FRIDAY, AUGUST 3, 2012
Leo tarehe 03 Agosti 2012 kwa mujibu wa
Kanuni ya 68 (7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge na kwa kuzingatia kuwa
marekebisho yamefanyika kwenye ratiba ya bunge ambapo Mkutano wa Bunge sasa
umepangwa kuahirishwa tarehe 16 Agosti 2012 na hoja za wabunge zimeondolewa
kwenye ratiba.
Nimeomba muongozo ama Serikali itoe
kauli bungeni ya kutengua tangazo lililotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na
Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ili kuwezesha mafao ya kujitoa
kuendelea kutolewa au uongozi wa Bunge uruhusu niwasilishe muswada binafsi wa
sheria kwa hati ya dharura tarehe 16 Agosti 2012 kwa ajili ya kufanya
marekebisho kwenye sheria husika ili kuruhusu mafao ya kujitoa kuendelea
kutolewa.
Pamoja na hatua hiyo ya kuomba muongozo
nimechukua hatua ya ziada ya kumwandikia Katibu wa Bunge kumweleza kusudio la
kuwasilisha Muswada Binafsi juu ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii
(The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 kwa hati ya dharura
kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).
Lengo la Muswada huo ni kufanya
marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits)
ili kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya
jamii anapoacha kazi na kuhitaji kupewa mafao yake kabla ya kufikisha umri wa
kustaafu kwa hiari (miaka 55) au kwa lazima (miaka 60) au pale anapopata
ulemavu wa kudumu.
Nimeomba kupatiwa ushauri na usaidizi wa
kisheria kwa mujibu wa Kanuni ya 21 (1) (d), (e) na (2) ili kuweza kuandaa
Muswada Binafsi wa Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (1), Taarifa ya Muswada
huo kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (2), hati ya kuwasilisha muswada kwa dharura na
hoja ya kutengua masharti kuhusu muda wa utangazaji wa Miswada ya Sheria kwa
mujibu wa Kanuni ya 81 (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).
Kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (5) masharti
kuhusu muda wa utangazaji wa Miswada ya Sheria yanaweza kuwekwa kando na
kutenguliwa kwa hoja kutolewa na kuamuliwa kama kutawasilishwa Bungeni hati
iliyowekwa saini na theluthi mbili ya Wajumbe wote wa Kamati kama ni Muswada wa
Kamati na kwa Muswada wa Mbunge hati iliyowekwa saini na Wabunge wasiopungua kumi
inayoeleza kuwa muswada binafsi uliotajwa katika hati hiyo ni wa dharura.
Naomba kutoa taarifa kwamba kuanzia
jumatatu tarehe 6 Agosti 2012 nitaanza kukusanya saini za wabunge wanaounga
mkono kuwasilishwa kwa muswada tajwa kwa hati ya dharura kufanya haraka
marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits)
ili kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya
jamii.
Nimeomba pia kwa Katibu wa Bunge kwa
mujibu kifungu cha 10 cha Sheria ya ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Cap 296
R.E 2002 kupatiwa nakala ya taarifa na nyaraka zifuatazo kwa ajili ya kujiandaa
kuwasilisha muswada husika: Social Security Ammendment Act no.5 ya mwaka 2012,
Sheria za Hifadhi ya Jamii zinazohusika, Taarifa na mapendekezo
yaliyowasilishwa na kupelekea kufutwa kwa mafao ya kujitoa (withdrawal
benefits) na maelezo kuhusu hatua ambayo kifungu husika kiliingizwa na hatimaye
kupitishwa na Bunge tarehe 13 Aprili 2012.
Pamoja na kuomba taarifa na nyaraka
kupitia kwa Katibu wa Bunge natoa mwito kwa wadau wa mifuko ya hifadhi ya jamii
kutunipatia maoni na mapendekezo kwa ya kuzingatiwa kwenye Muswada Binafsi wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social
Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 katika kipindi cha wiki moja.
Ikumbukwe kwamba kifungu cha kufuta
mafao ya kujitoa kilichozua mgogoro hakikuwepo wakati muswada uliposomwa kwa
mara ya kwanza bungeni tarehe 1 Februari 2012 bali kiliwasilishwa kupitia
jedwali la marekebisho ya Wizara lililowasilishwa tarehe 13 Aprili 2012 bila
malengo na madhumuni yake kuelezwa kwa ukamilifu.
Kupitishwa kwa kifungu hicho
kumethibitisha maneno niliyoyatoa bungeni kuwa tumefika hapa tulipo kutokana na
‘uzembe wa bunge na wabunge’ na kwa hili pamoja na mchango nilioutoa bungeni
kwa maandishi siku hiyo juu ya haja ya kuwa mfumo mpana zaidi wa pensheni na
hifadhi ya jamii (universal pension and social security) pamoja na kuwa
sikuunga mkono kifungu husika kilichoingizwa kinyemela naomba radhi kwa
wananchi wa Ubungo na wafanyakazi kwa kutokuwasilisha jedwali la marekebisho
kupinga kifungu hicho kuingizwa.
Izingatiwe kuwa ili kurekebisha hali
hiyo tarehe 27 Julai 2012 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na
Madini kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Serikali itoe maelezo maelezo
kuhusu taarifa zilizotolewa bungeni tarehe 13 Aprili 2012 kuwa wafanyakazi
ikiwemo wa migodini kupitia vyama vyao walihusishwa kutoa maoni yaliyopelekea
kufutwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits); suala ambalo Chama Cha
Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO) kililikanusha.
Hata hivyo, Waziri wa Nishati na Madini
wakati wa majumuisho ya Hotuba yake tarehe 28 Julai 2012 hakutoa majibu yoyote
bungeni kuhusu suala hilo hali ambayo imesababisha migongano kuendelea katika
migodi mbalimbali kuhusu madai hayo hali ambayo kwa taarifa nilizozipata tarehe
1 na 2 Agosti 2012 inaweza kusababisha migomo migodini. Kufutwa kwa fao la
kujitoa kumelalamikiwa pia na wafanyakazi na wadau wa hifadhi ya jamii katika
Jimbo la Ubungo na katika taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, suala hili na tukio husika
litumike kama rejea ya bunge na wabunge kuikatalia Serikali kuwasilisha
marekebisho yenye athari kubwa kipindi cha mwisho na hivyo wabunge kukosa fursa
ya kupata maoni ya wananchi na pia Serikali itakiwe kuomba radhi kufuatia
kulipotosha bunge kuwa wadau wa hifadhi ya jamii hususan wafanyakazi na vyama
vyao walishirikishwa na kuridhia wakati ambapo wamejitokeza na kukanusha madai
hayo yaliyotolewa na Wizara bungeni.
Kwa upande mwingine kufutwa kwa mafao ya
kujitoa msingi wake haupo kwenye marekebisho ya sheria yaliyofanyika tarehe 13
Aprili 2012 pekee bali ni udhaifu katika mfumo mzima wa kisera na kisheria wa
hifadhi ya jamii nchini hali ambayo inahitaji wadau kutaka mabadiliko makubwa.
Hivyo, naungana na wote wenye kutaka
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kutengua
taarifa kwa umma iliyotolewa ya kueleza kuwa “kufuatia kuanza kutumika kwa
Sheria hiyo (ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa
kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka
na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau”.
Aidha, pamoja na Mamlaka kueleza
kwamba sitisho la fao la kujitoa si kwa sababu za Kiserikali au Mifuko
kufilisika ni vizuri mamlaka ikaeleza kwa uwazi na ukweli sababu zingine za
kufanyika kwa marekebisho hayo zaidi ya ile ya kutimiza malengo ya Hifadhi ya
Jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa Mwanachama anapostaafu anapata mafao bora
yatakayomwezesha kumudu hali ya maisha ya uzeeni. Tahadhari za Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa za Hesabu za mwaka 2010/2011 na miaka
mingine zinaashiria masuala ya ziada ambayo yanaweza kuwa yameisukuma Serikali
kuja na mbinu zingine za kuhakikisha uendelevu wa mifuko ikiwemo kupitia
marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii.
Tafsiri ya marekebisho ya ratiba
yaliyofanyika ni kuwa hoja binafsi niliyoiwasilisha kwa katibu wa Bunge kutaka
bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka za kuboresha
upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka haitapata nafasi ya
kujadiliwa bungeni. Aidha ratiba hiyo mpya hoja binafsi iliyoelezwa kuwa
itawasilishwa na Mbunge wa Kisarawe Seleman Jafo kuhusu kufutwa kwa mafao ya
kujitoa kufuatia marekebisho ya sheria za Hifadhi za Jamii nayo haitawasilishwa
kwenye mkutano huu wa Bunge unaoendelea kama
ratiba haitafanyiwa marekebisho.
Hata hivyo, izingatiwe kuwa chanzo cha
kufutwa kwa mafao ya kujitoa ni marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii hivyo
ufumbuzi wa kurejesha fao la kujitoa unapaswa kuwa ni marekebisho ya sheria
hatua ambayo njia ya haraka ya kuifikia ni kuwasilishwa kwa muswada wa sheria
ama na serikali au kamati au mbunge badala ya hoja binafsi.
Hoja binafsi inaweza kuwezesha bunge
kujadili na kupitisha maazimio ya kuitaka Serikali kuwasilisha marekebisho ya
sheria au kuishauri na kuisimamia serikali na mamlaka zake katika utekelezaji
wa sheria lakini sheria itaendelea kuwa palepale mpaka marekebisho
yatakapofanywa kwa kuwasilishwa muswada wa sheria hatua ambayo nimeamua
kuanzisha mchakato wa kuwezesha ichukuliwe.
Wenu katika kuwawakilisha wananchi,
John Mnyika (Mb)
03/08/2012
Bungeni-Dodoma
No comments:
Post a Comment