Ndugu zangu
Jana niliwaahidi kuwa
nitawapa kisa kimoja nilichotoa ahadi kwa rafiki yangu Evans namna
nitakavyopambana na umaskini. Naam raha ya ahadi ni kuitimiza na si vinginevyo.
Tukiwa chuoni tulikuwa na
mawazo mengi sana
namna tutakavyokabiliana na maisha ya mtaani, chuoni kweu tulikuwa na wanafunzi
kutoka mataifa mbalimbali Afrika, lakini watanzania tulikuwa na urafiki mkubwa
na wakenya. Nadhani Kiswahili kimetuunganisha si unajua watanzania kingereza
tatizo?
Sasa nilijenga urafiki mkubwa
na ndugu Evans Musoka Luseno, Mkenya huyu mwenyeji wa Nairobi , urafiki wetu ulitokana na kufanana
malengo. Katika maisha hakuna kitu kizuri kama
kuwa na rafiki mnaefanana malengo.
Hivyo mwenzangu aliamua
akimaliza chuo siku akirudi Nairobi kutoka Kampala moja kwa moja
atafikia kwake na si kwao. Kwakuwa mimi ninakaa na mzazi wangu wa kike katika
nyumba ya kaka yangu hivyo sikupanga kuhama nyumbani maana nyumba ni kubwa na
kuhama kwangu itakuwa ni kukimbia majukumu wala si kuanza maisha mapya.
Mimi nilimuahidi rafiki yangu
yule kuitendea haki shahada yangu ya mawasiliano ya umma, na hasa niliamua
kujikita katika uandishi wa makala katika magazeti ili nipate malipo
yatakayoniwezesha kumlea mama yangu. Nilifanya hivyo baada ya kurudi na nikawa
ninaandika makala nyingi iwezekanavyo katika magazeti, tatizo likaja kwenye
malipo. Sikuwa nikipata chochote kwa makala zile ‘nilikopwa.’
Mwezi uliopita nilikwenda
mjini Kampala
kufuatilia matokeo yangu na namna ya kuendelea na shahada ya pili (master
degree), nikiwa njiani kurudi nyumbani nilimtembelea rafiki yangu Musoka na pia
nilipanga kupata nafasi ya kukutana na wangu wa ubani, naam shemeji yenu ni
mkenya.
Nilishitushwa sana na mafanikio aliyoyapata ndugu yangu yule, ana nyumba
ya vyumba viwili, choo na jiko ndani, analipa takriban elf kumi ya Kenya kwa mwezi.
Si pesa ndogo kwa Tanzania .
Tulizungumza mambo mengi na
nilishituka zaidi niliposikia hana kazi ya kuajiriwa ila ni mjasiriamali, ana
bodaboda na baadhi ya miradi. Mwisho wa wiki anakwenda kuchekesha (Standup
comedy) na anapata senti za kujikimu. Kadhalika anakwenda katika stesheni ya televisheni
na kujitolea kufanya kazi (volunteering).
Tulizungumza mambo mengi sana na niliona haya kwa kutotekeleza hata kimoja katika tulivyoahidiana
nilijisikia uchungu sana pale aliponambia hana
msaada wowote kutoka kwa ndugu yake na kama
haitoshi yeye ndie anaemsaidia mama yake. Kwa pamoja tuliamua tupange upya
mikakati yetu,na tulipanga tuwasiliane na dada Monica Akech mwanafunzi kutoka Uganda tuliwahi kusoma nae ili tuanzishe jarida ‘magazine’
ya east Africa , itakayobeba mambo kutoka kila
kona ya nchi tatu hizi.
Baada ya kurudi nyumbani na
kuona mambo bado nimagumu katika kuanzisha jarida hilo nikaamua kwanini nisianzishe jarida la
kwenye mtandao? Ndipo nikapata wazo hili la kuanzisha blogu ya kijamii.
Hivyo naamini huko aliko Nairobi , rafiki yangu ameanza kuona juhudi zangu nami
najisikia faraja sana
kwa kukamilisha ndoto yangu hii. Nafarijika kwa mafanikio ninayoendelea
kuyapata na nafurahi kuona blogu yangu imekuwa chanzo cha habari za watu wengu
kutoka nchi zifuatazo idadi ya watu wanaotembelea kwenye mabano, USA (970), Tanzania
(193), Russia (49), UK (29), Kenya
(19), Bahrain (4), Oman (4) na Germany (1).
Na leo asubuhi saa nne
nilishatembelewa na watu 51, ambao kwa siku za awali hao walikuwa wakitembelea
kwa siku tatu. Jana nilitembelewa na watu 310 na jumla ya watu wote
wanaotembelea tangu blogu ianzishwe ni watu 2584.
Hii ni hatua kubwa sana na ninamshukuru
Mungu kwa kila jambo. Nimeandika haya si kwa kutaka sifa bali ni kukupa moyo
wewe unaesoma kuwa kila kitu kinawezekana usivunjike moyo, anza sasa kutimiza
ndoto yako, kesho haijawahi kuonekana, hivyo huijui.
HAFIDH KIDO
0713 593894/ 0752 593894
DAR ES SALAAM , TANZANIA
hafidhkido@yahoo.com
No comments:
Post a Comment