Monday, August 6, 2012

Leo nilikuwa na siku nzito sana tangu nianze kazi ya uanahabari..... nitawaletea mkanda mzima kwa mfumo wa picha..

Ndugu zangu,

Leo tuliitwa na Badra Masoud, msemaji wa shirika la umeme TENESCO kuenda ofisi zao za ilala jengo la wizara ya nishati na madini saa tatu asubuhi  kwa ajili ya taarifa kwa vyombo vya habari.

Naam, tuliondoka ofisini kwa gari za shirika hilo la ugavi wa umeme nchini tukaelekea eneo la mwananyamala A, tukamkamata jamaa mmoja anahusika na kuuza umeme na kuunganisha watu umeme kwa njia za wizi.

Bwana huyo anaitwa Ibrahim Said, ndie aliekutwa ofisini na bosi wake anaitwa Mussa Hajji, ambao kwa pamoja wanaendesha kampuni ya usambazaji na uunganishaji umeme inayoitwa 'No Voltage Distribution Contractors'. Kwa maelezo yake ni kuwa kampuni hiyo ina miaka saba katika biashara hiyo haramu ya kuuza na kuunganisha umeme.

Cha kushangaza kwa mujibu wa majirani na mjumbe wa eneo hilo kwa muda wote huo hakuna hata mtu mmoja aliekuwa akijua hao jamaa wanafanya biashara gani.

"Sisi hatujui anafanya nini hapa, tunaona tu kila siku anakuja na kufungua ofisi sisi hatuna habari nae. kama alikuwa anauza umeme ndiyo tumejua leo," alieleza jirani wa bwana huyo anaeitwa Aziza Salum.

Aidha mjumbe wa eneo hilo la Mwananyamala A maarufu tawi la chama cha wananchi CUF, Said Ramadhan, alisema "Mimi ninaiona ofisi hii kwa miaka mingi inafika kumi, na hawa mabwana hata siku moja sikupata kujua shughuli wanayofanya. Unajua mimi nikiwa mjumbe sihusiki na kujua shughuli za watu mpaka nitakapopata mashaka kuhusiana na aina ya mizigo unayoingiza mtaani kwangu," alisema.

Hata hivyo Shirika la Tanesco halikuweza kujua ni hasara kiasi gani kampuni hiyo imewasababishia mpaka hapo wataalam wao watakapofanya tathmini ya kina kuhusiana na Units za umeme zilizopotea.

Watu hao walikutwa na vifaa vyote vya tanesco ikiwemo nyaraka za kuunganisha umeme kwa watumiaji wapya, nguo za mafundi wa tanesco, viatu na glovu maalum za kupanda juu ya nguzo za umeme na vifaa nyeti vya shirika hilo.

Hafidh Kido
Dar es Salaam, Tanzania
6/08/2012

No comments:

Post a Comment