Tuesday, August 14, 2012

Habari mseto kutoka BBC Swahili leo.


Nchini Saudi Arabia tayari kuna vyuo vikuu, afisi na hata migahawa inavyowatenganisha watu kutokana na jinsia zao.
Kwa sasa tayari mji mmoja wa viwanda unaonuiwa kuwa wa wanawake pekee ujulikanao kama Hofuf umeanza kustawishwa Mashariki mwa taifa hilo.
Serikali imeahidi kuwa miji mingine ya wanawake pekee itajengwa katika maeneo mengine ya nchi.
Juhudi hizo ni mojawapo ya mipango ya Serikali ya kutoa nafasi nyingi zaidi za kazi kwa wanawake ambao wanashikilia asilimia 15 pekee ya wafanyakazi nchini, ingawa wanawake wengi zaidi ndio wanaofuzu na vyeti vya shahada ya kwanza katika vyuo vikuu kuwazidi wanaume.
Mkereketwa wa haki za wanawake nchini Saudi Arabia, Reem Asaad, anasema kwamba wanawake wanapendelea zaidi kufanya kazi wakiwa mbali na wanaume.
Alisema mwamko huu mpya ni sehemu moja ya mpango maalumu wa kuwapa uhuru wa kifedha zaidi wanawake katika himaya hiyo.
Chanzo BBC Swahili.

Naibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusiana na Maswala ya Kibinadamu, Valerie Amos, anatarajiwa kutembelea Syria na Lebanon, katika juhudi za kuimarisha misaada kwa waathiriwa wote wa mapigano kati ya Serikali na makundi ya waasi nchini Syria
Kulingana na ratiba ya Umoja wa Mataifa, Bi Valerie Amos, atatembelea Syria na Lebanon kuanzia leo tarehe 14 hadi 16, Agosti, mwaka huu.
Ziara hiyo ya siku tatu inatazamia kumulika hali ya kibinadamu inayozorota nchini Syria na jinsi inavyoathiri wale walio nchini humo au wale wanaotorokea mataifa jirani, kukiwemo Lebanon.
Hali nchini Syria imezorota majuma machache yaliyopita kufuatia kusambaa kwa mapitano katika mji mkuu wa Damascus na Aleppo na katika miji mingine pia. Inadaiwa kuwa zaidi ya watu milioni mbili wameathiriwa na mapigano hayo na zaidi ya milioni moja wametimuliwa kutoka makaazi yao nchini Lebanon.
Zaidi ya watu 140,000 wametoroka na kuingia katika mataifa jirani ya Lebanon, Jordan, Uturuki na Iraq.
Katika ziara yake nchini Syria, Bi Amos anatarajiwa kujadiliana na maafisa wa Serikali jinsi jamii ya kutoa misaada inavyopaswa kuimarisha ugawaji wa misaada kwa waathirika wa mapigano hayo. Wale watakaoshirikishwa katika mashauriano ya kuimarisha misaada nchini humo watakuwa maafisa wa Serikali, tawi la Syria la Mwezi Mwekundu na mashirika mengine ya kutoa misaada.
Nchini Lebanon, Bi Amos atakutana na familia za waliotoroka Syria na kujadiliana na Serikali na makundi ya kutoa misaada ya kibinadamu nchini humo jinsi wanavyopaswa kusaidia wakimbizi.
Ziara hii ya Bi Amos imefanywa wakati ambapo wapiganaji nchini Syria wameonyesha kwenye vidio walioisambaza kwenye mtandao wakionyesha jinsi walivyoangusha ndege ya kijeshi ya Serikali ya aina ya Mig 23. Picha hizo zinaonyesha rangi na alama zinazothibitisha kama ndege za jeshi la Syria.
Chanzo BBC Swahili

Vatican imeamuru bawabu wa zamani wa Baba Mtakatifu Benedict ashtakiwe kwa wizi wa nyaraka za siri kutoka ofisi binafsi ya Baba Mtakatifu.
Paolo Gabriele na mfanyakazi mwingine wa Vatican Claudio Sciarpelletti wanashutumiwa kuiba hundi yenye thamani ya dola za kimarekani laki moja.
Bawabu huyo alikamatwa mwezi Mei mwaka huu kufuatia uchunguzi wa taarifa za shutuma za rushwa katika mako makuu Vatican ya kanisa katoliki duniani.
Amekiri kufanya wizi wa nyaraka hizo akisema kuwa alidhani alikuwa akilisaidia kanisa kwa kufichua maovu hayo.
Chanzo BBC Swahili

No comments:

Post a Comment