Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akitoka kuswali Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni, jana. Picha na Mpigapicha Wetu.
Ponda alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa
akitoa mawaidha ya Ijumaa katika Msikiti wa Mtambani, wilayani Kinondoni.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, kumhukumu kifungo cha mwaka mmoja nje, baada ya kupatikana na hatia ya
kuingia isivyo halali katika eneo la Markazi Chang’ombe.
Alisema kwa muda mrefu Waislamu nchini wamekuwa na madai ambayo
Serikali haijaonyesha dhamira ya kuyashughulikia.
“Waislamu wamekuwa wakinyanyasiki katika nchi yao utadhani wakimbizi, tuna madai ya msingi
ambayo hayahitaji watu kufungwa au kuundiwa kesi kwa hiyo sasa ni wakati wa
Serikali kuunda tume tutakayokwenda kuwaeleza matatizo yetu na vithibitisho
vyake,” alisema Ponda.
Ponda alisema atahakikisha kuwa anawatetea Waislamu ili wapate
haki zao zinazopokwa na baadhi ya watu wasiowapenda waumini wa dini hiyo.
“Wamekuwa wakinitungia njama za kuniondoa kwa misingi ya kuwa
mimi siyo Mtanzania, hakuna wa kuniondoa hapa nchini na nitapambana hadi hatua
ya mwisho na kuhakikisha kuwa Waislamu wanapata uhuru wao,” alinena Sheikh
Ponda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alielezea kusikitishwa kwake juu ya kauli kwamba Sheikh Ponda asingeweza kupata
dhamana katika kesi iliyokuwa ikimkabili.
“Vyombo vyetu haviko makini, tuliambiwa Ponda hawezi kupata
dhamana lakini leo hii amefungwa kifungo cha nje, hii inatia shaka na uamuzi
uliokuwa ukiendelea,” alisema Profesa Lipumba.
Mtaalamu huyo wa uchumi, alitumia nafasi hiyo kuwataka Waislamu
kuungana na kuhakikisha kuwa wanatetea haki zao.
“Tuache unafiki, tuungane na kumsikiliza Ponda kwa kauli zake,
matendo yake ili kufikia kile ambacho Waislamu wanakitaka,” alinena Profesa
Lipumba.
Umati mkubwa wa waumini wa Kiislamu walimiminika kutaka kusikia
mawaidha ya katibu huyo kwa mara ya kwanza baada ya kutoka gerezani juzi.
Katika tukio hilo , waumini pia walichanga fedha kwa ajili
kumwezesha Sheikh Ponda kugharimia matibabu ya afya yake na sehemu ya fedha
hizo walipewa mawakili wake ili wafanye maandalizi ya kukata rufaa.
Pia Mei 18 mwaka huu, waumini hao wamepanga kufanya dua (Itikafu) itakayofanyika katika msikiti huo kwa ajili ya kumwombea Sheikh Ponda na wenzake.
Pia Mei 18 mwaka huu, waumini hao wamepanga kufanya dua (Itikafu) itakayofanyika katika msikiti huo kwa ajili ya kumwombea Sheikh Ponda na wenzake.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment