Wazungu wa
unga wabuni njia za siri kuwakwepa polisi
Na Hafidh
Kido
Kila kukicha
mbinu mpya za uingizaji na usambazaji dawa za kulevya nchini hubuniwa na wauza
dawa hizo maarufu ‘mazungu ya unga’, kwa lengo la kukwepa vyombo vya usalama.
Raia mwema
limeweza kuibua mbinu mpya inayotumiwa na wauzaji wadogowadogo wa dawa hizo
maarufu ‘mapusha’ ambao si rahisi kuwafahamu kwani ni vijana wanaoishi katika
jamii na kushiriki katika shughuli zote za kijamii.
Mbinu hiyo
ni kutundika jozi ya viatu vinavyopendwa na vijana aina ya ‘All Star’katika
nyaya za umeme kwa lengo la kuonyesha kuwa eneo hilo dawa zinapatikana. Uchunguzi wa Raia
Mwema, umebaini kuwa katika wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam mbinu hiyo
inatumiwa sana katika maeneo ya Tandale,
kinondoni mkwajuni, msasani, Kinondoni B katika mitaa ya Wibu, Togo na Ufipa.
Ni vigumu
kuamini lakini juhudi za gazeti hili ziliweza kukutana na mtumiaji wa dawa hizo anaeishi mtaa wa Wibu
Kinondoni ambae hakutaka jina lake
litajwe gazetini alisema;
“Sina
uhakika sana na
mbinu hiyo ya kutundika ‘All Star’ juu ya nyaya za umeme kuwa ni alama ya
kuuzwa mdude (dawa za kulevya), lakini naweza kukubaliana na maneno yako kwani
maeneo yote kunakouzwa ‘mdude huwaga’ nakuta alama hiyo.
“Zamani
tulikuwa tunaiga wamarekani kutundika ‘All Star’ katika nyaya za umeme, sasa
hata sijui kuna uhusiano gani na biashara hii. Ila naweza kukuthibitishia kuwa
ni kweli kila kunapouzwa ‘mdude’ huwa kuna viatu aina ile,” alimalizia.
Raia Mwema,
ilijaribu kumtafuta kijana mmoja anaeishi mtaa wa Togo Kinondoni B ambae
alitajwa na mtumiaji huyo kuwa ndie ‘pusha’ muuzaji wake; ingawa nae alikiri
kutofahamu chochote kuhusiana na alama hizo kutumika na wauzaji, ila alipobanwa
na maswali alisema;
“Mimi naona
tu maeneo mengi ninapokwenda kununua ‘busta’ (kifuko cha dawa za kulevya chenye
uwezo wa kuzalisha kete 200 mpaka 250), huwa nakuta ‘All Star’ zimetundikwa juu
ya umeme lakini kiukweli sijui maana yake nini.
“Kwa mfano
mtaa wa Ufipa karibu na ofisi za CHADEMA kuna dogo ‘anabana mzigo’ (anauza dawa)
pale au ukienda bonde la mkwajuni pembeni ya barabara utakuta viatu vingi vipo
juu ya umeme pale pia kuna jamaa wanabana mzigo,” alisisitiza muuzaji huyo kwa
sharti la kutotajwa jina lake
kuhofia kukamatwa.
Ilibidi
gazeti hili livae uhusika na kuamua kuingia katika kijiwe cha wauzaji na
watumiaji dawa dawa hizo katika mtaa wa Ufipa Kinondoni makaburini, hali
aliyokutana nayo mwandishi wa gazeti hili ni mbaya sana kwa watumiaji wa dawa hizo.
Asilimia
kubwa ni vijana wadogo kati ya miaka 15 mpaka 25, mazungumzo yanayotawala
vijiwe hivyo ni namna ya upatikanaji wa pesa kwa njia ya wizi ama kujadili
jaribio la wizi lililoshindikana ama kufanikiwa.
Mwandishi alifanikiwa
kujifanya kama mtumiaji kwa kubadili sauti yake na kuwa kama
mvutaji ila ujanja uliotumika ilikuwa ni kununua kete na kudanganya kuwa
atakwenda kuvutia chumbani kwake ili kupoteza malengo. Cha kufurahisha ni kuwa
eneo hilo nalo
kulikuwepo viatu hivyo juu ya nyaya za umeme, mwandishi alipouliza maana ya
alamaa hiyo majibu yalikuwa hivi;
“Si unajua
tena wana wanapenda kujifananisha na unyamwezini (Marekani), hii haina maana
yoyote mbwembwe tu za kujifanya nao wako mbele,” alijibu mmoja wa watumiaji
wale huku akijitahidi kuutafuta mshipa wa kujidunga dawa hizo.
Lakini
mwandishi alipojaribu kudadisi mvutaji mwingine alisema; “Unajua mwana nini huu
mdude hauhitaji alama mimi nikisikia (alitaja jina la muuzaji wa kijiwe hicho)
anauza mdude nitamwambia mwenzangu, na huyu atamwambia yule basi wateja wote
utashangaa wanakufata hata saa sita ya usiku.”
Timu yetu
haikuishia hapo bali ilikwenda katika ofisi za
kikosi cha kupambana na dawa za kulevya nchini na kukutana na kamishna
msaidizi mwandamizi wa polisi, ambae ni mkuu wa kitengo cha kudhibiti dawa za
kulevya nchini Godfrey Nzowa, na kueleza kuwa anazo taarifa za kila mbinu mpya
inayotumiwa na wauzaji wakubwa na wadogo wa dawa za kulevya nchini, kwani wana
vijana wao katika kila eneo linalosifika kwa biashara hiyo.
“Hiyo mbinu
nimeisikia kutoka kwa vijana wangu, lakini nasi pia hatuna uhakika nayo kwani bado
ni mpya ila tutaufanyia kazi utafiti wenu,” alisema Nzowa.
“Sisi
tunafuata sheria ya kudhibiti dawa za kulevya sura ya 95 ‘The drugs and
prevention of illicit traffic in drugs’ ambayo inaegemea sana katika waingizaji kuliko watumiaji na
wasambazaji, ingawa upande huo nao hatuufumbii macho,” aliongeza.
Akifafanua
juu ya madhara kwa watuamiaji afande Nzowa, alieleza kuwa mtumiaji anatumia
gramu 0.11 mpaka 0.01 ambayo hiyo ni kete moja, akatoa mfano mtu akiingiza kilo
moja ya dawa za kulevya ataharibu idadi kubwa ya watu wapatao milioni.
Hata hivyo
kwa mujibu wa afande Nzowa jeshi la polisi linakumbana na changamoto za kukosa
fungu la kutosha kutoka serikalini pamoja na wanajamii kwani alidai wauzaji wa
dawa za kulevya ni watu wenye uwezo mkubwa kifedha.
“Mwaka jana
tulikamata kilo 264 za heroin ila mwaka huu mpaka kufikia mwezi wa tano
mwishoni tumeshakamata kilo 250; utaona tatizo halipungui bali linazidi
kuongezeka, na sababu kubwa ni kukosa ushirikiano kutoka kwa raia wema hasa
kukosekana kwa elimu ya kutosha,” alisisitiza.
Nzowa, ambae
ndie mkuu wa kitengo hicho kwa jeshi la polisi alidai kuwa vijana wake ambao
wapo chini ya kikosi kazi kilichoundwa na Rais Kikwete mwaka 2006 ili kukomesha
uingizwaji na uuzaji wa dawa hizi wamesambazwa katika maeneo yote yanayoonekana
ni tishio kwa biashara hiyo na sehemu zote za usafiri kuanzia bahari, hewa na
barabara.
“Vijana wetu
wapo kila sehemu na wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha biashara hii
inakoma, kwa mfano jiji la Dar es Salaam maeneo
yaliyoshamiri biashara hii ni Mzizima, Mafia, Wibu , Togo
na Mandazi Road
Msasani. Maeneo yote hayo tuna watu wetu ambao wanatupa taarifa kila asubuhi,”
aliongeza Nzowa.
Nae kamishna
wa tume ya kudhibiti dawa za kulevya Christopher Shekiondo, alikiri kuwepo kwa
elimu ndogo ya vita dhidi ya dawa za kulevya na kulalamikia fungu dogo
wanalopata kutoka serikalini.
“Kazi yetu
ni kuratibu namna ya kutoa elimu dhidi ya dawa za kulevya na kuwafikia waingizaji,
wasambazaji na watumiaji lengo likiwa ni kujenga urafiki na kuwaeleza ubaya wa
biashara hii. Lakini kazi hiyo inahitaji pesa nyingi kwani kuweza kuwafikia
watu wote hao lazima uwe na kiasi cha kutosha.
“Hatuhusiki sana na wauzaji
wadogowadogo wala watumiaji, kazi hiyo tumewaachia wenzetu wa jeshi la polisi mashirika
yasiyo ya kiserikali sisi ni waratibu tu,” alidai Shekiondo.
Ingawa
alikiri kuwa yapo mashirika ya nje yanayowapa msaada wa kifedha na kimbinu
lakini wananchi nao wanapaswa kusaidia vita hii kwani mara nyingi wauza dawa za
kulevya wanapoonekana na utajiri wa haraka husifiwa katika jamii.
“Biasharaa
hii inaonekana kuwavutia vijana wengi kwani ina utajiri wa haraka, zipo nchi
zinatoa hukumu ya kifo lakini unasikia kila siku watu wanakwenda. Tumeamua na
sisi kuweka adhabu kali iwe fundisho.
“Adhabu ya
sasa ni kifungo cha miaka isiyozidi ishirini lakini April mwaka huu bunge
lilipitisha sheria mpya sidhani kama Rais ameshaitia saini lakini ikikamilika anaekamatwa
na dawa za kulevya za viwandani kama madras,
cocaine ama heroin adhabu yake itakuwa ni kifungo cha maisha,” alisisitiza
Shekiondo.
Tatizo la
dawa za kulevya nchini limekuwa sugu hasa ikizingatiwa ni biashara inayohusisha
watu wenye pesa nyingi wengine wakiwa viongozi wa juu serikalini.
Lakini mwaka
2006, Rais Kikwete aliamua kutangaza vita dhidi ya wauzaji dawa za kulevya, na
miaka ya hivi karibuni aliingia katika mzozo na viongozi wa dini kwa kudai kuwa
atawataja vigogo wa dawa za kulevya miongoni mwao wakiwa ni viongozi wa dini.
Kwa
kuonyesha kikosi kazi cha Rais Kikwete kipo makini wiki iliyopita walikamatwa
raia wawili wa kigeni Edwin Swen kutoka Liberia
na Benjamin Anuorah kutoka Nigeria ,
ambao walikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere
wakielekea nchini Liberia
kupitia Kenya
ambapo walikamatwa na pipi 150 wakiwa wamezimeza tumboni.
Taarifa
iliyotolewa na ofisi ya kamishna msaidizi Godfrey Nzowa, inaeleza kuwa pipi
hizo kwa pamoja zilikuwa na thamani ya Tsh 109,395,000/= watuhumiwa hao
walikuwa wakiendelea kutoa pipi nyingine tumboni.
KIDO JEMBE
0752 593894
No comments:
Post a Comment