Hapa mzuka wa Mzee Akilimali ukiwa umepanda anaanza kuzungumza kwa ishara na sauti ya juu.
Hapa akiweka msisitizo.
Na Hafidh Kido
Mabingwa wa soka Tanzania bara Dar es Salaam Young Africans, wametangaza
kutofanya sherehe ikiwa watafungwa na watani wao wa jadi wekundu wa msimbazi
Simba katika mechi itakayowakutanisha uwanja wa taifa Mei 18.
Katika mechi hiyo yenye
ushindani mkubwa ambayo ndiyo itafunga pazia la ligi kuu ya soka vodacom Tanzania bara,
Yanga wamejitapa kuwafunga Simba kwa idadi ya mabao ambayo hawakuyataja lakini
wakiweka wazi kuwataka waamuzi wa mechi hiyo kufuata sheria 17 za mchezo huo.
Akizungumza na waandishi wa
habari makao makuu ya klabu hiyo leo mchana katibu wa wazee wa Yanga, Mzee
Ibrahim Akilimali alisema katika mchezo huo lazima wawachinje wapinzani wao ili
kuongeza furaha ya ubingwa.
“Kwanza
tunawashukuru viongozi wetu kwa kutuongoza vema mpaka tumenyakua ubingwa msimu
huu, wanachama na wachezaji wana imani kubwa na uongozi wao. Lakini ili
kuongeza furaha ya ubingwa huu lazima katika mchezo wa Mei 18 tuwachinje Simba
ili tusherehekee kwa shangwe na vigelegele.
“Mwenye macho haambiwi tazama
timu yetu ni timu bora kuliko timu zote msimu huu, lakini tunaomba kitu kimoja
waamuzi watakaochezesha mchezo huo wanatakiwa kutumia sheria 17 za soka na
tunaahidi tutawafunga kwa kiasi tunachokitaka,” alisema mzee Akilimali kwa
sauti ya kujitapa.
Aidha wakati akijibu maswali
ya waandishi wa habari Mzee Akilimali aliyezungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa
wazee wa Yanga, Alhaj Jabir Makatundu alisema mchezo wa msimu uliopita dhidi ya
watani wao ulijawa na mizengwe mingi pamoja na kukosa umakini kwa waamuzi kiasi
wakafungwa mabao matano, lakini msimu huu Simba wasitegemee makosa yale yatajirudia.
“Ule mchezo wa msimu uliopita
haukuchezeshwa ‘fair’ haiwezekani mchezo mmoja uwe na offside 18, Yanga
tulionekana tumeotea mara nyingi zaidi mpaka wale watangazaji wa Supersport
walishangaa, ndipo wakaambiwa hao ni Simba na Yanga mambo kama
hayo ni ya kawaida.
Mjumbe mwingine mzee Hashim
Mwika aliongeza kuwa msimu uliopita Yanga walifungwa na Simba kwasababu wazee
hawakuwa radhi na uongozi ndiyo maana laana yao ikawafanya wachezaji wasiwe na umakini
uwanjani.
“Wazee tulivua kofia ndiyo
maana Yanga ilikubali kipigo cha mabao mengi kiasi kile, wazee tuliiwachia
radhi klabu lakini msimu huu tupo vizuri na kila idara inashirikiana vilivyo
kuhakikisha tunafanya vizuri,” alisema.
Katika hatua nyingine mzee
Akilimali anayefahamika kwa vituko alipoulizwa swali na KIDOJEMBE juu ya
wapinzani wao kuweka kambi Zanzibar alijibu; “Huo ni uoga, uoga ndiwo
unaowafanya kuweka kambi Zanzibar, sisi tutabaki hapahapa Dar es Salaam tena
tutaweka kambi yetu hapahapa klabuni hatuogopi kitu, na tukifungwa na Simba
hata hiyo sherehe yenyewe hatufanyi itakuwa haina maana.”
Msimu uliopita yanga
ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa Simba na Azam FC
walioshika nafasi ya pili. Kitu kilichoibua simanzi kubwa ni pale Simba
walipochukua ubingwa kwa mbwebwe na kuwafunga watani wao mabao 5-0.
Mabao hayo yameonekana kuwapa
kiwewe Yanga hasa ikizingatiwa walikuwa na migogoro ya kiuongozi, lakini msimu huu
Yanga wamejipanga vizuri wakatangaza ubingwa mapema na kuwaacha watani wao
wakigombania nafasi ya tatu huku nafasi ya pili ikikaliwa na Azam FC walewale.
HAFIDH KIDO
Kidojembe @gmail.com
+255 713 593894
+255 752 593894
DAR ES SALAAM , TANZANIA
10 MEI, 2013
No comments:
Post a Comment