Mbunge wa Nkasi Kaskazini Ali Keisy akimtupia lawama mbunge wa Urambo Mashariki Prof Juma Kapuya nje ya ukumbi wa bunge jana, huku mbunge mwingine akiwapoza.
Katika mchango wake, Keisy alisema haungi mkono hoja kwa sababu
Barabara ya Sumbawanga hadi Kanazi-Mpanda mpaka Kibaoni haijajengwa kwa kiwango
cha lami.
Alisema zilitengwa Sh27 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara
hiyo lakini mpaka sasa Wachina waliopewa zabuni ya ujenzi huo wamekosa fedha na
wameamua kuuza kokoto.
Mara baada ya Bunge kuahirishwa, Keisy akiwa nje ya ukumbi huo
alifuatwa na Mbunge wa Urambo Mashariki, Profesa Juma Kapuya, Omary Nundu
(Tanga Mjini), Mendrady Kigola (Mufindi Kusini) na Rita Kabati (Viti Maalumu)
na kumzonga.
Baada ya wabunge hao kumzonga, Profesa Kapuya ambaye amewahi
kuwa waziri serikalini alihoji kitendo cha mbunge huyo kupinga bajeti... “Kwa
nini umekataa kuunga mkono hoja? Ulikuwa unalidanganya Bunge wakati unachangia
si kweli huko Rukwa hakuna barabara, barabara mnazo.”
Kessy alionekana kukerwa na swali hilo na kumjibu kwa hasira: “Nyinyi na mimi
nani ni mbunge Nkasi? Mimi sina unafiki napinga kutokana na yaliyopo jimboni
kwangu sipo hapa bungeni kuwafurahisha nyinyi na wala Serikali. Nipo kwa
masilahi ya wananchi wangu.” Baada ya majibu hayo, mbunge huyo aliondoka haraka
eneo hilo .
Baadaye jioni mwandishi wetu alimfuata ili kupata ufafanuzi juu
ya msimamo wake... “Hakuna barabara kwangu, kwa nini niunge mkono hoja?
Namshangaa sana
Kapuya kwa tabia aliyonionyesha pale... Mbona mama Margaret Sitta amesema
Tabora hakuna barabara hawakumfuata?”
Alisema wabunge hao hawana haki ya kuhoji kwa nini hakuunga
mkono hoja kwa kuwa kila mmoja amekuja bungeni kutokana na kushinda katika
jimbo lake. Akichangia hotuba ya bajeti hiyo, Kessy alisema haungi mkono hoja
kwa asilimia 100 hadi pale atakapoelezwa lini barabara hizo zitajengwa.
Alisema zaidi ya vijiji 30 vya mwambao wa Ziwa Tanganyika na
Barabara ya Kipili hadi Bandarini ni mbovu kwa kiasi kikubwa na muda wake wa
ujenzi kumalizika umeshapitiliza miezi mitatu iliyopangwa.
Alisema nchi imegawanyika kwani baadhi ya majimbo ya wabunge
yana lami hadi mlangoni lakini Nkasi hawajawahi kuiona akitoa mfano wa Jimbo la
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (Mpanda Mashariki) Same Mashariki kwa Anna Kilango.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment