KAULI YA SERIKALI BUNGENI KUHUSU TAARIFA YA AWALI
YA TUME YA TAIFA YA KUCHUNGUZA MATOKEO YA MTIHANI WA TAIFA WA KIDATO CHA NNE
MWAKA 2012
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 49(1) ya
Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2007, naomba kuwasilisha Taarifa ya
Awali ya Tume ya Taifa ya kuchunguza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha
Nne mwaka 2012.
2. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa
Matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2012 yalionesha kuwa kiwango cha
ufaulu kimeshuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni.
Matokeo yaliyotangazwa mwezi Februari, 2012 yalionesha kwamba kati ya Wanafunzi
367,756 waliofanya mtihani huo, Watahiniwa 126,847 ndio waliofaulu. Katika
idadi hii, Wanafunzi waliofaulu katika Daraja la Kwanza
hadi la Tatu ni 23,520, sawa na Asilimia 6.4 na Daraja la Nne ni 103,327, sawa
na Asilimia 28.1. Watahiniwa 240,909, sawa na Asilimia 65.5 ya Wanafunzi wote
waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 walipata Daraja la Sifuri.
3. Mheshimiwa Spika, kushuka kwa kiwango cha ufaulu
kulihusu shule za aina zote, yaani Sekondari za Serikali ikijumuisha
zilizojengwa kwa nguvu za Wananchi, Shule Binafsi na Seminari. Takwimu
zinaonyesha kwamba ukilinganisha matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2011 na mwaka
2012, Shule za Wananchi matokeo yao yameshuka kwa Asilimia 1.82; Shule za Umma
za zamani (Kongwe) yameshukwa kwa Asilimia 6.43; Shule Binafsi yameshuka kwa
Asilimia 6.39; na kwa Shule za Seminari yameshuka kwa Asilimia 7.29. Hali hii
inaonyesha kwamba, matokeo katika Shule za Wananchi yameshuka kwa kiwango
kidogo ikilinganishwa na yale ya Shule za Umma za zamani (Kongwe), Shule Binafsi
na Shule za Seminari ambazo zilitegemewa kufanya vizuri zaidi ya zile za
Wananchi ambazo matokeo yao
yameshuka zaidi kwa kati ya Asilimia 6.4 na 7.3.
4. Mheshimiwa Spika, kutokana na matokeo hayo
yasiyoridhisha na ambayo yapo nje kabisa ya mwenendo wa ufaulu kwa miaka ya
karibuni, Serikali iliamua kuunda Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha
Ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012 kwa madhumuni ya kupata
ufumbuzi wa kudumu.
HADIDU ZA REJEA
5. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchunguzi ilipewa Hadidu za
Rejea zikiwemo zifuatazo:
i. Kubainisha sababu za matokeo mabaya ya Mtihani wa
Kidato cha Nne mwaka 2012;
ii. Kubaini sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu
katika mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2011 hadi 2012;
iii. Kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua kukabiliana na
tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu mara moja, kipindi cha muda
mfupi, kati na kipindi cha muda mrefu;
iv. Kutathmini nafasi ya Halmashauri katika kusimamia Elimu ya Sekondari katika Halmashauri zake;
iv. Kutathmini nafasi ya Halmashauri katika kusimamia Elimu ya Sekondari katika Halmashauri zake;
v. Kuanisha sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia
hali hii ya matokeo.
6. Mheshimiwa Spika, katika kutafakari Hadidu za Rejea
hizo, Tume imejikita katika kujibu Maswali Makuu matatu.
i) Kwa nini matokeo ya Kidato cha Nne kuanzia mwaka 2008
yamekuwa na mserereko wa kushuka kuliko miaka iliyotangulia?
ii) Kwa nini Wanafunzi wa Kidato cha Nne wa mwaka 2012
matokeo yao
yalikuwa mabaya kuliko ya wenzao wa mwaka 2011 pamoja na kwamba ufaulu ulishuka
tangu mwaka 2008? na
iii) Nini kifanyike.
WAJUMBE WA TUME YA UCHUNGUZI
5. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchunguzi iliongozwa na Prof.
Sifuni Mchome kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania na ndiye alikuwa
Mwenyekiti. Wajumbe wengine waliteuliwa kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu, Baraza la
Wawakilishi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,
Madhehebu ya Dini, Chama cha Walimu, Muungano wa wenye Shule Binafsi na
Muungano wa Walimu wa Sekondari. Orodha ya Wajumbe wa Tume hiyo ni kama ifuatavyo:
NA. JINA TAASISI ANAYOTOKA NAFASI
1. Prof. Sifuni Ernest Mchome Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania Mwenyekiti wa Tume
2. Mhe. Bernadeta K. Mushashu (Mb.) Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Makamu Mwenyekiti
3. Mhe. Abdul J. Marombwa (Mb.) Bunge la Jamhuri ya Muungano waTanzania Mjumbe
4. Mhe. Suleiman H. Hamisi (MBLW) Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mjumbe
5. Mwalimu Honoratha Chitanda Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mjumbe
6. Ndugu Rakesh Rajani
TWAWEZA Mjumbe
7. Mwalimu Daina W. Matemu Umoja wa Wakuu wa Shule za SekondariTanzania Mjumbe
8. Mwalimu Kizito Innocent Lawa Taasisi ya ElimuTanzania Mjumbe
9. Mwalimu Mabruki J. Makame
Baraza la Elimu Zanzibar Mjumbe
10. Prof. Mwajabu K. Possi
Chuo Kikuu chaDar es Salaam
Mjumbe
11. Mwalimu Nurdin Mohamed Chuo cha Ualimu cha Al-Harmain Mjumbe
12. Ndugu Peter Maduki Baraza la Kikristo la Huduma za Jamii Mjumbe
13. Ndugu Mahmoud A. K. Mringo Chama wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali Mjumbe
14. Ndugu Abdallah H. Mohamed Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar Mjumbe
1. Prof. Sifuni Ernest Mchome Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania Mwenyekiti wa Tume
2. Mhe. Bernadeta K. Mushashu (Mb.) Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Makamu Mwenyekiti
3. Mhe. Abdul J. Marombwa (Mb.) Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
4. Mhe. Suleiman H. Hamisi (MBLW) Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mjumbe
5. Mwalimu Honoratha Chitanda Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mjumbe
6. Ndugu Rakesh Rajani
TWAWEZA Mjumbe
7. Mwalimu Daina W. Matemu Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari
8. Mwalimu Kizito Innocent Lawa Taasisi ya Elimu
9. Mwalimu Mabruki J. Makame
Baraza la Elimu Zanzibar Mjumbe
10. Prof. Mwajabu K. Possi
Chuo Kikuu cha
11. Mwalimu Nurdin Mohamed Chuo cha Ualimu cha Al-Harmain Mjumbe
12. Ndugu Peter Maduki Baraza la Kikristo la Huduma za Jamii Mjumbe
13. Ndugu Mahmoud A. K. Mringo Chama wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali Mjumbe
14. Ndugu Abdallah H. Mohamed Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar Mjumbe
TAARIFA YA TUME YA UCHUNGUZI
6. Mheshimiwa Spika, tarehe 28 Aprili, 2013 Tume ya
Uchunguzi wa Matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012 ilikamilisha kazi yake katika
Awamu ya Kwanza na kutoa Taarifa ya Awali.
Uchambuzi wa Taarifa hiyo ya awali unaonesha kuwa kutokana na Uchunguzi
uliofanyika, kwa muhtasari Tume imebaini mambo muhimu yafuatayo:
6.1 Matokeo ya Kidato cha Nne kuanzia mwaka 2008 yamekuwa
na mserereko wa kushuka kuliko miaka iliyotangulia kwa sababu mbalimbali
ikiwemo changamoto zinazotokana na mafanikio yaliyopo sasa ya kuongezeka sana
kwa Idadi ya Shule za Msingi na za Sekondari, hususan kati ya mwaka 2001 na
sasa (2013); na hivyo kuwa na idadi kubwa ya Wanafunzi waliopo Shuleni.
Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 1961 hadi 2001 Idadi
ya Wanafunzi wa Shule za Msingi imeongezeka kutoka Wanafunzi 486,470 (1961)
hadi 4,875,764 mwaka 2001, sawa na ongezeko la Wanafunzi 4,389,294 katika
kipindi hicho cha takriban miaka 40. Hata hivyo, kati ya mwaka 2001 hadi 2012
Wanafunzi wameongezeka kutoka 4,875,764 mwaka 2001 hadi 8,247,472 mwaka 2012,
sawa na ongezeko la Wanafunzi 3,371,708 katika kipindi cha takriban miaka 11 na
hivyo kufanya jumla ya Wanafunzi wote wa Shule za Msingi kuwa 8,247,472 mwaka
2012.
Kuhusu Shule za Sekondari Idadi ya Wanafunzi imeongezeka
kutoka 11,832 mwaka 1961 hadi 289,699 mwaka 2001 ambayo ni sawa na ongezeko la
Wanafunzi 274,867 katika kipindi hicho cha miaka 40. Lakini kati ya mwaka 2001
hadi 2012 Idadi ya Wanafunzi imeongezeka kutoka 289,699 (mwaka 2001) hadi
1,884,270 mwaka 2012, sawa na ongezeko la Wanafunzi 1,594,571 katika kipindi
cha miaka 11 tu.
Juhudi hizi zimetokana na Mipango mbalimbali iliyoandaliwa
chini ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu wa mwaka 1999. Mipango hii ni
pamoja na:
1. Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) wa mwaka
2002 ambapo:
a) MMEM I ambayo ililenga katika kufungua Shule zaidi ili
Wanafunzi wengi wa rika lengwa waweze kujiunga na Elimu ya Msingi;
b) MMEM II ambayo ililenga katika kuboresha ubora wa elimu
itolewayo katika Shule za Elimu ya Msingi; na
c) MMEM III ambayo ililenga katika kuendelea kuimarisha
ubora wa Elimu ya Msingi baada ya mafanikio ya MMEM I na MMEM II.
2. Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) wa
mwaka 2004 ambapo:
a) MMES I ambayo ililenga katika kufungua Shule zaidi za
Sekondari katika ngazi ya Kata ili Wanafunzi wengi zaidi wanaomaliza Elimu ya
Msingi waweze kujiunga na Elimu ya Sekondari Kidato cha Kwanza ;
na
b) MMES II ambayo ililenga katika kuendelea kuimarisha ubora
wa Elimu ya Sekondari kadri Idadi ya Wanafunzi wa Elimu ya Sekondari
wanavyoendelea kuongezeka.
Changamoto zinazoambatana na mafanikio haya ni pamoja na
mazingira yasiyoridhisha ya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo upungufu wa
miundombinu muhimu ya shule kama vile
Madarasa, Maabara, Madawati, Maktaba, Nyumba za Walimu, Hosteli na majengo
mengine muhimu ya Shule. Vilevile, kuna tatizo la uhaba wa Walimu, Vitabu, zana
za kufundishia na matatizo ya Ukaguzi wa Shule. Vilevile, Tume imebaini kuwa
Mfumo wa Elimu ya Msingi na Sekondari unakabiliwa na changamoto nyingine
mbalimbali ambazo Taifa inapitia kwa sasa ikiwemo masuala ya Kisera, Kisheria,
Kimfumo, Kimuundo pamoja na changamoto za uhaba wa Rasilimali Fedha na
Rasilimali Watu. Tume inaendelea kufanyia kazi maeneo haya kwa kushirikiana na
Wataalamu na Wadau wengine;
6.2 Kuhusu matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012, Tume
imebaini kwamba, pamoja na Wanafunzi hawa kuwa katika mazingira yanayofanana na
ya wenzao wa miaka iliyopita na kwamba ufanisi katika shule kwa ujumla umekuwa
unashuka kwa sababu mbalimbali, ufaulu wao umeshuka zaidi kwa sababu ya
mabadiliko ya mchakato wa kuandaa na kutoa matokeo ya mtihani kwa mwaka 2012.
Mfumo uliotumika mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na
ule uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyotangulia. Uchunguzi unaonesha kuwa
mwaka 2011, Baraza la Taifa la Mitihani lilikuwa linachakata Alama za mwisho
kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika kutegemea hali ya ufaulu wa
Mwanafunzi ambao ni “National Mean Difference” (NMD). Utaratibu huu ulitokana
na tofauti ya Wastani wa Kitaifa wa Alama za Maendeleo kutoka Alama za
Maendeleo Endelevu (Continued Assessment – CA) za Watahiniwa wote na Wastani wa
Kitaifa wa ufaulu wa Mitihani ya mwisho kwa somo husika. Kila Mtahiniwa
aliongezewa “National Mean Difference” iliyokokotolewa katika Alama za Mtihani
wa mwisho ili kupata Alama itakayotumika kupata Daraja la ufaulu. Kimsingi,
kila somo lilikuwa na NMD yake kulingana na Continued Assessment (CA) zilivyo
kwa mwaka husika.
Lakini mwaka 2012 Baraza lilitumia Mfumo Mpya ambao
ulikuwa haubadiliki kutegemea hali ya ufaulu wa Mwanafunzi, yaani kuwa na
Viwango Maalum vya Kutunuku (Fixed
Grade Ranges ).
Tume imebaini kwamba, pamoja na kwamba Mfumo huo uliandaliwa kwa nia nzuri,
Utaratibu huo mpya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya
kutumika.
MAPENDEKEZO YA AWALI YA TUME
7. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia masuala mbalimbali
yaliyojitokeza wakati wa uchunguzi, Tume katika Taarifa yake ya awali imetoa
mapendekezo mbalimbali yakiwemo yale yanayohitaji kutekelezwa kwa haraka.
Kutokana na kuwepo kwa mapendekezo hayo ambayo inabidi yafanyike kwa haraka,
tarehe 29 Aprili, 2013 Baraza la Mawaziri lilipokea Taarifa ya Awali ya Tume na
kuijadili ambapo liliridhia mapendekezo hayo yaanze kutekelezwa mara moja.
Maamuzi hayo ya Baraza la Mawaziri yanalenga kutenda haki kwa Walimu na
Wanafunzi ambao juhudi zao za kufundisha na kujifunza zimepimwa kwa kutumia
Mfumo mpya ambao hawakupata fursa ya kushirikishwa na kuandaliwa. Mapendekezo
hayo ni yafuatayo:
i. Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yafutwe
na yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011;
ii. Standardisation ifanyike ili matokeo ya Wanafunzi
yalingane na juhudi walizoziweka katika kusoma kwa mazingira na hali halisi ya Tanzania na
uamuzi wa Taifa kuongeza idadi ya Shule na Wanafunzi wakati uwekezaji katika
ubora unaendelea;
iii. Baraza la Taifa la Mitihani limeelekezwa kuzingatia
kuwa pamoja na kwamba Sheria ya kuanzishwa kwake inawaruhusu kufanya
marekebisho ya mchakato wa mitihani, lakini marekebisho yoyote ya kubadilisha
Utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya Mitihani,
lazima yahusishe Wadau wote wanaohusika na Mitaala, Ufundishaji na Mitihani.
Wakati Tume inaendelea kukamilisha kazi yake, uamuzi wa
Baraza la Taifa la Mitihani wa kutumia utaratibu mpya wa kupanga viwango vya
ufaulu na madaraja ya matokeo ya Mitihani uliotumika mwaka 2012 usitishwe na
badala yake Baraza la Mitihani litumie Utaratibu wa mwaka 2011 kwa Kidato cha
Nne na cha Sita kwa Mitihani yote ukiwemo utaratibu wa Standardization na kutoa
Matokeo mapya kwa kuzingatia maelekezo haya.
Aidha, mchakato wa Mfumo wa Tuzo wa Taifa (National
Qualifications Framework) na Mfumo wa kutahiniwa/kutathmini maendeleo ya
Mwanafunzi katika masomo yake (National Assessment Framework) ukamilishwe
haraka iwezekanavyo.
UTEKELEZAJI WA MAPENDEKEZO YA TUME
8. Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa mapendekezo
hayo, Baraza la Mawaziri limeamua kwamba utekelezaji wa mapendekezo hayo uanze
mara moja.
9. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchunguzi itaendelea
kukamilisha Taarifa yake vizuri kwa kuhusisha Wadau mbalimbali ili kupata maoni
zaidi na ushauri wao juu ya mambo mbalimbali yaliyobainika wakati wa uchunguzi
kabla ya kuikamilisha na kuitoa kwa matumizi ya Umma na Vyombo mbalimbali.
HITIMISHO
10. Mheshimiwa Spika, Serikali inaipongeza sana Tume kwa kutoa
mapendekezo ya awali ambayo Serikali imeyaridhia. Aidha, Serikali inawashukuru
Wananchi wote na Wadau mbalimbali wa Sekta ya Elimu wanaoendelea kutoa maoni na
ushauri wao kwa Tume.
11. Mheshimiwa Spika, Serikali inawahakikishia Wananchi
kuwa itaendelea kuboresha Elimu Nchini ili kuwezesha Watoto wetu wapate
mafanikio katika maisha na maendeleo yao ,
kwani Wahenga wanasema “Elimu ni Ufunguo wa Maisha”.
12. Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment