Tuesday, May 14, 2013

Maskini, Wilfred Lwakatare......


Dar es Salaaam. Jitihada za mawakili wa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare, kumchomoa mahabusu, jana ziligonga mwamba na sasa atalazimika kuendelea kusota mahabusu hadi Mei 27 mwaka huu.
Mawakili hao wa Lwakatare jana waliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, impatie dhamana, Lwakatare baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kumfutia, mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili yeye na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura, ambayo hayana dhamana.
Juzi mmoja wa mawakili hao, Peter Kibatala aliliambia gazeti hili kuwa walikuwa wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa wangeweza kumtoa kwa dhamana kwa kuwa walikuwa tayari wamekamilisha masharti ya dhamana.
Hata hivyo, jitihada zao ziligonga mwamba kufuatia kitendo cha hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Aloyce Katemana, kutokuwapo mahakamani na hivyo kusababisha kesi hiyo kuahirishwa hadi Mei 27.
Mapema, Wakili Mkuu wa Serikali, Prudence Rweyongeza aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilikuwa imepangwa kwa ajili ya kutajwa na kuomba ipangiwe siku nyingine ya kutajwa.
Hata hivyo, Wakili Kibatala aliiomba mahakama impe dhamana Lwakatare huku akirejea uamuzi wa Mahakama Kuu, kuwafutia mashtaka ya ugaidi na kubakiwa na shtaka la kula njama ambalo kisheria linadhaminika.
“Pamoja na kwamba hakimu mhusika hayupo, lakini tunaomba dhamana kwa kuwa tunaamini kuwa mahakama yako inaweza kutoa dhamana kwa kuzingatia kuwa dhamana ni haki na hasa kwa kuzingatia kuwa amekaa mahabusu kwa muda mrefu na afya yake (Lwakatare) si nzuri,”alidai Wakili Kibatala.
Hata hivyo, Wakili Rweyongeza alipinga maombi hayo ya dhamana akidai kuwa yametolewa nje ya muda kwa mujibu wa taratibu.
Pia alidai kuwa uamuzi wa mahakama unaanza baada ya mkurugenzi wa mashtaka, kuwasilisha maelezo ya kesi.
Wakili Kibatala alipangua hoja hizo akidai kuwa hoja za Wakili Rweyongeza zinalenga katika kuondoa haki ya dhamana na kwamba hakuna pingamizi lolote la kisheria.
Huku akitoa mifano ya kesi kadhaa wakili huyo alisisitiza kuwa hata katika hatua hiyo mahakama inaweza kutoa dhamana wakati taratibu nyingine zikiendelea.
Hata hivyo, Hakimu Sundi Fimbo alisema kwa kuwa yeye si hakimu anayesikiliza kesi hiyo hawezi kuamua lolote na kwamba anachokifanya ni kurekodi hoja za pande zote kwenye jalada la kesi.
Aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 27, mwaka huu.
Juzi Wakili Rweyongeza aliliambia gazeti hili kuwa wanasubiri kupata nakala ya uamuzi wa Mahakama Kuu, kuhusu kuwafutia mashtaka ya ugaidi ili waweze kuona hatua ambazo wanaweza kuzichukua, kama ni kukata rufaa au la.
Katika hatua nyingine, mahakama jana iliwaacha solemba wafuasi wa Chadema baada ya kusikiliza na kuahirisha kesi hiyo bila wao kujua.
Wafuasi hao wa Chadema walikuwa wamefurika katika ukumbi wa mahakama namba mbili wakisubiri kesi hiyo, lakini wakati wakisubiri katika ukumbi huo, kesi hiyo ilikuwa ikiendelea katika ‘chamber’ ya Hakimu Fimbo hadi ilipomalizika.
Lwakatare na Rwezaura walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manne, matatu kati yake yakiwa ya ugaidi na moja la jinai ya kawaida.
Mashtaka hayo yalikuwa ni kula njama, kupanga kumteka Dennis Msacky na kisha kumdhuru kwa kutumia sumu na kufanya mkutano wa vitendo vya kigaidi.
Hata hivyo Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka hayo matatu ya ugaidi na kubakiwa na shtaka moja tu la kula njama za kutenda kosa la kumdhuru Msacky kwa kutumia sumu.
Uamuzi huo wa Mahakama Kuu ulitokana na maombi ya jopo la mawakili wa Lwakatare waliyoyawasilisha mahakamani hapo wakiiomba ipitie uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka, kuwafutia kesi ya awali na kisha kuwakamata na kuwafungulia tena kesi ya mashtaka hayohayo.
 MWANANCHI

No comments:

Post a Comment