Friday, August 3, 2012

Jamani eennhh...?!!! leo jembe kakumbuka enzi zake za mshairi atiii....


(1)Hakuna Mkamilifu
Kunradhi waungwana, watungaji maarufu
Napenda yangu kunena, maneno ya tahalifu
Kuaridhia sufufu,
Sufufu wenye maana, ndio ninowaarifu
Siyo wanaojivuna, kumkiuka Latifu
Hakuna mkamilifu, kila mtu kapungua

Kwa wazee na vijana, bingwa na sahaulifu
Wakarimu na hiana, bozi na hao kumbufu
Walioijaza kufu,
Kufu ya kuridhiana, walio hai na wafu
Walio kisaidiana, kwa mambo matambulifu
Hakuna mkamilifu, kila mtu kapungua

Ni vema kuambizana, hapana mkamilifu
Mkamilifu Rabana, Muumba wetu Raufu
Kauli hii sadifu
Sadifu amini sana, ndio kweli sadikifu
Kwa mlimwengu hakuna, jaza yetu ni pungufu
Hakuna mkamilifu, kila mtu kapungua

Hakuna kubishana, kujifanya takilifu
Tumwachie Subuhana, isemavyo misahafu
Vitabu vitakatifu
Vitakatifu twaviona, bashiri hilo nasifu
Dhana nyingine hapana, huo ndio upunjufu
Hakuna mkamilifu, kila mtu kapungua

Mathias Mnyampala (Diwani ya Mnyampala 1962)

(2)Mtu Bora
Mtu bora mwelekevu, ni mwiko kuwa na chuki
Na shida kuwa mtovu, katika mambo ya haki
Mtu bora hana wivu, wala choyo hakitaki
Wala si mtu mvivu, na kwa wote ni rafiki
Na kwa hivi ana nguvu, daima katika dhiki

(3)Tulivyo
Haji duniani mtu apendavyo,
Wala haondoki kama atakavyo,
Hanayo hiari ya kufanya hivyo,
Hawezi kusema kuwa hivi sivyo,
Lakini Mwenyezi ni aamruvyo,

Mwenyezi hakika ni aamruvyo,
Hatuwezi kukana ikawa sivyo,
Wala kunena ya kuwa hivi ndivyo,
Hiyo ndiyo namna sisi tulivyo,

Na namna yetu ikiwa ni hivyo,
Ni wajibu wetu kufuata vivyo,
Ndipo tuwapo watu kama tulivyo,
Kuwa juu yetu Mungu huwa ndivyo,
Mfadhili wetu kumkana sivyo,

(4)Ulimwengu wa kelele
Kila mtu ana kima, cha chini au kilele
Watu wengine wazima, wengine wana uele
Wengine wana heshima, wengine kajichokele
Wengine wana lawama, wengine thawabu tele
Na wengine wako nyuma, na wengine wako mbele
Ndivyo ulivyo daima, ulimwengu wa kelele
 
Kila kiumbe tazama, ana namna ya hali
Ambavyo ukiipima, tafauti hukabili
Kila mtu ana dhima, na mashaka mbalimbali
Maisha yetu ni bima, tunacheza na ajali
Kisha yaweza kukoma, bila kuwa na muhali
Mauti yatutazama, katika kila mahali

Shaaban Robert ( Mwafrika aimba 1969)

(5)Wakati
Twakimbizana na muda, mfano wendawazimu
Twenda mbio kama punda, au farasi kuzimu
Yametuvimba mafunda, kwa kutamani vitamu

Tunaoneana choyo, kwa uchache wa elimu
Zimetukauka nyoyo, kwa tabia zetu ngumu
Twafanya mambo ambayo, hutenda machakaramu

Kila kitu hakifai, wachache wamestakimu
Kwa pepeo la matlai, jahazi hufika lamu
Kwenda kutafuta rai, kwa mamufti na imamu

(6)Mambo hubadilika
Dunia kigeugeu, na mambo hubadilika
Pazima hupata ngeu, pabovu kusalimika
Shibe hufuata mbweu, wa njaa huyayatika

Wa juu hushuka chini, mwerevu huadhirika
Imamu mshika dini, hukosa kuwaidhika
Mara akenda motoni, kwa dunia kumteka

Muovu hupata njia, hafula akaongoka
Pasipo kutarajia, mwamini akapotoka
Njia uliyokujia, kurudia si mwafaka

Mjuvi akikosea, mjinga huelimika
Machache ya kudasia, hujaa yakafurika
Mwema mshika wosia, mara hiyo hugeuka

Subira mwanzo wa heri, na shufaa kadhalika
Saburi huleta mazuri, mabaya kukuepuka
Ajabu hupendwa shari, mama mzaa dhihaka

Ibada na uongofu, sababu ya kuumbika
Kufuru mambo machafu, maudhi kwa mtukuka
Ila twashiba udufu, udhalili na mashaka

Sala na ibada njema, funguo za kuongoka
Kufuata ya karima, huepusha kudhurika
Ajabu tuna nakama, maovu tumeyashika

Hafidh a. Kido 2011



No comments:

Post a Comment