Mkurugenzi Mtendaji wa
Tanesco Bw. William Mhando, amesimamishwa kazi jana kupisha uchunguzi juu ya
tuhuma dhidi yake za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Bodi ya wakurugenzi ya
Shirika la Umeme Nchini -TANESCO- imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa
TANESCO Mhandisi WILLIAM MHANDO ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali
zinazoelekezwa dhidi ya Menejimenti ya TANESCO.
Taarifa hiyo imetolewa
na mwenyekiti wa bodi hiyo Jenerali Mstaafu ROBERT MBOMA ambapo katika taarifa
yake amesema maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao cha dharura kilichofanyika
jana kujadili masuala mbalimbali ikiwemo tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya
ya madaraka.
Taarifa zinasema katika
kikao hicho, Bodi iliona tuhuma hizo ni nzito hivyo ni vyema zikafanyiwa
uchunguzi huru na wa kina mara moja.
Jenerali MBOMA katika
taarifa hiyo amesema uchunguzi huo utaanza mara moja kwa kutumia mchunguzi
huru.
Aidha Bodi hiyo, leo
imefanya kikao kingine cha dharura ambapo imeamua kuwasimamisha kazi mara moja
wafanyakazi wengine wakiwemo naibu mkurugenzi mtendaji, huduma za Shirika Ndugu
ROBERT SHEMHILU, afisa mkuu wa fedha Ndugu LUSEKELO KASSANGA na meneja mwandamizi,
manunuzi Ndugu HARUN MATTAMBO.
Jenerali MBOMA amesema
kufuatia hatua hizo zilizochukuliwa, Bodi imechukua hatua stahiki ili
kuhakikisha shughuli za kiutendaji na uendeshaji wa TANESCO zinaendelea kama kawaida.
No comments:
Post a Comment