Mtoto wa miaka kumi
anaamka asubuhi katika kitanda cha kamba, chumba hakina sakafu ni udongo,
amelala na nguo alizocheza nazo kutwa siku ya jana. Chumba kidogo vitanda
viwili lakini wamelala watano madirisha madogo ya kupitishia hewa ila la
kushukuru hakina mlango hivyo hewa itapitia mlangoni.
Anakurupuka kitandani,
mswaki upo katika kopo moja lenye miswaki ya watu kama
saba, hakuna dawa ya meno anatumia mkaa, anaoga kwa kutumia viganja vyake maji
ya baridi na choo ni hichohicho cha haja kubwa, ndogo na kuoga.
Hana haja ya kutafuta
kaptula ya shule kwa maana ndiyo aliyokesha nayo tangu jana alipotoka shuleni,
anakumbuka shati lake alivaa mdogo wake na bado amelala nalo, anamwamsha
ili ampatie shati lake
akamilishe sare ya shule.
Hajapiga pasi, hana
viatu vya kupiga rangi wala mkoba wa vitabu.
Anakwapua madaftari yake
mawili anayoyatumia kuandikia masomo saba mumo kwa mumo. Hana haja ya kuomba
nauli kwa maana anatembea kwa miguu mpaka shuleni ingawa ipo umbali
mrefu.
Kumbuka hajanywa chai
kwa maana mama na baba ndiyo wamekwenda shambani kuitafuta; akifika shule
amechelewa na mwalimu anamngoja kwa adhabu kwani hana fagio la kufanyia usafi
na amechelewa.
Akishatandikwa bakora
anaingia darasani, madawati hayatoshi anakaa chini; anakumbuka kalamu yake
iliisha wino na baba alimuahidi akienda mjini kuuza mazao yake atamnunulia ila
hajafanya hivyo ima kwa kusahau au hakuona umuhimu wa kununua kalamu ya mtoto
na kuacha kumnunulia rafiki yake pombe kilabuni.
Mwalimu anafundisha mara
anaingia mkuu wa shule anataja majina, na kusema ambae hakusikia jina lake atoke
darasani kwani tangu muhula uanze hawajaleta pesa za mchango wa majengo. Hivyo
waende nyumbani wakawaambie wazazi wawalipie. Badala ya kurudi nyumbani watoto
wasio watiifu wanaamua kupitia maporini na kuwinda ndege ama kupopoa maembe.
Miaka saba inamkuta
mtoto akimaliza elimu ya msingi kwa mtindo huo. Wachache wanafaulu na wengi
wanashindwa kuendelea na elimu ya sekondari.
Waliobahatika
kuchaguliwa hali wazazi wana uwezo wanaendelea na masomo, ila wenye bahati
mbaya wanaishia hapo kwani wazazi hawana uwezo na serikali nayo haina uwezo
kubeba mzigo wote huo ingawa ada ya mtoto mmoja kusoma sekondari ya serikali
haizidi laki moja, lakini serikali inapoteza zaidi ya bilioni kadhaa kwa
kutokusanya kodi, hali wabunge, mawaziri na maafisa wa serikali gharama za
magari na ofisi zao ni kubwa kulingana na aina ya maisha waliyochaguliwa na
serikali.
Waliobahatika kusoma
mpaka kidato cha sita wengi wataishia hapo na wachache wataingia elimu ya juu,
kwa mkopo wa serikali ambao unatolewa pale serikali inapojisikia tena kwa
kiwango wanachojisikia. Mtoto kwa kuwa ameshazoea shida huamua kusota kwa miaka
mitatu ama minne chuoni wakihemea kidogo wanachopata.
Baada ya hapo ajira huwa
ni hadithi nyingine isiyosimulika, kwa maana huajiriwi mpaka uwe una ujuzi wa
miaka mitatu, sasa sijui chuoni kuna ujuzi gani.
Na kwa wale wenye mawazo
ya kujiajiri msingi wa kujiajiri ni mkopo wa kanzi ‘Bank’ kwa lugha ya kigeni,
na huo huupati mpaka uwe na kitu kisichohamishika. Shamba la ukoo lazima
litolewe sadaka.
Na kwa wale waliokomea
darasa la saba ambao ni wengi kuliko hawa wa chuo kikuu huamua kujikita katika
kilimo, nguvu wanazoziingiza katika kilimo hazilingani na kipato
wanachostahiki. Huamua kukimbilia mjini wakabishane na maisha.
Hawana elimu, hawajui
kuongea lugha ya kigeni, hawajui kuvaa makoti na tai, hivyo hawaajiriki.
Wanaamua kujiajiri, lakini hawana mjomba wala baba mdogo wa kuwashika mkono,
wanaamua kuuza nguo, kuuza bidhaa ndogondogo za kushika mkononi (umachinga).
Serikali inaona aibu kwa
wageni na wafadhili wanaokuja nchini hasa ikizingatiwa jiji la Dar es salaam ndipo kilipo
kiwanja kikuu cha kupokelea wageni. Kwa lugha rahisi ndipo ilipo sebule ya
nchi, napo ndipo wamachinga walipojaa. Inaamua kuwafukuza, haiwataki,
wanawanyang’anya bidhaa zao. Mtaji unarudi sifuri.
Kwa wale walioamua
kujifichaficha wanapata vijisenti, wanapanga chumba, lakini inabidi apange
chumba nje ya mji kwani katikatika ya mji ni ghali sana . Anapata chumba kitunda takriban
(kilometa 30 kutoka mjini), kwa mwezi ni shilingi elfu kumi na tano, chumba
hakina umeme. Kwa kuwa ameshakuwa barobaro inampasa aoe, anaagiza mchumba wake
wa kijijini aletewe.
Mke kwa kuwa ameshazoea
kufanya kazi hataki kuwa mama wa nyumbani anaamua kupika chakula ‘mama lishe’.
Mume kutoka nyumbani mpaka mjini kila siku kwenda na kurudi anatumia shilingi
elfu moja ya nauli, akila chakula cha mchana na chai ni shilingi elfu mbili,
ukichangaya na nauli jumla inakuwa shilingi elfu tatu kila siku.
Mapato yake ya biashara
kwa siku ni shilingi elfu kumi, akitoa pesa ya mtaji elfu tano inabaki elfu
tano. Akitoa matumizi ya kila siku elfu tatu maana yake anabakiwa na elfu
mbili. Kila siku, kwa wiki anapata elfu kumi na mbili kwa kuwa jumapili hafanyi
kazi maana watu hawaji mjini.
Kwa mwezi anapata
shilingi elfu arobaini na
nane. Hapo hajalipia kodi ya chumba elfu kumi, hajanunua mahitaji ya nyumbani,
hajamtumia mzazi wake hela ya mafuta ya taa kijijini, yeye, mkewe na watoto
hawajaugua wakajitibu.
Bila ya kusahau biashara haiwi nzuri kila siku, kuna
faida na hasara, mama lishe ambae ndie mkewe hajatupiwa chakula chake na askari
wa jiji, yeye mwenyewe kama machinga
hajatupiwa bidhaa zake na askari wa jiji. Hajakutana na vibaka njiani wakampora
kila alichokuwa nacho. Hapajatokea michango ya misiba, harusi au rafiki kumtaka
msaada tu wa kifedha.
Kumbuka nimetoa mfano wa
Tanzaia, lakini nchi nyingi za kiafrika kama
siyo zote hayo ndiyo maisha halisi wanayoishi ama tunayoishi.
Utaona kwamba maisha ya
mwanaadamu anaeishi Afrika ni magumu sana ,
yanakufunza mambo mengi kiasi unaweza kuishi mahala popote duniani hutojali
utakutana na mabalaa gani.
Wazungu na ukichaa wao
wote huko ulaya wanapokutana na waafrika wanafanya kazi ngumu katika mazingira
hatarishi huwa wanashangaa mambo haya tunayaweza vipi.
Wapi tulipokosea, nini
cha kufanya au nani wa kumshika ili aturekebishie haya.
Viongozi tukiwachagua
wanajali familia zao tu, mtu anapoingia madarakani anafikiria atumie njia gani
abaki madarakani, na si kuwa atumie njia gani kututoa katika huu umasikini wa
kutupwa.
Si tu masikini ndiwo
wanaopata taabu hizi na mateso; Hata walio katika hali nzuri kifedha, bado
wanakutana na changamoto nyingi za kimaisha.
Umeme, maji na barabara
bado ni tatizo, umeamua kurudi nyumbani ili umalizie kazi za kiofisi, foleni ya
magari inakuchelewesha, unafika nyumbani umechoka unataka uoge na ulale kidogo
ili ufanye kazi za ofisi kesho bosi anazitaka. Unakuta maji yamekatika, kutoka
nyumbani mpaka maji yanapotoka ni mbali si haba.
Unaaamua kulala
hivyohivyo.. unaamka unawasha mashine yako unaanza kufanya kazi, umefika
katikati ya kazi umeme unakatika unarudi baada ya saa sita. Umeshakata tamaa na
akili haikuruhusu kufanya kazi na kesho bosi anaitaka asubuhi na mapema.
Unaamua kulala ili kesho
uamke mapema uwahi ofisini ukaimalizie huko, unaamka mapema kweli lakini kupata
daladala ya ofisini ni kwa kugombania, unakaa kituoni nusu saa ndipo unapata
gari, njiani unakutana na foleni isiyotembea, unafika ofisini bado umewahiwahi,
unafungua kazi unakuta imeliwa na virusi ama umeme umekatika. Je kwa hali hiyo
tutafika?
HAFIDH KIDO
0713 593894/ 0752 593894
DAR ES SALAAM, TANZANIA
hafidhkido@yahoo.com


No comments:
Post a Comment