendekezo hayo ambapo baada ya kuyapitisha itayapeleka tena
FIFA. Taarifa (notice) ya Mkutano Mkuu wa Dharura ambayo kikatiba ni siku 30
itatolewa Juni 12 au 13 mwaka huu.
Baada ya Mkutano Mkuu wa Dharura wa marekebisho
ya Katiba, Kamati ya Utendaji itakutana kati ya Julai 14 na 15 mwaka huu kuunda
Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Maadili ili kuruhusu mchakato wa
uchaguzi uanze.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)
Mei 9,
2013
No comments:
Post a Comment