Tuesday, July 24, 2012

Mgomo baridi wazorotesha huduma Muhimbili..


PAMOJA na kuwa mgomo wa madaktari uliotikisa nchi kutajwa kuwa umemalizika, huduma katika hospitali kubwa nchini zikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH), Taasisi ya Mifupa (Moi) bado si za kudhirisha Mwananchi limebaini.

Kuzorata kwa huduma hizo kunatajwa kuwa ni kutokana na ukimya uliopo kwa sasa baina ya serikali na wataalamu hao ambao mara kadhaa wameomba kurejea katika meza ya majadiliano na serikali hata baada ya kurejea kazini.

Kwa muda mrefu wataalamu hao walikuwa kwenye mgomo wa wakishinikiza serikali kutekeleza madai yao ,lakini mgomo huo umetulizwa kwa serikali kuwatimua kazini madaktari waliokuwa kazini na kusitisha usajili kwa ambao idadi yao imefikia zaidi ya 380.

Miongoni mwa majibu ya serikali kwa madaktari hao yaliyotolewa baada ya vikao sita vya kamati iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kushughulikia madai yao ni kuwa wataalamu hao ni wafanya kazi wa kawaida kama watumishi wengine wa umma na hivyo taratibu za madai yao zingeshughulikiwa kwa kufuata taratibu za kawaida.

Mmoja wa maofisa katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili aliyezungumza kwa sharti la jina lake kutotajwa gazetini, alisema majibu hayo yamedhoofisha utendaji kazi wa wataalamu hao ambao kwa sasa wanaondoka kwenye maeneo ya kazi mara tu muda wakazi unapomalizika.

“Awali wataalamu hao walikuwa wanafanya kazi bila kujali muda wa kuondoka kazini ,lakini sasa muda ukiisha hata kama alikuwa hajamaliza kutembelea wagonjwa anaondoka kwenye kituo cha kazi na ukihoji anakuambia naye ni mfanyakazi wa kawaida kama ilivyo kwa wafanya kazi wa sekta nyingine za watumishi wa umma”alisema ofisa huyo ambaye siyo daktari kitaaluma.

Baadhi ya madaktari bingwa walipohojiwa na Gazeti hili walibainisha kuzorota kwa huduma hizo, huku wakitaja sababu kubwa kuwa ni idadi ya watumishi wachache baada ya wenzao kufukuzwa kazi na pia kutokuwa na majibu ya kuridhisha juu ya madai yao.

“Madaktari walio katika mafunzo hufanya kazi kubwa, kutokuwapo kwao kunasababisha pengo katika utendaji kazi wa kila siku”alisema Mmoja wa madaktari hao na kuongeza: 

“Pia na sisi tumeambiwa ni sawa na wafanya kazi wengine walio katika sekta za utumishi wa umma,tufanya kazi kama wao na muda unapoisha tutaondoka kwenye vituo vya kazi hata kama kutakuwa na mahitaji mengine ya kitaalamu”alisema mmoja wa madaktari hao kutoka MNH.

Alipoulizwa juu ya kuzorota kwa huduma hizo Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Dk Edwin Chitage alitaja sababu mojawapo kuwa idadi ya madaktari waliofukuzwa na kusitishwa usajili katika hospitali za umma ni kubwa.

Dk Chitage alitaja baadhi ya hospitali kubwa alizodai kuathiriwa na tukio hilo la kufukuzwa kazi kwa madaktari kuwa ni MNH , Hospitali ya Rufaa Mbeya, Bugando (Mwanza),KCMC (Moshi),na Hospitali ya Rufaa Dodoma.

Dk Chitage alibainisha kuwa huduma katika hospitali zote kubwa zilizokumbw ana mgogoro bado hazijarejea katika hali ya kawaida na hiyo ni kutokana na idadi ndogo ya madaktari waliobaki pamoja na kutokuwa na majibu sahihi juu ya madai yao waliyowasilisha serikalini.
Akizungumzia hilo Katibu Mkuu wa (MAT) Dk Rodrick Kabangila alisema inasikitisha kuona serikali imekaa kimya licha ya jitahadi zilizofanywa na chama hicho za kutaka kukutana katika meza ya majadiliano.

“Madaktari wazungumzia hatima .
Wakati serikali ikiwa kimya juu ya mgogoro huo kwa sasa, viongozi wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT),Jumuiya ya Madaktari na Madaktari waliofukuzwa na kusimamishwa jana walikutana Dar es Salaam kujadili mustakabli wao.

Katibu wa Jumuiya hiyo Dk Chitage alilihalikisha Gazeti hili juu ya kufanyika kwa mkutano huo ambapo alisema mapendekezo yatakayotokana na mkutano yatasambazwa kwenye vyombo vya habari.
Chanzo: kamanda wa matukio blog


No comments:

Post a Comment