Monday, July 2, 2012

Historia haipotoshwi iwacheni ijitetee.


Na Hafidh kido
Nimesoma makala nyingi  katika magazeti ya siasa kuhusu historia ya mapinduzi Zanzibar , kadhalika nimepata kushuhudia malumbano ya hoja juu ya uhalali wa Mwalimu Nyerere kupewa jina la baba wa Taifa, ilhali kwa maelezo ya wapinga hayo wanasema wapo watu ambao walistahili kupewa hadhi hiyo lakini si Nyerere .
Kitu kinachonipa tabu ni kimoja, hivi mtu anaweza kupindisha historia kweli? Naamini katika kipindi hicho kulikuwa na wasomi na watu makini wenye uwezo wa kutunza kumbukumbu na kuandika kila kinachotokea. Sasa huku kusema historia imepotoshwa kunatoka wapi kama si kujitafutia umaarufu.
Ambacho nilitegemea mtu kuandika ni kusema ‘tukumbushane katika historia’ hivyo mtu ambae kwa kipindi kirefu alikuwa akiamini tofauti atakaa chini kutafakari na kuisoma upya historia na si vinginevyo. Kuliko kuanza kushutumu watu kwa kusema hili lilikuwa hivi lakini matokeo yake sasa linatamkwa hivi.
Kwa mfano, kuna waandishi na wanahistoria wakongwe sitowataja humu,  ambao kwa kipindi kirefu nimeshuhudia makala zao za malumbano juu ya uhalali wa hayati Mwalimu Nyerere kuwa muasisi wa harakati za uhuru Tanganyika . Mmoja katika waandishi hao anadai udini ndiwo uliofanya majina ya wazee wa Dar es Salaam kama Abdulwahid Sykes, Dossa Azziz na wengi ambao walikuwa waasisi wa chama cha TAA na wakamkaribisha Nyerere katika mapambano hayo mwaka 1952, lakini matokeo yake sasa wao hawatajwi tena.
Hapa nina swali, hivi mtu kutajwa pia unaomba? Mimi naamini katika shughuli yoyote inayohusu mapambano lazima kutakuwa na kiongozi, ninachotaka kujua ni kuwa kwa kipindi hicho kulikuwa na viongozi wangapi, na tutakuwa na mababa wa taifa wangapi katika taifa moja, ama hao wapambanaji katika kupata uhuru kimetokea nini mpaka wakasahauliwa na historia.
Ninavyofahamu  jamii haifichwi na kitu ipo siku ukweli utadhihiri na utaumbuka, lawama nyingi ametupiwa Mwalimu Nyerere kwa kuwasahau wazee waliomfadhili wakati wa mapambano,naamini wazee walimfadhili Nyerere ili baadae wajukuu zao waje kunufaika na si wao kunufaika mmoja mmoja. Ila kama kuna tafsiri nyingine ya msaada ule waliokuwa wakimpa Nyerere basi naomba nisahihishwe.
Kwa upande wa visiwani Zanzibar wapo watu wanalalamika kuwa Karume hakuwa jemedari wa mapinduzi matakatifu ya mwaka 1964, na kuwa wapo watu ambao kihalali ndiwo waliopasa kuwa vinara wa kutajwa katika mapinduzi hayo. Kwa kifupi mapinduzi yalipindua vinara wa mapinduzi.
Hapa nataka kujua kitu, hivi wewe utakuwaje kinara wa mapinduzi halafu upinduliwe ndani ya siku mbili kisha jina lako lisahauliwe kabisa  litajwe jina la mtu mwingine ambae hata hakushiriki kushika japo kisu cha kupakia siagi katika mkate wakati wa kitahanana cha mapinduzi.    Hili siafikiani nalo tena hata kidogo.
Inatajwa kuwa John Okello mwenye asili ya Uganda ama Kenya , sina hakika; Maana historia inamtaja hata kushiriki vita ya ukombozi ya MauMau Kenya , lakini jina hili naliona lina asili ya moja ya makabila ya Uganda .
Bwana huyu anatajwa kuwa ndie alikuwa jemedari wa mapinduzi na ndie alietangaza mapinduzi hayo, ni kweli na nasadiki kwa mujibu wa vitabu vya historia na hata kutoka midomoni mwa watu walioshuhudia na kushiriki mapinduzi hayo kuwa Okello ndie aliekuwa jemedari wa mapinduzi na kuyatangaza.
Lakini hiyo haimaanishi Karume hakuhusika na mapambano, si lazima awe ameshika bunduki lakini mipango pia ni mapambano, sasa mbona huyo Okello baada ya kuyatangaza mapinduzi alitamka kumuita Karume aje achukue nchi yake. Jemedari gani wa mapinduzi anamuita mtu legelege aje achukue nchi ambayo hata hajashiriki kuipindua?
Najua watu watasema hata Karume hana asili na Zanzibar , lakini yeye kwa mujibu wa wabobezi wa historia alikuja Zanzibar akiwa mgongoni mwa mama yake, hii peke yake inaonyesha alikuwa chini ya miaka mitatu. Sasa mtoto alieanza kuishi katika nchi tangu akiwa na miaka mitatu mpaka kufikia umri wa kuoa na kuzaa pia akapata kushiriki shughuli za kisiasa na kuwa mwenyekiti wa chama kikubwa cha siasa cha wakati huo Afro-Shirazi Party (ASP), utasema vipi hana asili ya nchi hiyo.
Watu hupenda kuvuruga akili changa za vijana kwa kupandikiza chuki za kihistoria, naomba niseme watu hawa waiache historia ijiteteee yenyewe, naamini hakuna mtu anaeweza kuvuruga ama kutia mkono wake katika jambo linalohusu historia.
Kuna maandiko mengi sana hasa ya waandishi wa nje ambao walipata bahati ya kuzuru Tanganyika na Zanzibar kwa vipindi tofauti, majina ya Karume na Nyerere ndiyo yanayotamkwa katika harakati za uhuru wa maeneo yote mawili ambayo kwa kipindi hicho yalikuwa ni mataifa mawili tofauti.
Nikiri kuwa hao wanaotajwa na waumini wa kupinga ukweli kuwa ndiwo waliostahili hadhi walizonazo viongozi wawili hawa Karume na Nyerere, nao ki hakika wana haki ya kutajwa kama washiriki katika mapambano, lakini hadhi hiyo mbona wamepewa!
Tanzania bara kwa mfano, mitaa, barabara kuu, kumbi ama sehemu fulani za kiserikali na maeneo ya nchi yamepewa majina  ya watu hao. Na hiyo ndiyo njia pekee ya kuwakumbuka wapambanaji hao, na kwa kukumbusha tu wale ambao walikuwa na elimu ama ufahamu wa mambo ya kimataifa walipewa nafasi katika serikali ya awamu ya kwanza kama mabalozi, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya na nafasi nyingine ambazo walistahili wao kupewa kulingana na uwezo wao.
Nadhani watu wanaamini mtu kukumbukwa na Rais wa nchi mpaka ujazwe mapesa, ama ukoo wako uheshimike kama ukoo wa kifalme kwa kuwa tu ulikuwa ukimpa nauli muasisi wa nchi hii ama ulikuwa ukinywa nae kahawa na uliwahi kusafiri nae gari moja wakati mkihudhuria moja ya mikutano ya kutafuta uhuru, basi tu nawe utajwe kama kiongozi wa mapambano ya uhuru wa Tanganyika. Si hivyo jamani.
Kwa sababu hata katika hotuba ya mwanzo ya Mwalimu mbele ya baraza la mawaziri 11 wa mwanzo wa Tanganyika huru alitamka kuwa wananchi ndiwo wenye mamlaka juu ya baraza lile na serikali kwa ujumla, wao ni kama watumishi tu na watafuata kila ushauri mzuri watakaopewa na wananchi.
Hii inadhihirisha kuwa kila kilichofanyika kwa ajili ya Tanganyika kupata uhuru ilikuwa ni ihsani ambayo malipo yake ni kuhakikisha watu wote bila kujali ushiriki wao katika kupata uhuru wananufaika na matunda ya kuwa huru na si vinginevyo.
Sitaki kuamini kuwa watetezi hao wa kupinga hadhi ya Nyerere katika Tanzania walitaka Mwalimu apite kila eneo aangalie watu wote waliomsaidia basi nae atie mkono mfukoni na kuwasaidia, uungwana hautufundishi hivyo. Unaposaidia kitu tena hasa katika masuala ya kitaifa usitegemee malipo, we subiri rehema ya Mungu kama huyo mtu atakukumbuka fahuwa kama atakusahau basi amini ulichofanya ni kwa lengo moja tu la kuhakikisha Tanganyika inaondoka katika makucha ya wakorofi wa kizungu.
Kadhalika wapo watu wanaomshutumu Mwalimu na suala la udini, mimi ni Muislamu na ninasimamia katika imani yangu sitetereki, ila kusema Mwalimu Nyerere alichukia waislamu na ndiyo maana aliwasahau wazee wa Dar es Salaam kwa kuwa ni waumini wa dini hiyo hilo halina ukweli hata kidogo.
Naomba niseme ikiwa wazee wa Dar es Salaam waliona maslahi yao yasingetimia kwanini wasingeendelea na harakati zao za kutafuta uhuru ilhali walikuwa na watu wasomi tena waliobobea katika fani zote, maana waislamu tunaamini mtu aliesoma elimu ya dini ya kiislamu anakuwa na maarifa makubwa kuliko mtu yeyote.
Kwanini walipata tabu ya kumtafuta mkatoliki Julius Nyerere, ambae hata mitaa ya Dar es Salaam aliokuwa haijui. Ikadaiwa Abdulwahid Sykes akajikosesha uenyekiti wa TAA makusudi ili Nyerere ashinde kiti hicho mwaka 1953, kwanini aliamua kufanya yote hayo? Maana yake mzee wangu Abdulwahid Sykes ambae namuheshimu sana katika mapambano ya uhuru wa Tanganyika , aliona umuhimu na uwezo wa Nyerere wazungu wanaita ‘potential.’
Hivyo kuitwa kakwe baba wa taifa ni halali kabisa maana hao wazee na viongozi wa TAA ndiwo waliompa ‘green light’ Nyerere na mpaka leo tunamuita hivi tunavyomuita.
Niseme tu kuwa makala haya hayajalenga kumkosoa mtu yeyote, mimi ni mchanga wa historia lakini ni mwanafunzi mzuri wa kukosolewa, hivyo lengo langu ni kujifunza zaidi kwa yule ambae ataona makala haya yamemkwaza. Lakini siku zote historia hufuata kile kilichotendeka historia ni kumbukumbu haipindishwi, na anaejaribu kufanya hivyo ipo siku ataumbuka.
KIDO JEMBE
0752 593895

No comments:

Post a Comment