Sunday, May 12, 2013

Nawaz Sharif aelekea kushinda uchaguzi nchini Pakistan...


Nawaz Sharif

Kiongozi wa chama cha Pakistan cha Muslim League, Nawaz Sharif, amezungumza na wenzake chamani kuhusu namna ya kuunda serikali yake mpya baada ya uchaguzi mkuu wa Jumamosi.
Matokeo yasiyo rasmi yanaonesha kuwa Muslim League itakuwa na viti vya kutosha bungeni kuunda serikali, lakini huenda kikahitaji kuungwa mkono na vyama vengine.
Bwana Sharif, ambaye amewahi kuwa waziri mkuu mara mbili kabla, alisema kuwa watu wameonesha wanaamini kuwa chama chake kinaweza kuleta mabadiliko.
Mcheza kriketi maarufu wa zamani, Imran Khan, ambaye huenda akawa kiongozi wa upinzani, aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi; lakini alisema taarifa za udanganyifu kwenye kura zinavunja moyo.
Chama tawala cha PPP inaelekea kuwa kimeshindwa vibaya.                                                                   Ali Akbar Rafsanjani
     
Nako huko Iran inaelezwa kuwa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Ali Akbar Hashemi Rafsanjani, amejiandikisha kugombea urais katika uchaguzi wa mwezi ujao.
Bwana Rafsanjani mwenye umri wa miaka 78 aliandikisha jina lake dakika chache kabla ya muda kumalizika wa kupeleka maombi.
Mwandishi wa BBC anasema Bwana Rafsanjani ni mpinzani wa viongozi wa msimamo mkali walio karibu na kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.
Mpatanishi mkuu katika mazungumzo kuhusu mradi wa nuklia wa Iran, Saeed Jalili, piya amependekeza jina lake.
Rais anayeondoka madarakani, Mahmoud Ahmadinejad, ameshatumika mihula miwili na hawezi kugombea tena urais.
Wagombea urais watachujwa na halmashauri maalumu, Guardians Council, kabla ya kuruhusiwa kusimama katika uchaguzi.
BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment