Friday, July 13, 2012

Dk Slaa aendelea kulivimbia jeshi la Polisi nchini.


Na Hafidh Kido

Katibu mkuu wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutokutoa taarifa zozote kwa jeshi la Polisi kuhusiana na suala lao la kutafutwa na watu anaodai ni wana usalama akidai hiyo ni kazi yao kufuatilia ukweli.

Akizungumza na wanahabari nje ya jengo la makao makuu ya jeshi hilo leo mchana alipokwenda kujisalimisha yeye na Gdbelss Lema, Dk slaa amesema hawezi kutoa taarifa zozote kwani hana imani na jeshi hilo juu ya masuala yanayomfika.

"Siwezi kusema chochote na wala sijabadili msimamo wangu wa kutotoa taarifa zozote kwa jeshi hili. Maana zipo taarifa nyingi tumeshawahi kuwapatia lakini kwa dharau tu hawajatekeleza hata moja, sasa inakuwaje wanataka wanihoji," aliuliza.

Hata hivyo wanahabari walikuwa na wakati mgumu katika  jengo hilo baada ya kusubiri kwa muda mrefu tangu saa nne kamili muda ambao Dk Slaa na Lema waliingia kufanya mahojiano na polisi mpaka saa sita na dadkika 28 mchana walipotoka.

Askari waliwazuia wanahabari kupiga picha na kuwataka watoke nje ya eneo hilo kwa madai wao hawajaita wanahabari.

Akizungumza na wanahabari mnadhimu wa polisi H.R. Mbezi, alisema hakuna ruhusa mwanahabari yeyote kupiga picha wala kuzungukazunguka kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

"Nani amewapa ruhusa kupiga picha, hamjui ni kinyume cha sheria na tunao uwezo wa kuchukua kamera zenu na kufuta picha zote mlizopiga," alihoji Mbezi na kuendelea "Tunawaomba muende kwa afande Kova kituo kikuu cha Polisi atawapa taarifa zaidi," alisema lakini wanahabari waliendelea kuwepo mpaka walipoitwa katika ukumbi wa mkutano na msemaji wa jeshi hilo afande Advera Senso.

Hata hivyo afande Senso hakuwa na la ziada zaidi ya kurudia yaleyale ambayo wanahabari walikuwa wakiyajua na ndiyo maana walikuwa hapo.

"Sisi tumewaita viongozi hawa wa CHADEMA ili kuwahoji na ikiwezekana watupe ushirikiano kutokana na taarifa zao walizozitoa wiki iliyopita kuwa wanatishiwa maisha na baadhi ya watu wa jeshi la polisi," alisema Senso.

wiki iliyopita viongozi wa chama hicho wakiongozwa na mwenyekiti wao Freeman Mbowe waliita wanahabari makao makuu ya chama hicho mtaa wa Ufipa Kinondoni wakidai kuna wana usalama wanafuatilia nyendo za Katibu mkuu wao Wilbrod Slaa, mbunge wa Ubungu John Mnyika na aliekuwa mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema.  

Lakini baada ya jeshi la polisi kupewa agizo na waziri wa mambo ya ndani Dk Emmanuel Nchimbi, kuwa wachukue maelezo za viongozi hao, chadema waligoma kutoa ushirikiano wowote kwa jeshi hilo kwa madai hawana imani nalo.

NB: Samahani wadau nilipiga picha nyingi lakini kamera ya jembe imeleta hitilafu sikuweza kuziweka kwenye mtandao. Ila nawaahidi ikikaa sawa nitawawekea nanyi mfaudu..

HAFIDH KIDO
0713 593894/ 0752 593894
DAR ES SALAAM, TANZANIA
hafidhkido@yahoo.com

No comments:

Post a Comment