Friday, May 10, 2013

Sheikh Ponda huru......



Miongoni mwa watuhumiwa katika kesi hiyo akifurahia kuwachiwa huru katika mahakama ya Kisutu jana.



                                                             Kilio cha furaha hiki.

 Watu wakiangalia furaha ya wafuasi wa Sheikh Ponda kutoka upande wa pili wa mahakama, hili ni jengo la Raha.com au Raha Tower.

 Sheikh Ponda katikati akiwa na jamaa zake mara baada ya kuwachiwa huru jana, mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

 Sheikh Ponda akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hukumu yake kuisha kwa mafanikio.


 Miongoni mwa watu waliohudhuria kushuhudia hukumu ya kesi hiyo wakiwa na furaha mitaa ya Posta jana.

Siku ya jana shughuli zote zilisimama kwa saa kadhaa kutokana na idadi kubwa ya wafuasi wa Sheikh huyo kuwa na furaha kupita kiasi wakitoa kauli ya 'Takbiiiir, Allah Akbar"


Dar es Salaam. Furaha zilitawala jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda Issa kuhukumiwa kifungo cha nje cha miezi 12 huku wenzake 49 wakiachiwa huru.
Katika kesi hiyo, Sheikh Ponda na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh59.6 milioni, uchochezi na kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali.
Katika hukumu hiyo, Mahakama ilimhukumu Sheikh Ponda kifungo hicho cha nje kwa kosa moja la kuingia kwa nguvu katika eneo hilo la ardhi isiyo yake.
Hukumu hiyo iliwaachia huru washtakiwa wenzake wote baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Kabla ya hukumu, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka alisema upande wa Jamhuri hauna kumbukumbu za makosa mengine ya jinai dhidi ya mshtakiwa lakini akaiomba Mahakama impe adhabu stahiki kwa mujibu wa sheria.
Akitoa hukumu hiyo iliyosomwa kwa saa 2:12, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Victoria Nongwa Nongwa alisema: “Kwa kuwa mshtakiwa hana rekodi ya makosa ya jinai na kwa kuwa amekaa rumande kwa muda mrefu baada ya DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) kuzuia dhamana yake, ni haki kuangalia muda huo.”
“Hivyo Mahakama chini ya Kifungu cha 25(g) cha Kanuni za Adhabu, mshtakiwa unaachiwa kwa masharti ya kutokutenda kosa kwa miezi 12. Unatakiwa ulinde amani na kuwa na tabia njema katika jamii. Ukishindwa hiyo utarudi hapa kwa adhabu nyingine inayokufaa.”
Awali, Hakimu Nongwa alichambua ushahidi wa mashahidi wote 16 wa upande wa mashtaka na 53 wa utetezi akasema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Alisema umeshindwa kuthibitisha katika kosa la kwanza, la tatu na la nne, yaliyokuwa yanawakabili washtakiwa wote na katika shtaka la tano lililokuwa likimkabili Sheikh Ponda na Mshtakiwa wa tano, Sheikh Mukadam Swalehe ambaye ni Kiongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu.
Katika shtaka la pili, Hakimu Nongwa alisema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa wa kwanza tu, Ponda na kwamba kwa upande wa washtakiwa wengine umeshindwa kuiridhisha Mahakama kuwa walitenda makosa hayo.
Alisema hakuna ushahidi unaoonyesha jinsi washtakiwa hao walivyohusika katika makosa.
Hata hivyo, kwa upande wa mshtakiwa wa tano japo kuna maelezo ya onyo yanayoonyesha kuwa alikiri, lakini akasema maelezo ya onyo tu ya mshtakiwa hayatoshi kumtia hatiani, bali upande wa mashtaka ulipaswa kuweka wazi suala hilo.
Hakimu Nongwa aliponda upelelezi kuwa haukufanyika kwa umakini kiasi kwamba kuna mambo ambayo hayakuwa wazi yaliyoibuliwa na upande wa utetezi, ambayo kama upelelezi ungefanyika kwa umakini, washtakiwa wote wangetiwa hatiani.
“Kuna hisia zinazoonyesha kuwa hawa washtakiwa walishiriki katika makosa haya, lakini sasa Mahakama haiwezi kuwahukumu kwa kushuku tu,” alisema Hakimu Nongwa na  kuionya Jamhuri kujiepusha na mashtaka ya kula njama ambayo hata yenyewe inajua kuwa ni vigumu kuyathibitisha.
Wafurika mahakamani
Mahakama ya Kisutu pamoja na maeneo jirani, jana yalifurika watu waliokuwa wakifuatilia hukumu hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi katika sehemu kubwa ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Magari manane yaliyokuwa yamesheheni askari polisi, mbwa na farasi yalionekana katika eneo la Mahakama hiyo. Mbali ya hao, pia walikuwapo askari kanzu na wengine waliokuwa wamevalia sare.
Wafuasi hao wa Sheikh Ponda walianza kuingia mahakamani hapo saa mbili asubuhi lakini kutokana na askari kuweka kizuizi kwenye lango kuu, wengi waliishia nje.
Baada ya kupata taarifa kuwa Sheikh Ponda ameachiwa, wafuasi hao walishangilia wakisema ‘Takbir! Allahu (Mungu ni mkubwa).’
Furaha ya  wafuasi hao, ilisababisha watu wote waliokuwa ofisini katika majengo yaliyo karibu na Mahakama hiyo pamoja na wapita njia kuacha shughuli zao ili kushuhudia.
Baadhi walitoka nje ya ofisi na majengo ili kufuatilia kwa karibu.
Ponda anena
Mara baada ya kuachiwa, Sheikh Ponda alivitaka vyombo vya dola kuacha kutengeneza kesi nzito ambazo inashindwa kuzithibitisha.
“Kuwepo na mfumo thabiti ambao utafanya kesi zisiwe za kubambika au matakwa ya wanasiasa,” alisema na kuongeza kuwa kuachiwa kwake si fadhila, bali ni haki yake kulingana na misingi ya sheria.
Alisema tatizo linalosababisha kesi kuharibika ni mfumo mbovu na ndiyo maana Tanzania inashirikiana na mataifa mengine katika kufanya upelelezi kama lile la Marekani la FBI na kusema ipo haja ya nchi kuwa na mfumo utakaowezesha kuwa na vyombo makini vya upelelezi.
Baada ya kutoka kortini, wafuasi wa Sheikh Ponda waliandamana hadi Msikiti wa Mtambani, Kinondoni ambako alizungumza nao baada ya kupelekwa hapo na gari la polisi.
MWANANCHI

2 comments:

  1. Kweli huyu mtu anawekwa ndani kwa muda mrefu, anaathirika kisaikolojia, mwisho wa siku anaambiwa hana kosa. Tuweni makini, kwani sio yeye anayeathirika kisaikolojia wapo, familia yake na waumini wenzake.
    Inahitajika washitakiwa nao wanapoonekana hawana hatia walipwe fidia.

    ReplyDelete
  2. Suala kama hili linawakumba watanzania wengi sana, ipo haja mahakama zetu kufikiria namna ya kesi wanazopewa na Jamhuri kuzisimamia.

    ReplyDelete