KAMPUNI tatu za madini zinazoendesha shughuli zake nchini, zimewekewa vikwazo na Serikali ikiwa ni kuzishinikiza kulipa mabilioni ya fedha za kodi inazodaiwa.
Habari zilizopatikana na
kuthibitishwa na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini zimetaja kampuni hizo
kuwa ni Tanzanite One, Mgodi wa Dhahabu wa Geita (Geita Gold Mining Ltd – GGML)
na Kampuni ya Resolute (Resolute Mining Tanzania Ltd).
Kwa pamoja, kampuni hizo
zinadaiwa zaidi ya Dola za Marekani milioni 5.2 (zaidi Sh8.188 bilioni) kwa
viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni wastani wa Sh1,574.74 kwa
Dola moja ya Marekani. Fedha hizo ni malimbikizo ya tozo na kodi mbalimbali
ambazo zilipaswa kulipwa kwa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
Kutokana na hali hiyo,
Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeanza kuchukua hatua dhidi ya
madeni hayo kwa kuzinyima kampuni husika vibali mbalimbali vya kutekeleza
shughuli zao kama hatua ya kushinikiza malipo
hayo.
Kwa upande wa Tanzanite
One, Serikali imeripotiwa kukataa kuhuisha leseni yake ya uchimbaji ambayo uhai
wake ulitarajiwa kumalizika Juni 30, mwaka huu wakati kwa upande wa GGML na
Resolute zinakabiliwa na hatari ya kunyimwa leseni za kusafirisha madini kwenda
nje ya nchi (Export Licenses).
Naibu Waziri wa Nishati
na Madini, Steven Masele alithibitishia kampuni hizo kudaiwa na kwamba Serikali
imeanza kuchukua hatua.
“Lazima tusimamie sheria
na kwa kweli katika hili, Serikali haitanii hata kidogo. Kama
kuna kampuni inadaiwa fedha zozote za umma lazima zilipwe na huo ndiyo wajibu
wetu kwa niaba ya Watanzania,” alisema Maselle.
Tanzanite One
Kampuni ya Tanzanite One
inayoendesha shughuli za uchimbaji wa madini ya vito katika eneo la Mererani
mkoani Arusha, inadaiwa zaidi ya Dola za Marekani milioni mbili kutokana na
kutolipa kodi mbalimbali kati ya mwaka 2004 – 2008.
Kutokana na hali hiyo,
Serikali imezuia kutolewa kwa leseni mpya kwa Tanzanite One hadi itakapokuwa
imelipa au imeanza kulipa deni hilo
pamoja na kutekeleza matakwa mengine ya Sheria ya Madini ya 2010.
Masharti hayo ni pamoja
na kurejesha asilimia 50 ya hisa zake serikalini kwa mujibu wa sheria hiyo ili
zigawanywe kwa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro na kwa wananchi wazawa.
Chanzo chetu katika
Wizara ya Nishati na Madini kilisema leseni ya uchimbaji ya kampuni hiyo
ilitarajiwa kumalizika Juni 30, mwaka huu na kwamba hadi juzi, ilikuwa
haijapewa leseni mpya na ilitakiwa kutimiza masharti iliyopewa kwanza.
No comments:
Post a Comment