Wanaadamu tumekuwa na
viburi vingi kutokana na neema alizotujaalia muumba ardhi na mbingu, bila ya
fahamu kuwa viburi hivyo huturudia wenywe pale tufikapo kikomo.
Hatujui tulitendalo!
linaweza kuwa jibu la haraka kwa wale wavivu wa kufikiri. Lakini nakataa kuwa
ni hivyo, kwa maana viburi tuvifanyavyo huazimia kabisa na mara nyingine
tunatenda mchana kweupeee!!
Leo nimeamua kutoa mfano
mdogo kabisa juu ya uwezo wa Mungu na udhaifu wa mwanaadamu. Kula: Naam hatuna
ujanja katika hilo ,
juu ya viburi vyetu vyote na haraka ya kuhangaikia maisha lakini lazima
tutafute kula.
Husemwa njaa haina
mjanja wala mwamba. Lakini tumejifunza nini katika tukio hilo ambalo tunaonekana kulizoea tu kuwa
lazima tule; umepata kujiuliza halafu ya kula ni nini, kulala? Ama kuzidisha
maasi kwa Mungu aliekujaalia baraka ya kupata kula.
Tazama, unaweza kuwepo
katika shughuli iwe harusi au msiba, lazima katika ratiba kutakuwepo muda wa
kula. Hudhani wanaadamu ni dhaifu kwa alietuumba na ndiyo maana hatuwezi
kujizuia kula? Mpaka sasa umechukua uamuzi gani kumshukuru muumba wako kwa
kukujaalia neema hiyo ya kupata kula.
Kwa maana nusu ya maisha
yetu tunayatumia kutafuta kula. Madhambi mengi yanasababishwa na harakati za
kutafuta kula. Magomvi na usaliti husababishwa na harakati ya kutafuta tonge.
Umepata kutenga muda na kufikiri kuhusu hili?
Tumeamrishwa na dini
kufanya ibada, lakini ibada yenye utulivu ni ile ifanywayo na kiumbe alieshiba,
kwa maana huaminika katika dini kuwa kiumbe alieshiba ana utulivu wa nafsi.
Mungu anasema ‘kuleni na kunyweni kisha mumuabudu aliewaumba.’
Hudhani kula pia ni
ibada. Lakini tunakula kwa ibada kweli? Mimi na wewe tunapaswa kulijibu swali
hili kwa mifano ya maisha halisi tunayoishi. Je tunakula ili tuishi ama
tunaishi ili tule.
Dini iliyo na ukamilifu
ya kiislamu inasema, mja anapokula hapaswi kushiba sana bali kiwiliwili chake kinapaswa kipate
nguvu tu. Kwani kushiba sana
huleta uvivu na maradhi; na pia haifai kulakula kila wakati kwani nako huleta
maradhi na uvivu. Umelizingatia hilo ?
Nchi zilizoendelea sasa
zinapigana na ulafi usio na msingi, maana wananchi wake wamevimbiana na miili
kupata maradhi ya mara kwa mara. Sukari, moyo, cholesterol, shinikizo la damu
na saratani yamekuwa ni maradhi yaletwayo na kula hovyo. Umelizingatia hili?
Hatuwezi kuepuka kula,
hata tuwe na nguvu kiasi gani. Hapa pana hekima kubwa sana na mazingatio kwa wenye akili.
Umelizingatia hili?
HAFIDH KIDO
0713 593894/ 0752 593894
DAR ES SALAAM, TANZANIA
20/07/2012

No comments:
Post a Comment