Thursday, May 16, 2013

UFAFANUZI KUHUSU LIGI YA MABINGWA MIKOA



Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) ilianza tarehe 12 Mei 2013 ikishirikisha klabu bingwa za mikoa yote ya Tanzania Bara, isipokuwa mikoa ya Pwani na Manyara ambayo kutokana na sababu tofauti ilishindwa kuwasilisha majina ya klabu zake hadi siku ya mwisho iliyowekwa na Kamati ya Mashindano, yaani tarehe 10 Mei 2013.



Suala la kukosekana kwa wawakilishi wa mikoa hiyo miwili limezua maswali mengi kiasi kwamba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linalazimika kutoa ufafanuzi kwa faida ya wadau wote wa mpira wa miguu.



Ligi ya Mabingwa wa Mikoa, ambayo ni mpya baada ya TFF kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa mpira wa miguu, ilipangwa kuanza tarehe 5 Mei 2013, lakini hadi tarehe ya mwisho ya kuwasilisha majina ya mabingwa wa mikoa, yaani tarehe 2 Mei 2013 mikoa michache ndiyo iliyokuwa imemaliza ligi zao na kupata mabingwa.



Kuchelewa huko kwa mikoa kumaliza ligi zao kuliilazimisha Kamati ya Mashindano ya TFF kuongeza muda wa mikoa kuwasilisha majina ya wawakilishi hao hadi tarehe 10 Mei 2013 na hivyo siku ya kuanza kwa Ligi kusogezwa mbele hadi tarehe 12 Mei 2013.



Hadi kufikia tarehe hiyo mpya ya mwisho ya kuwasilisha majina ya mabingwa wa mikoa, ni mikoa sita tu iliyofaidika na kuongezwa huko kwa muda na kupata wawakilishi wake. Mikoa hiyo ni Iringa, ambayo pamoja na kuongezwa kwa muda, iliandika barua ya kuihakikishia Kamati ya Mashindano kuwa itapata bingwa kabla ya kuisha kwa siku ya tarehe 10 Mei 2013.



Mikoa mingine ni Lindi, Mtwara, Geita, Tabora na Dodoma.

Mkoa wa Manyara haukuweza kumaliza ligi yake hadi mwisho wa siku ya tarehe 10 Mei 2013 na hivyo Kamati ya Mashindano iliyosubiri majina hadi saa 12:00 jioni siku hiyo kuamua kuwaondoa wawakilishi wa Manyara kwenye ratiba.



Awali, Kamati ya Mashindano iliamua kuwa ratiba ya mechi za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa ipangwe tarehe 7 Mei 2013, ikishirikisha mikoa ambayo ilishapata mabingwa wake, lakini baada ya kuona baadhi ya mikoa ilikuwa haijakamilisha ligi zake, Kamati iliamua kuwa ratiba ipangwe kwa kutumia majina ya mikoa kwa matumaini kuwa hadi kufikia tarehe 10 Mei 2013, mikoa itakuwa imeshapata wawakilishi wake na kwa kuwa ratiba inahusu mikoa jirani, ingekuwa rahisi kwa timu kusafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine.



Lakini Mkoa wa Manyara haukuweza kufanya hivyo na Kamati kulazimika kuuondoa kwenye ratiba kutokana na kushindwa kukidhi utashi huo.

Mkoa mwingine ambao uliondolewa kwenye ratiba ni Pwani ambayo pamoja na kutuma jina la mwakilishi wake, Kamati ilipokea malalamiko kutoka klabu zilizoshiriki Ligi ya Mkoa, zikidai kuwa jina la bingwa wa Pwani lililowasilishwa TFF lilikuwa batili kwa kuwa klabu ya Kiluvia United haikustahili kushiriki Ligi ya Mkoa kutokana na ukweli kuwa haijasajiliwa mkoani Pwani na wala haikushiriki ligi ya mkoa msimu uliopita. Kamati ya Mashindano iliiondoa Pwani kwenye ratiba na kulirudisha suala hilo mkoani.



Ingawa Katibu wa Pwani alijaribu kuishawishi Sekretarieti ya TFF iliangalie suala hilo kwa undani zaidi, Sekretarieti ilimjibu kuwa lilishafanyiwa uamuzi na Kamati, hivyo uamuzi huo usingeweza kutenguliwa na kumshauri katibu huyo arejee mkoani kwake kuwasiliana na viongozi wenzake kuona ni jinsi gani mkoa unaweza kunusuru hali hiyo kwa kufanya uamuzi ambao ungeuwezesha mkoa kupata mwakilishi.



Kwa mantiki hiyo, masuala ya Manyara na Pwani yalikuwa ndani ya uongozi wa mikoa husika na si Kamati ya Mashindano ya TFF kwa kuwa Kamati ilitaka ipatiwe jina la bingwa ambaye alipatikana kwa mujibu wa mfumo mpya wa Ligi ya Mikoa.



Ligi ya Mabingwa wa Mikoa inachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na hivyo timu zilizokutana tarehe 12 Mei 2013, zitarudiana mwishoni mwa wiki hii na kupatikana timu zitakazosonga mbele kwenye raundi nyingine hadi timu tatu bora zitakazopanda daraja kwenda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zitakapopatikana.



Ligi za Mikoa, kwa mujibu wa kanuni mpya, zinatakiwa ziwe na timu kati ya 16 na 20 na zinatakiwa zicheze mechi mbili za nyumbani na ugenini, hata kama zitakuwa zinatumia uwanja mmoja.



Uamuzi wa kubadilisha mfumo huo ulifanywa ili kuhakikisha kuwa mikoa inakuwa na na mashindano kwa mwaka mzima na hivyo kuiwezesha mikoa kujikita katika kutafuta mbinu za kupata fedha na kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu kwenye mikoa yao.



Uamuzi huo pia unasaidia kupunguza mtindo wa wachezaji kuzunguka klabu tofauti katika msimu mmoja kwa kuwa wanalazimika kutulia kwenye klabu moja hadi muda wa usajili unapofika.



Pamoja na wachezaji kutulia sehemu moja kwa muda mrefu, pia walimu wanapata fursa ya kujikita vizuri kwenye programu zao kwa kuwa wanakuwa na uwezo wa kufuatilia maendeleo ya wachezaji wao.

Pamoja na hayo yote, mfumo huo utasaidia kurudisha msisimko kwenye mikoa na hivyo kutoa fursa kwa vijana wengi wenye vipaji kuonekana na kuendelezwa.



TFF inatoa wito kwa viongozi wa mikoa kuanza kubuni sasa mikakati ya kuendesha ligi hizo msimu unaokuja kwa kuwa hakutakuwa na nafasi tena ya kuongeza muda kwa mikoa kuwasilisha majina ya wawakilishi wao.





Angetile Osiah

Katibu Mkuu

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mei 16, 2013



No comments:

Post a Comment