Saturday, August 4, 2012

Ufaransa yachukua jumba la mtoto wa Rais wa Equatorial Guinea alilolipata kifisadi....


Wakuu wa Ufaransa wamelichukua jumba lililoko mjini Paris la mtoto wa rais wa Equatorial Guinea.

Hatua hiyo iliyochukuliwa mwezi uliopita, na ndio kwanza kutangazwa, ni sehemu ya uchunguzi unaofanywa juu ya ulaji rushwa.
Jumba hilo la ghorofa 6 liko katika barabara ya Avenue Foch, moja kati ya mitaa ya fakhari ya Paris.
Thamani yake inakisiwa kuwa euro 100 milioni.
Anayemiliki jumba hilo ni Teodoro Nguema Obiang Mangué ambaye anachunguzwa kwa ulaji rushwa na utumizi mbaya wa mali ya umma.
Wakili wake nchini Ufaransa anasema mteja wake ana kinga na hivo hawezi kushtakiwa, kwa sababu hivi sasa ni waziri wa kilimo wa Equatorial Guinea.
Baba ake, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, ni rais.
Equatorial Guinea inatoa mafuta mengi, lakini utajiri wote unadhibitiwa na familia chache.
Familia ya Obiang inashukiwa inatumia mali ya taifa kununua nyumba Ufaransa.
Mwaka jana polisi wa Ufaransa walichukua magari 15 ya fakhari ya Bwana Obiang, mtoto wa rais.
Siku za nyuma wakuu wa Ufaransa wameshutumiwa kuwa hawakusikiliza tuhuma kuhusu mabaya yanayofanywa na viongozi wa Afrika wenye uhusiano mwema na Ufaransa.
Lakini tangu Disemba mwaka wa 2010, majaji wa Ufaransa wamekuwa wakiwachunguza viongozi wa Equatorial Guinea, Congo na Gabon, pamoja na familia zao, na vipi wameweza kumiliki majumba nchini Ufaransa ya thamani ya mamilioni ya euro.

Chanzo: BBC Swahili.

No comments:

Post a Comment