Taarifa kwa Mwananchi Jumapili iliyotolewa Alhamisi wiki hii na
Taasisi ya Tafiti Kukabiliana na Magonjwa ya Mzio na Kuambukiza (NIAID) ya
nchini Marekani ilieleza kuwa mfumo wa kifaa hicho siyo tu utasaidia
kurahisisha chanjo kukabiliana na VVU, bali hata kwa magonjwa mengine
yanayosababishwa na virusi kama mafua na yale yanayosababisha uvimbe wa ini.
“Ni mfumo wa hali ya juu wenye uwezo wa haraka wa kuchambua
chembechembe kinga zenye uwezo wa kuangamiza aina mbalimbali za VVU
zinazopatikana duniani,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliyoambatanisha majina ya wanasayansi nguli wa
NIAID ambao wamethibitisha kifaa hicho chenye mfumo mpya katika teknolojia ya
kuchambua VVU, umeweka wazi kuwa matatizo waliyokuwa wakipata wanasayansi
katika kudhibiti virusi sasa imepata ufumbuzi.
Uzuri wa kifaa hicho unaelezwa kwamba ni kuweza kuchambua na
kutofautisha chembe kinga za aina mbalimbali, hata kujua idadi na uwezo wake
katika kushambulia adui katika mwili wa binadamu.
“Uchambuzi wa kifaa hiki unaweza kutumika kuchunguza namna mwili
wa binadamu unavyoweza kukabili maradhi mengine yanayosababishwa na virusi kama vile mafua na uvimbe wa ini,” anaeleza sehemu ya
taarifa hiyo.
Wanasayansi nguli wa NIAID waliothibitisha uwezo wa kifaa hicho
ni Mtaalamu wa Dawa na Mifumo ya Kibiolojia, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya
Chanjo, Profesa Peter Kwong na Mkuu wa Idara ya Kinga, Profesa John Mascola.
Wataalamu hao wanaeleza kuwa kifaa hicho kina uwezo wa
kutofautisha ni chembechembe gani za kinga zenye uwezo wa juu katika kukabili
virusi vya maradhi.
Kupitia njia hiyo, inaelezwa kuwa ni rahisi kubaini chanjo yenye
nguvu, hivyo kuharakisha upatikanaji wa chanjo itakayothibitishwa kukabiliana
na VVU.
Kulingana na teknolojia na tafiti mbalimbali, VVU bado hajaipata
tiba au chanjo madhubuti, ingawa wameweza kupata dawa zenye uwezo mkubwa wa
kupunguza makali ya virusi hivyo (ARVs).
Hadi sasa tafiti mbalimbali zimeonyesha uwezekano wa kupatikana
tiba na chanjo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kwa sasa tafiti nyingi zipo kwenye majaribio, NIAID inaeleza
kuwa kupatikana kwa kifaa hicho kutaharakisha kazi ya kuchanganua uwezo wa chanjo
hizo katika kukabiliana na VVU.
Taasisi hiyo ya utafiti inaeleza kuwa mfumo wa kifaa
kilichokuwepo awali, haukuwa na uwezo wa kuchambua kiufasaha chembe kinga
mbalimbali wala umahiri katika kukabiliana na virusi.
“Hata hivyo, kwa sasa itakuwa rahisi kuchambua sampuli za damu,
hata kutofautisha makabiliano dhidi ya virusi kulingana na makusudio yetu.
Awali hatukuwa na teknolojia ya kufanya hivyo,” ilieleza sehemu
ya taarifa hiyo ya NIAID.
Kwa jinsi kifaa hicho kinavyofanya kazi, walikifananisha na
mashine ya kutambua alama za vidole kinachoweza kutofautisha watu bila kukosea.
Kulingana na taarifa ya watafiti hao, kifaa hicho kina uwezo wa
haraka wa kufanya kazi hata kwa kutumia kiwango kidogo cha damu, kuliko njia
nyingine zozote.
Ugonjwa wa Ukimwi iligundulika miaka 30 iliyopita, hadi sasa
umeua watu wengi na kusababisha kupungua kwa nguvukazi pamoja na wataalamu wa
sekta mbalimbali hasa katika nchi maskini.
Kauli ya Serikali
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid ameelezea kuwa ugunduzi huo ni ukombozi kwa dunia katika kuharakisha upatikanaji wa chanjo ya VVU.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid ameelezea kuwa ugunduzi huo ni ukombozi kwa dunia katika kuharakisha upatikanaji wa chanjo ya VVU.
“Ni jambo zuri hasa katika kuharakisha upatikanaji huo wa
chanjo… Maana virusi (VVU) hawa wamekuwa na tabia ya kubadilikabadilika, hata
kufanya iwe kazi ngumu kupata antibodies (chembe kinga) watakaosaidia mwili
kupambana na virusi wa Ukimwi,” alisema Dk Rashid.
Alikiri kuwa zipo tafiti mbalimbali za chanjo ya Ukimwi duniani,
lakini zimekuwa zikisuasua kutokana na ugumu wa vifaa madhubuti vya kuchunguza
mwenendo wa chembe kinga, hata uwezo wake, hivyo kazi hiyo kuchukua muda mrefu.
Dk Rashid akasema, ugunduzi kama
huo ni muhimu kwa wakati huu ambapo kuna juhudi za kutafuta tiba na chanjo ya
Ukimwi.
Kuhusu juhudi za Serikali kupata kifaa hicho ili kuharakisha
shughuli za utafiti nchini, Dk Rashid alisema kuwa taratibu zake ni hadi pale
kitakapothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Alisema vifaa vyovyote vinavyohusiana na tiba vinaweza kuingizwa
nchini baada ya kupata maelezo na umuhimu wake katika kulisaidia taifa kwa
uthibitisho wa WHO.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi
(Tacaids) Dk Raphael Kalinga alisema iwapo wanasayasni hao watakuwa
wamefanikiwa katika hilo
ni mafanikio katika teknolojia ya kukabiliana na VVU.
“Ni hatua nzuri,” alisema Dk Kalinga akisisitiza kuwa ni jambo
linaloinufaisha dunia na hakuna anayeweza kukataa maendeleo.
Pamoja na pongezi hizo, Dk Kalinga alisema ugunduzi wa aina hiyo
utasaidia zaidi, hasa uchunguzi kwa watoto wachanga, ambao kazi yake imekuwa
ngumu ukilinganisha na watu wazima.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment