Dunia imefanywa kuwa
uwanja mkubwa wa kila nakama na amali zinazosaidia maisha kuendelea ima kwa
taabu au mafanikio. Mungu akaamua kuwapa wanaadamu maarifa ya kuweza kuyamudu
mazingira ya kidunia baada ya baba yetu kuasi huko mbinguni na kutupwa ardhini kutiwa
adabu.
Maisha yana changamoto
nyingi sana ,
baba yetu Adam, ndie anaesadikiwa kuwa ni kiumbe pekee aliepata kuishi duniani
na kuwa na elimu nyingi akifatiwa na nabii Hidhri alietajwa katika visa vya
Mtume Mussa.
Nae nabii Suleiman,
anasadikiwa kuwa ndie mwanaadamu aliepata kuwa na hekima sana . Lakini umeshawahi kujiuliza tofauti ya
hekima na elimu ama ufanano wao?
Mungu, mwingi wa rehema
baada ya kugundua maisha ya duniani ni magumu kuishi, na kumtuma kwake mwanaadamu
kuja kuishi duniani ingekuwa ni hatari na taabu aliamua kumpa maarifa ili aweze
kuitawala dunia.
Kwa kuwa awali hakukuwa
na utaratibu wa elimu tuliyonayo sasa Mungu alishusha ‘ilhaam’ ama maono kwa
wateule wachache na kuwaamuru wasambaze elimu ama hekima hiyo aliyowapatia.
Leo tuna vyuo vingi,
shahada na mavyeti ya kila taaluma yanatolewa kwa wasomi wetu; lakini dunia
imekuwa mahala pagumu kuishi kuliko zama ambazo hakukuwa na vyuo hivi
vinavyosadikiwa kutoa elimu. Kuna kitu kinakosekana. Hekima.
Naam tuna wasomi wengi
lakini hawana hekima juu ya usomi wao, matokeo yake hawazitumii elimu zao
kusaidia kuondoa matatizo katika jamii zilizowazunguka na hata majirani zao.
Tofauti ya elimu na
hekima ni kuwa elimu unaipata darasani ama kwa kukaa karibu na mwenye elimu
ukaiga aina ya maisha anayoishi ama kwa kusoma maandiko yake. Lakini hekima
haipatikani darasani wala kwa kusoma maandiko, bali hekima hutoka kwa Mungu ama
kwa kukaa karibu na mwenye hekima akakukuza katika mwenendo huo.
Na ndiyo maana ukiona
mtu anafanya mambo ya ajabu yasiyokubalika katika jamii, ni mara moja mtu
kuuliza huyu ametoka wapi, wa ukoo gani huyu, kabila lake ama wazazi wake ni
watu wa wapi, na vitu kama hivyo. Na baada ya
hapo ndipo yanapokuja masuala kama kiwango cha elimu na aina ya kazi ama
kipato, ingawa vina uhusiano mdogo sana
na tabia ya mtu ama hekima.
Elimu ni neno la kiarabu
lililochopolewa na kuingizwa katika lugha ya Kiswahili: msingi wake ni neno
‘Ilmu’kwa lugha ya kiarabu. Ikimaanisha ufahamu wa kuyajua mazingira ama
utaalamu juu ya suala fulani la kijamii.
Mtaalamu ni neno pia
lililotokana na lugha ya kiarabu lenye maana mtu alieelimika ‘ataalim’
alieelimika. ‘El- alaamaa’ mwenye elimu kuu ama mkufunzi.
Hivyo uwiano wa elimu na
hekima ni wa karibu sana ,
na ndiyo maana katika dini ya kiislamu hekima ni muhimu kwa wanazuoni. Huwezi
kuwa mkufunzi wa masuala ya dini ya kiislamu kama
hauna hekima.
Hekima pia ni neno
lililotokana na lugha ya kiarabu lenye maana ya mtu mwenye kujua hukumu ya
mambo. Wale watu waliosoma ‘fiqhi’ ama maulamaa wenye kuweza kutoa fatwa
‘hukumu’ ni lazima wawe na hekima.
Hivyo ili uitwe mwenye
elimu ‘ataalim’ ni lazima uambatane na hekima. Na ndiyo maana wasomi wa shahada
ya uzamivu (PHD) ‘Doctor of Philosophy’ ni lazima watunukiwe cheo cha heshima
cha ‘professor’ pale anapoonyesha hekima ya hali ya juu katika taaluma yake.
Ama kiongozi wa kijamii
kama Rais, Waziri ama mtu yeyote anaefanya maamuzi yake ya kuisaidia jamii kwa
kutumia hekima, vyuo vikuu huamua kumtunukia shahada ya uzamivu (PHD), kama
ishara ya kutambua hekima yake aliyoitumia katika kutatua matatizo ambayo wao kama wasomi yalikuwa yakiwasumbua na walishindwa
kuyatatua.
Hapa pia naomba niweke
wazi: kuna tofauti kubwa kati ya msomi na mwenye elimu. Msomi ni Yule ambae
anajishughulisha kutafuta elimu- anaweza aipate hiyo elimu ama laa. Anaweza pia
kuwa alishahitimu vyuo kadha kwa kusoma, lakini hawezi kuwa ni mwenye elimu.
Ila mwenye elimu: ni
Yule ambae ameshasoma ama bado anasoma lakini athari zake katika jamii
zinaonekana. Anaweza kutoa maamuzi ambayo jamii nzima yananufaika kwayo. Lakini
msomi anaweza kuwa mtu yeyote tu ambae amepitia vyuoni na kutunukiwa vyeti
lukuki.
Mfano mzuri katika vyuo
vikuu vyetu vya sasa, tunao wasomi maelfu kwa malaki, ambao wanahitimu na ambao
bado wanaendelea kusoma. Lakini wameisaidia vipi jamii kwa usomi wao. Mara
nyingine hata hawajaelewa walichokuwa wakikisomea kwa maana walitaka jamii tu
ijue kuwa nao wapo vyuoni.
Ila wenye elimu ni
wachache, ambao wanajitahidi kuzitumia elimu zao kufundisha wengine ama kufanya
mambo yatakayosaidia jamii zao kupiga hatua.
Je, tunaweza
kutofautisha baina ya elimu na hekima? Nadhani ni sawa na kusema gari na
mafuta, ni vitu ambavyo havikimbiani vinategemeana kila kimoja kinamuhitaji
mwenzie.
Naomba kuwasilisha.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM , TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
26/07/2012
No comments:
Post a Comment