Thursday, May 30, 2013

Sakata la wabunge wa Kenya kujiongezea mishahara.

Rais Wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa kauli kali kupinga hatua ya wabunge wa Kenya kutaka kujiongezea mishahara. Rais Kenyatta amesema kuwa taasisi zote za serikali na afisi zingine zote za umma zitafuata mapendekezo yaliyotolewa na tume ya kudhibiti mishahara bila upendeleo wowote.

Wabunge wa Kenya wamekuwa wakilumbana na tume hiyo wakidai imewanyanyasa kwa kuwapunguzia mishahara yao.
Taarifa zinazohusiana

Kenyatta emesema malumbano kati ya wabunge na tume hiyo imelemaza kazi za serikali na kwa hilo rais Kenyatta emewataka wabunge kukomesha kero zao kwa kushirikiana na tume ya kudhibiti mishahara ili kuelezea malalmiko yao kwa kufuata sheria.

Mapema Jumanne tume hiyo ya mishahara , ilitoa onyo kwa makarani wa bunge wenye jukumu la kuwalipa mishahara wabunge kuwa huenda wakapatikana na hatia ya kutumia vibaya mamlaka yao na kufuja pesa za umma ikiwa watawalipa mishahara ya juu wabunge kinyume na ile iliyowekwa na tume hiyo katika gazeti rasmi la serikali.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Sarah Serem ameonya kuwa makarani wa bunge la taifa Justin Bundi na yule wa Senate, Jeremiah Nyegenye huenda wakapatikana na hatia ya matumizi mabaya ya mamlaka ikiwa watakiuka agizo hilo.

"katiba inatupa mamlaka ya kudhibiti mishahara ya maafisa wa serikali. Na hivyo ndivyo tulivyofanya,'' alisema mwenyekiti wa tume hiyo Bi Serem.

Bi Serem alisema kuwa tume hiyo ilichapisha mishahara watakayopokea wabunge kwenye gazeti rasmi la serikali kwa ilikuwa kwa nia nzuri.

"SRC haikushurutishwa kuchapisha taarifa hiyo katika gazeti rasmi la serikali. Lakini tuliamua kufanya hivyo kwa nia njema na ili wananchi waweze kupata habari hiyo.'' aliongeza Bi Serem

Tume hiyo hata hivyo iliwapongeza Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kwa kusisitiza kuwa serikali ipunguze matumizi ya pesa za uma.

Bi Serem alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa na wawili hao ili kutenga pesa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Onyo la tume limekuja siku moja baada ya wabunge kupiga kura kupinga tangazo la tume hiyo kwenye gazeti rasmi la serikali kuhusu kiwango cha pesa watakachopokea wabunge.

Tangazo hilo lilisema kuwa kila mbunge atapokea shilingi laki tano za Kenya ambazo ni dola elfu sita. Wabunge hao wanapigania kulipwa dola elfu kumi na kuwafanya kuwa miongoni mwa wabunge wanaopokea kiasi kikubwa sana cha mishahara duniani
BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment