Friday, August 17, 2012

Waislamu na Serikali watunishiana misuli juu ya suala la Sensa...


Ikiwa zimebaki siku chache kuanza kwa zoezi la kuhesabu watu na makazi nchini Tanzania, Waislamu bado wanaendelea kushikilia msimamo wao wa kutoshiriki zoezi hilo la sensa kwa madai kuwa kuna watu wana maslahi na zoezi hilo na ndiyo maana Serikali haitaki kusikiliza agizo la Waislamu.

Akizungumza wakati wa hotuba ya sala ya ijumaa leo katika msikiti wa Kichangani magomeni mapipa, naibu imamu wa msikiti huo Omar Alhadi, alisema “si kama waislamu wanapinga Sensa kwa kuwa ni haramu la hasha, bali yapo mambo ambayo yakirekebishwa waislamu wala hatuna tabu tutashiriki sensa kama kawaida kwa maana sensa si haramu kisheria” alisema.

Hali hiyo imepokewa tofauti na Waziri mkuu Mizengo Pinda ambae alikuwa mgeni rasmi katika sherehe ya ufunguzi wa Sensa iliyoandaliwa leo jijini Dar es Salaam ikiwa ni moja ya njia za kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kulifikia zoezi hilo usiku wa tarehe 26 August mwaka huu. Ambapo Pinda alisisitiza kuwa hakutakuwepo kipengele cha dini ambacho ndicho kinachowafanya waislamu wa Tanznia kususia Sensa.

Awali akizungumza wakati wa sherehe hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadick alisema zoezi la sensa lipo kisheria na yeyote atakaepinga kushiriki atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kuwekwa ndani kwa miezi sita kwa kukaidi amri ya Serikali.

Zoezi hili la kuhesabu watu na makazi limeingia doa baada ya Serikali ya Tanzania kutangaza kuwa Wakristo ni wengi kuliko waislamu nchini Tanzania, hivyo waislamu kuhoji kuwa takwimu hizo walizipata wapi maana katika karatasi za sensa hakuna kipengele cha dini kitakachomuwezesha mtu kujua idadi ya waumini wa dini Fulani.

Hivyo waislamu wakaweka shinikizokuwa ili kuondoa utata wa idadi ya waislamu nchini hawatoshiriki sensa mpaka mamlaka inayohusika na zoezi hilo itakapoweka kipengele cha kumuuliza mtu dini yake ili baadae ijulikane idadi sahihi ya waislamu na wakristo nchini.

HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
17/08/2012
kidojembe@gmail.com    

No comments:

Post a Comment