Roma, Italia
Kauli ya waziri wa kwanza
mweusi nchini Italia kuhusu kujivunia kuzaliwa mweusi imezua mjadala mkubwa
nchini humo baada ya kudhamiria kujibu maneno ya ubaguzi wa rangi na jinsia dhidi
yake.
Cecilia Kyege mzaliwa wa
Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya uteuzi wake kuwa waziri anayeshughulikia
masuala ya ubaguzi wiki iliyopita alitangaza anajisikia fahari kuwa mweusi na
kwamba Italia si kweli kuwa ni nchi ya ubaguzi.
Waziri huyo ambaye alifika
Italia mwaka 1983 akiwa na umri wa miaka 18 tu anasema alikwenda Italia kwa
lengo la kusoma lakini akaona ni mahala pazuri kuendesha maisha yake.
Waziri Mkuu mpya wa Italia
Enrico Letta aliamua kuweka kitu tofauti katika baraza la mawaziri baada ya Jumamosi
iliyopita kumfanya Kyege kuwa mmoja wa wanawake saba katika serikali mpya.
Tangu kuteuliwa kwake kushika
wadhifa wa waziri anayesimamia masuala ya ubaguzi, Kyege amekuwa akiandamwa na
maneno ya udhalilishaji kwenye tovuti mbali kuhusiana na asili yake. Baadhi ya
majina mabaya anayobandikwa katika tovuti ni kama
"tumbili wa Kongo", "Zulu" na "Mweusi mpinga
Italia".
Aidha waziri huyo anapata
wakati mgumu kutokana na maneno ya kibaguzi na udhalilishaji kutoka kwa mbunge
wa jumuiya ya Ulaya Mario Borghezio, ambaye ni mwanachama wa (pro-devolution
League) ya Kaskazini, ambayo imekuwa na ushirika katika siku za nyuma na
aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi.
Borghezio amekwenda mbali
zaidi na kusema Waziri Kyege hafai kushika wadhifa huo kwani hana sifa za
uwaziri ila anapendeza kuwa mama wa nyumbani.
Mbali ya shutuma hizo
anazokumbana nazo waziri huyo ameendelea kuweka msisitizo wake kuwa Italia si nchi
ya kibaguzi na ana mpango wa kuandaa taarifa maalum katika bunge la nchi hiyo
ili kuundwa kwa sheria ambayo itaweza kuruhusu watoto waliozaliwa Italia na
wazazi wahamiaji kupata uraia wa moja kwa moja badala ya kusubiri mpaka kufikisha
umri wa miaka 18 ili kuomba.
"Mimi niliwasili nchini
Italia peke yangu nikiwa na umri wa miaka 18, na siamini katika kukata tamaa
mbele ya vikwazo," alisema Kyenge ambaye hataki neno mrangirangi
‘coloured’ linalotumiwa juu yake katika ripoti nyingi kwenye vyombo vya habari
vya Kiitaliano, "Mimi si mrangirangi, mimi ni mweusi na nasema kwa kiburi
kuwa ni mweusi."
Waziri Kyenge, ambaye ameolewa
na Mtaliano mweupe amesema yeye hakuwa na mtazamo hasa kama
Italia ni nchi ya ubaguzi wa rangi, na kuamini kwamba mitazamo ya uhasama
inatokana na ujinga.
"Italia ina desturi ya kukaribisha
wageni na sadaka ya ukarimu kwa watu wengine. Tunahitaji kutambua mila hizi na
kuzitumia siku hadi siku, "alisema.
Wakati akizungumza na gazeti
moja la Italia waziri huyo alisema tangu kuteuliwa kushika nafasi hiyo
ameshapokea ujumbe mwingi wa vitisho vya kifo dhidi yake, nyingine zikiwa ni
ujumbe wa udhalilishaji wa kingono katika mitandao kwa lengo la kumfanya akose
umakini katika kazi yake mpya.
Cecilia Kyenge Kashetu
amezaliwa Agosti 28, 1964 katika mji wa Katanga kijiji cha Kambove, nchini Kongo
(DRC) kitaaluma ni daktari wa macho na mwanasiasa, ambaye ameolewa mwaka 1994
na mhandisi Domenico, pia wamejaaliwa kupata mabinti wawili Julia na Maisha.
Anaishi katika mji wa
Castelfranco Emilia, ana shahada ya Madawa na upasuaji kutoka Chuo Kikuu cha
Cattolica del Sacro Cuore mjini Roma. Pia ni mtaalamu katika ‘ophthalmology’
katika Chuo Kikuu cha Modena
na Reggio Emilia.
HAFIDH KIDO
12 May, 2013
DAR ES SALAAM , TANZANIA
No comments:
Post a Comment