Waziri mkuu wa Tanzania
Mizengo Pinda, amewataka viongozi wa kisiasa kuacha kuweka ushabiki kwenye
tukio la bomu lililotokea Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita katika kanisa
katoliki.
Akitoa ripoti ya tukio hilo bungeni mjini Dodoma
leo mchana baada ya kutembelea eneo la tukio Pinda alisema tukio hilo ni baya na la
kushitusha hivyo kuwataka watanzania kuwa watulivu na kuwaombea majeruhi wapone
haraka badala ya kuanza kutupiana lawama.
“Ni tukio kubwa, kitendo
kibaya kisichofurahisha hata kidogo na mambo makubwa kama
haya tusiingize siasa wala rusiingize ushabiki tuwape moyo ndugu zetu wa
Arusha. Kwa bahati mbaya wamepitapita viongozi wa kisiasa kule badala ya
kuwafariji wahanga wameingiza visiasa,”alisema Pinda.
Awali akitoa taarifa hiyo
wakati wa mjadala wa bajeti ya wizara ya mambo ya ndani Waziri Mkuu alisema
katika wagonjwa 66 waliopelekwa hospitali ya Mount Meru tayari wagonjwa watatu
wamefariki dunia na wagonjwa 24 wamesharuhusiwa.
Akizungumzia watuhumiwa wanane
waliotiwa mbaroni kuhusiana na tukio hilo Pinda
alisema, “uchunguzi bado unaendelea, mpaka sasa jeshi la polisi linawashikilia
watuhumiwa wanane wane kutoka uarabuni, watatu ni raia wa Tanzania
akiwemo Joseph na Victor Ambroz. Hawa raia wa kigeni walikamatwa wakiwa njiani
kuelekea Nairobi
tunaendelea kuwafanyia mahojiano ili kubaini chanzo ni nini, na tunawaomba watu
wa Arusha watupe ushirkiano katika hili ikiwa kuna mtu mwenye taarifa zozote.”
Mbali ya Waziri Mkuu kiongozi
mwingine aliyetembelea eneo la tukio ni makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilal
ambaye alikwenda siku hiyohiyo ya tukio, kiongozi mwingine anayetarajiwa kufika
jijini Arusha ni Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete aliyekatisha ziara yake nchini
Kuwait ,
kiongozi mwingine ni makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar Seif Sharif Hamad.
Katika tukio hilo bomu la
kurusha kwa mkono lilitupwa katika kanisa la Mtakatifu Joseph, Parokia ya
Olasiti wakati ibada ya uzinduzi wa Parokia hiyo ambapo mgeni rasmi alikuwa ni
balozi wa Vatican nchini Askofu Francisco Mantecillo Padilla aliyekuwa mwenyeji
wa Askofu Josephat Lebulu wa kanisa hilo jimbo la Arusha.
HAFIDH KIDO
7th May, 2013
No comments:
Post a Comment