Wednesday, May 22, 2013
1.0. UTANGULIZI
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 (kifungu cha 18 (3)) imetoa wajibu kwa tume wa kuunda Mabaraza ya Katiba kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume.
Kifungu cha 17 (8) kinaeleza kuwa, isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo, Tume itabuni utaratibu unaofanana ambao utatumika kila upande wa Muungano.
Kifungu cha 18 (6) kinaeleza aina nyingine ya Mabaraza ya Katiba kwa kueleza kuwa Tume inaweza kuruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya Watu kuwasilisha maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba.
Ikumbukwe kwamba Kamati Maalum ya CHADEMA ilikutana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 7 Januari 2013 kuwasilisha maoni ya CHADEMA kuhusu katiba mpya kama ilivyoalikwa lakini pia kutumia fursa hiyo kuwasilisha mapendekezo ya CHADEMA kuhusu marekebisho na maboresho yanayohitajika kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba ili kupata katiba bora.
Tarehe 31 Januari 2013 Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa kwamba imeamua kuwa Mabaraza ya Katiba yatakuwa katika makundi mawili yafuatayo: Mabaraza ambayo Tume itayasimamia na kukusanya Maoni (Mabaraza ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa) na Mabaraza ambayo Tume haitayasimamia. Mabaraza hayo yatajisimamia yenyewe na kukusanya maoni yatakayowasilishwa kwenye Tume kwa mujibu wa maelekezo. (Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu).
CHADEMA baada ya kupitia muongozo huo na kwa kuzingatia kuwa tayari tume ilishafanya uamuzi kuwa mabaraza ya katiba yatakuwa ya wilaya, tarehe 14 Februari 2013 kiliwasilisha maoni na mapendekezo yake kuhusu uteuzi wa wajumbe ambayo kwa sehemu kubwa hayakuzingatiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo kusababisha matatizo makubwa katika mchakato mzima wa uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya.
Kufuatia hali hiyo katika Maoni ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tulitangaza kwamba CHADEMA itajitoa ushiriki wake katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2013:
“Mosi; Kufutwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata, na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja kwa
moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC;
Pili: Serikali ilete mbele ya Bunge hili tukufu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yatayofanyia maeneo yafuatayo marekebisho.”
2.0 MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU MWONGOZO WA MABARAZA YA ASASI, TAASISI NA MAKUNDI YENYE MALENGO YANAYOFANANA:
Bila kujali upungufu uliokuwepo katika uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa rasimu ya Mwongozo kuhusu Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi yenye malengo yanayofanana; hivyo, CHADEMA kinatoa maoni kuhusu rasimu hiyo kama ifuatavyo:
1. Uendeshaji (2.2) ; makundi yaliyotajwa ni yale yanayoanzia chini mpaka taifa na taifa: wakati ambapo kuna makundi ya ngazi ya chini pekee mathalani taasisi za jumuiya (CBOs), au taasisi iliyosajiliwa kwenye ngazi ya wilaya au hata mitandao ambayo haijasajiliwa, hivyo wigo upanuliwe kuruhusu makundi yote.
2. Utaratibu wa kutambua makundi (3.0); kipengele cha kutaka kuwasilishwe ‘taarifa ya kusudio’ kiondolewe, kinaongeza urasimu hasa kwa kuzingatia kwamba taarifa hizo zinawasilishwa tume makao makuu. Tume ikishatoa muongozo maana yake ni kwamba tayari imefungua mlango kwa makundi kujadili rasimu, hivyo ngazi pekee itayobaki iwe ni 4.0 ya kuwasilisha maoni. Hatua hii itachelewesha makundi ya kijamii kutumia haki na uhuru wako wa kikatiba wa kujumuika na kuwasilisha maoni.
3. Utaratibu wa kuwasilisha (4.0), maneno “Tarehe zitazoelekezwa na tume ya mabadiliko ya katiba” katika sentensi ya kwanza, kwa sababu inaweza kuleta tafsiri ya kwamba tume itayapangia tarehe za kukutana mabaraza hayo ya makundi ya kijamii ambayo kimsingi ni kuyaingilia. Tume ipange tu tarehe ya mwanzo wa kupokea maoni na mwisho wa kupokea maoni kwa awamu ya mabaraza. Tarehe ya kuanza uendeshaji imeshatajwa kwenye 2.2 “wakati wowote kuanzia tarehe itayotangazwa na tume”, tarehe ya mwisho wa kuwasilisha maoni imewekewa utaratibu kwenye 4.0 “ maoni yatawasilishwa kwa tarehe zitazoelekezwa na Tume”; hivyo sentensi hiyo ya kwanza haina haja ya kuwepo.
4. Uzito wa maoni (6.0), maelezo ya kwamba ‘maoni yatakuwa na uzito ulio sawa’, yanapaswa kufafanuliwa; kwa mantiki ya sentensi hii ni kwamba makundi yenye malengo yanayofanana hata yawe mengi kiasi gani yatakuwa na uzito sawa na mabaraza yatayosimamiwa na tume ambayo tayari yameshalalamikiwa kwamba yana hodhi ya chama kimoja na hayana uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi. Hivyo, tafsiri itolewe ambayo itahakikisha kwamba maoni ya wengi na matakwa ya umma yatatamalaki.
5. Tume kualikwa kusikiliza; Pamoja na kwa mujibu wa kipengele 2.2 mabaraza ya makundi yenye malengo yanayofanana ‘yatajisimamia na kujiendesha yenyewe’, pawepo na kipengele kwamba iwapo asasi, taasisi au kundi husika linaweza kuomba tume itume maafisa wake kuangalia/kusikiliza moja kwa moja ziada/zaidi ya utaratibu uliotajwa kwenye 4.0
3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO JUU YA MASUALA MENGINE KUHUSU UENDESHAJI WA MABARAZA NA UTOAJI MAONI JUU YA RASIMU:
Aidha, pamoja na maoni kuhusu muongozo; CHADEMA kinatoa maoni ya ziada kwa Tume kuzingatia yafuatayo:
· Muongozo wa kwanza uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ulihusu “Muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake”.
Hata hivyo, muongozo uliotolewa ulijikita katika muundo wa mabaraza na mchakato wa uteuzi wa wajumbe wa mabaraza hayo, lakini haujatoa maelezo na maelekezo ya kutosha kuhusu namna mikutano ya mabaraza ya katiba ya wilaya itavyoendeshwa na utaratibu mzima utakaotumika kujadili rasimu ya katiba mpya katika mabaraza hayo.
Aidha, CHADEMA kinapendekeza kwa mara nyingine kwamba tume itoe muongozo mwingine mahususi kuhusu uendeshaji wa mabaraza ya katiba ikiwemo utaratibu utakaotumika wakati wa kujadili rasimu katika mabaraza; aidha kabla ya muongozo huo kuanza kutumika wananchi wapewe nafasi ya kutoa maoni na mapendekezo kama ilivyokuwa kwa muongozo huu kuhusu uteuzi wa wajumbe.
· Kwa kuwa mpaka awamu ya nne ya ukusanyaji maoni ya wananchi binafsi ilipokamilika wananchi waliotoa maoni kwa njia ya simu walikuwa 16,261 tu kati ya idadi ya wateja wa makampuni ya simu za mkononi ambao watajwa kuwa zaidi ya milioni 20 (mobile phone subscribers); Tume ya Mabadiliko ya Katiba iweke mfumo wa wananchi binafsi kuweza kutoa maoni kuhusu rasimu ya katiba kupitia simu za mkononi.
CHADEMA kinarudia kutoa mwito kwa tume kushirikiana na makampuni ya simu kuwezesha ujumbe wa simu ya mkononi kutumwa kwenye kila mtanzania mwenye simu kumpa dondoo juu ya rasimu ya katiba na kumpa namba anazoweza kutuma maoni kwa njia ya simu na pia maelekezo ya namna ya kutuma ujumbe wa bure wa maoni yake.
Hii itafanya wananchi wengi kuweza kushiriki kutoa maoni. Aidha, pawepo na uwazi katika mfumo mzima wa maoni yanayokusanywa kwa njia ya simu na mitandao mingine ili kusiwe na uwezekano wa "kuchakachua".
4.0 HITIMISHO:
Pamoja na kuwasilisha maoni na mapendekezo haya izingatiwe kuwa madai ya Kambi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA kuhusu kufutwa kwa chaguzi za mabaraza na kuwasilishwa bungeni kwa muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba katika mkutano wa kumi na moja wa Bunge unaoendelea hayajatimizwa.
Waziri Mkuu aliahidi (wakati wa kuhitimisha hoja ya Ofisi ya Waziri ) kwamba Serikali italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa Bajeti.
CHADEMA kinasubiri ahadi hiyo kutekelezwa katika kipindi hiki ambacho kitaenda sambamba na Tume kutoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya kwa ajili ya kuanza kujadiliwa na Watanzania.
Endapo hadi kufikia mwisho wa kipindi hicho Serikali itakuwa haijaleta Muswada wa marekebisho yanayotakiwa; au endapo Muswada utakaoletwa hautakidhi matakwa ya kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya; basi CHADEMA itawaalika wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania nzima, pamoja na taasisi za kiraia na za kidini, vyama vya siasa na Watanzania wote wenye nia njema na taifa hili kuhamasisha umma kuikataa Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kura ya maoni itakayofanyika kwa ajili ya kuihalalisha Katiba hiyo mbovu.
Naomba kuwasilisha,
John Mnyika (Mb)
Kny. Katibu Mkuu
No comments:
Post a Comment