WAKAZI wa Jiji la Dar es Salaam hususan
maeneo ya karibu ya Barabara ya kwenda Morogoro wametakiwa kukaa chonjo
kutokana bomoabomoa itakayozikumba nyumba mbalimbali ili kupisha upanuzi wa
barabara hiyo kwa urefu wa kilometa 200 kutoka jijini kwenda Morogoro.
Waziri wa Ujenzi, Dk
John Magufuli alisema hayo jana alipozungumza kwenye mahafali ya nne ya Chuo
Kikuu cha Mtakatifu Joseph, Kitivo cha Uhandisi na Teknolojia jijini hapa.
Alisema barabara hiyo
inatarajiwa kujengwa njia sita umbali wa kilometa 200 kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.
Waziri aliwatahadharisha
watu waliojenga kwenye hifadhi ya barabara waanze kuondoka ili kupisha upanuzi
huo kabla hawajaondolewa kwa nguvu.
“Wote waliojenga kwenye
hifadhi ya barabara waanze kujiandaa kuondoka kwasababu sheria ni
msumeno,”alisema Dk Magufuli.
Akizungumzia wahitimu
walitunukiwa shahada na stashahada jana hiyo, aliwataka wahitimu hao kwenda
kufanya kazi kwa kusimamia sheria na kuzikabili changamoto zilizopo katika
jamii.
“Mkubali changamoto hata
kama ni kwa kulaaniwa maana ni afadhali kuuawa
kwa kukataa rushwa kwasababu utakuwa umelikomboa taifa,”alisema.
Pia alimwagiza
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakandarasi, Profesa Ninatubu Lema kuwapatia usajili
wanafunzi wote waliohitimu chuoni hapo na wale wanaoendelea na masomo ili
watakapokuwa wanatafuta kazi wasisumbuliwe.
Alisema hadi sasa kuna
wahandisi 11,400 waliosajiliwa na makandarasi 9,126. Pia waziri huyo alitoa
zawadi ya Sh1 milioni kwa wahitimu waliofanya vizuri katika masomo yao .
No comments:
Post a Comment