SERIKALI YA KENYA : imesema inazifanyia kazi taarifa za raia
wake kukamatwa na kufikishwa kortini nchini kwa tuhuma za kumteka na kufanya
jaribio la kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania , Dk Steven Ulimboka.
Hatua hiyo imekuja siku
moja baada ya Jeshi la Polisi kutangaza kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa
raia wa Kenya , Joshua
Mulundi anayetuhumiwa kuhusika na tukio la kumteka, kumpiga na kumtupa Dk
Ulimboka katika Pori la Akiba la Pande nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam
hivi karibuni.
Balozi wa Kenya nchini,
Mutinda Mutiso, alisema kwa njia ya simu jijini Dar es Salaam jana kuwa
Serikali yake itachunguza uraia na tuhuma zinazomkabili mtu huyo ili kubaini
ukweli.
“Ndiyo kwanza nimewasili
kutoka nje ya nchi…, nitafuatilia kwa makini kupata taarifa sahihi kutoka
kwenye vyanzo sahihi na mamlaka husika za hapa Tanzania
na Kenya
ili kupata taarifa ya kweli,” alisema Balozi Mutiso na kuongeza: “Siwezi
kueleza zaidi kwa sasa kwani itakuwa naeleza uvumi.”
MAT wadai kutoridhishwa
Wakati Balozi wa Kenya akisema
hayo, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimeelezea kutoridhishwa na hatua
hiyo kikisisitiza msimamo wake wa kutaka kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi kwa
lengo la kuwabaini wahusika na kuchukuliwa hatua stahiki.
MAT pia imesema kwamba,
inaendelea na mpango wake wa kuandamana, ikibainisha kuwa kesho itawasilisha
barua ya kuomba kibali cha kufanya maandamano ya amani Polisi.
Imefafanua kuwa malengo
ya maandamano hayo yaliyopigwa 'stop' na polisi kwa kile walichoeleza ni sababu
mbalimbali za kiusalama na kwamba, madai mengi ya madaktari yamefanyiwa kazi na
Serikali.
"Nisingependa
kuingilia suala la kipolisi kwa ujumla wake, lakini moja ya madai yetu ni
kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza tukio la kutekwa, kupigwa na kutupwa katika
Msitu wa Pande kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk Ulimboka," Katibu
Mkuu wa (MAT) Dk Rodrick Kabangila aliliambia Mwananchi Jumapili jana.
TUCTA nao wamo
Katika hatua nyingine,
Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (Tucta) limelipongeza Jeshi la Polisi kwa
kumkamata mtu anayedaiwa kumteka na kumpiga kiongozi wa mgomo wa madaktari, Dk
Steven Ulimboka.
Akizungumza jijini Dar
es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema kuwa, hatua ya
kumkamata mtuhumiwa huyo inaleta matumaini ya kuwabaini watu wengine
waliohusika na vitendo hivyo, jambo ambalo linaweza kurahisisha uchunguzi.
Alisema kutokana na hali
hiyo, jeshi hilo linatakiwa kuendelea na
uchunguzi ili waweze kuwabaini wahusika wengine na kubaini ukweli kuhusu tukio hilo ambalo limesababisha
kutokea kwa hisia tofauti katika jamii.
“Tunaliomba Jeshi la
Polisi liendelee na uchunguzi ili waweze kuwabaini watuhumiwa wengine na
kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema Mgaya.
Mkenya kukamatwa
Joshua Mulundi, ambaye
anatuhumiwa kumteka na kumtesa Dk Ulimboka alikamatwa na kupandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam juzi alasiri na kusomewa
mashtaka mawili na Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya.
Wakili Komanya alidai
mahakamani hapo kuwa, Mulundi ambaye makazi yake ni Murang'a nchini Kenya mnamo
Juni 26, mwaka huu akiwa eneo la Leaders Club alimteka Dk Ulimboka.
Hata hivyo, kumetokea
utata wa jina, umri wake na makazi ya mtuhumiwa huyo.
Wakati hati ya mashtaka
mahakamani inasema ni Joshua Mulundi mwenye umri wa miaka 21, mkazi wa Murang’a
nchini Kenya , taarifa ya
Jeshi la Polisi imesema anaitwa Joshua Mahindi mwenye miaka 31 na mkazi wa
Namanga nchini Kenya .
Katika shtaka la pili,
Wakili Komanya alidai kuwa tarehe hiyohiyo mshtakiwa alifanya jaribio la
kumsababishia kifo Dk Ulimboka kwa kumpiga katika eneo la Msitu wa Pande eneo
la Tegeta jijini Dar es Salaam ,
kinyume cha sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa
huyo alikana mashtaka hayo akidai kuwa makosa aliyoshtakiwa nayo siyo sahihi.
Hakimu Mkazi, Agnes
Mchome alimwambia kuwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina
mamlaka ya kusikiliza shauri hilo ,
isipokuwa Mahakama Kuu pekee.
Afya ya Dk Ulimboka
yazidi kuimarika
Akizungumzia hali ya
Afya ya Dk Ulimboka anayeendelea na matibabu nchini Afrika Kusini, Katibu Mkuu
huyo wa MAT alisema kuwa, Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania
anaendelea vizuri na sasa ameanza kufanya mazoezi ya kutembea.
"Taarifa tulizonazo
sasa ni kwamba, hali ya Dk Ulimboka inaendelea vizuri. Ameanza kufanya mazoezi
ya kutembea mwenyewe, anakula na pia anaweza kuzungumza vizuri. Amekuwa
akifanya mawasiliano yeye mwenyewe na madaktari wenzake wa hapa nchini ingawa
bado kuna matibabu anayoendelea nayo," alisema Dk Kabangila.
Mmoja wa Madaktari wa
karibu wa Dk Ulimboka aliyepo nchini, alisema Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya
Madaktari Tanzania
amewatumia ujumbe wa kuwashukuru wanataaluma wenzake na Watanzania wote
waliomchangia na kumwezesha kupata matibabu nchini humo.
Hata hivyo alisema kuwa,
Dk Ulimboka ameomba suala la tukio lake la kutekwa na kuumizwa lisiwe hoja ya
kujadili, badala yake madaktari na wananchi wote wajielekeze kudai haki zao,
ambazo Serikali haijazipa kipaumbele.
Dk Ulimboka
alisafirishwa nje ya nchi Juni 30 kwa ajili ya matibabu kufuatia jopo la
madaktari lililokuwa likimtibu likiongozwa na Profesa Joseph Kahamba kudai afya
yake imebadilika ghafla na pia angestahili kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya
vipimo na matibabu zaidi ambayo hayapatikani hapa nchini.
Chanzo: www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment