Na Hafidh kido
Dunia imegubikwa na maudhiko mengi sana , asilimia kubwa ya
maudhiko hayo husababishwa na aina ya marafiki tulio nao. Ni ngumu sana kujua yupi ni rafiki
wa kweli na yupi si rafiki wa kweli, kwa maana hawajapigwa chapa usoni
kuonyesha tabia zao za ndani.
Ubinafsi huchochea urafiki mbaya, waovu
wengi huunguzwa na choyo, kujipendelea wao kwanza na chuki ya maendeleo ya
jirani yake. Kukoma mambo hayo ni ngumu kama
ardhi na mbingu kukutana.
Ajabu ya dunia huwezi kuepuka marafiki;
kamwe haliwezekani hilo .
Lakini ni vema kuchagua yupi rafiki na yupi ni mwandani wako. Angalia kwa
makini maneno hayo mawili, rafiki na mwandani. Kuna fotauti kubwa sana kati ya hatua hizo
za maisha.
Watu tumeumbwa ili tuishi katika jamii ya
watu wengi, nafsi zetu ni dhaifu, ila Mungu muumba kila ajabu amejaalia nguvu
fulani ikujiayo kila unapodhuriwa na urafiki mbaya. Nguvu hiyo huitwa SUBIRA;
naam kusubiri ni ibada njema sana
katika dunia ya ghanima nyingi, ina msaada wa ajabu usiomithilika.
Marafiki ni watu wa karibu tunaoishi nao
katika jamii ama mkusanyiko wa watu. Inaweza mmezawa kijiji kimoja, mnasoma shule moja ama
mnafanya kazi afisi moja. Wote ni marafiki zako, huwezi kuwaepuka hata kidogo.
Lakini katika lundo hilo
la marafiki lazima utakua na mmoja tu ama wawili ambao ni wandani wako, walipo
wao ndipo ulipo wewe, wafanyalo wao ndilo ufanyalo wewe hamuepukani.
Mwandani wako ni kama
ndugu, hamuachani na kila akengeukapo maadili si wewe tena unaemrekebisha bali
jamii ndiyo inayomrekebisha kwa kumkumbusha ‘tazama mwenzako alivyo, tofauti na
wewe umebadilika kabisa. Kwanini hufanyi kama
afanyavyo rafiki yako?’ Nadhani umenielewa.
Tazama tunazawa sehemu mbali na kukulia
sehemu mbali, tunasoma shule ya msingi hapa, na tunasoma sekondari sehemu
yingine. Ama tunamaliza chuo kikuu sehemu moja na kufanya kazi sehemu nyingine.
Kote huko unapoondoka unaacha lundo la marafiki, na huwezi kuwaepuka hata
kidogo wamekuganda na ima watakuja kukusaidia au wao watahitaji msaada kwako.
Ndivyo dunia ilivyo maajabu na vizugumkuti ni vitu vya kawaida sana .
Marafiki ni watu wazuri sana
kuwa nao, kadhalika ni wabaya sana
unaposhindwa kufaya wanachotaka. Siku zote wao wapo sahihi, hawakosei wala
hawahitaji kurekebishwa; ukifanya lenye heri nao utasifiwa mpaka kizazi chako
cha ishirini kilichopita, na ukiwakosea utatukanwa na kukumbushiwa maovu yako
ya tangu utotoni. Ndivyo dunia inavyowatesa wanaadamu, ama inavyofanya
wanaadamu watesane wao kwa wao.
Wapo marafiki ambao wanakujua pindi uwapo
na shida, hao ni wazuri sana .
Wapo marafiki wanaokuonya pindi unapopotea, wakumbatie sana
marafiki hao usiwaache, wapo marafiki wanaokuvuta utoke kwenye shimo la hatari,
wapende sana na
ikiwezekana kawatambulishe kwenu.
Lakini wapo marafiki ambao wanasubiri
upotee ndipo wakuseme, kaa mbali nao ila usiwatenge maana si kosa lao bali
hawajiamini. Wapo marafiki ambao ukiwaambia ukweli hukasirika na pengine
huiambia jamii wewe ndie mbaya maana unamzulia mambo asiyo nayo, rafiki huyo
muepuke baki kumpa salamu tu lakini si siri zako. Wapo marafiki ambao hukufata
pindi wawapo na shida tu, ni vema wasaidie, ila unapogundua wewe ukiwa na shida
wanakuepuka huna budi kuwaepuka nao.
Msomaji usione hawa marafiki ni ni watu
waishio dunia ya peke yao ,
bali tumo nao humuhumu pengine mmoja wao ukiwa wewe au mimi mwandishi. Maana
kama tukisema kuna marafiki wabaya kila mmoja atasema mimi si mmbaya, husemwa
nyani haoni kundule.
Ukimnyooshea mtu kidole kimoja jua
vilivyobaki hukurejelea wewe, hakuna wa kumfunga paka kengele ila muandishi
anajaribu kuiasa jamii tuwe marafiki wema kwa marafiki zetu.
Wewe ukiwa mwema na Yule akipendezewa na
wema wako basi dunia itakua ni mahala salama na bora pa kuishi. Lakini kila
mmoja akisema Yule ndie mmbaya, basi sote tutakua wabaya. Ikiwa unamnyooshea
Yule hata nae anamnyooshea Yule ambae ni wewe. Umeona mkanganyiko
huo?
Anza kubadilika sasa, kuwa rafiki mwema
ili rafiki yako nae awe mwema. Maana urafiki mmbaya huzaa chuki, magomvi na
hasada kubwa katika dunia. Ulimwengu umeshakinai vurugu zisababishwazo na
urafiki mbaya, ardhi imeelemewa na damu imwagwayo kwa urafiki mmbaya.
Huoni kidole chako ukikitumia vyema kuziba
tundu imwagayo damu kwa
urafiki mbaya itasaidia kizazi chetu kiishi katika mazingira bora?kuliko kidole
hicho kukitumia kuwanyooshea marafiki wabaya, ambapo bila kutazamia hata wewe
hunyooshewa. Badilika, anza
sasa kumkumbatia rafiki uliekosana nae.
Neno dogo sana
la kuomba radhi huweza kubadilisha jambo kuu kama
dharau, chuki na hasada. Hukuchukua sekunde chache sana
kusema ‘SAMAHANI’ lakini bila ya kutambua itakuchukua miaka mingi sana kuhuzunika,
kutaabika na kukosa amani kwa kushindwa kuzitumia hizo sekunde chache za kusema
samahani ama kuomba radhi.
Naomba kuwasilisha…
No comments:
Post a Comment