Kaka yangu Maggid
Mjengwa, katika maandiko yake humu facebook, alipata kuandika utaratibu wake wa
maisha kila anapoamka asubuhi. Nilivutiwa sana
na muda ambao hufanya mazoezi ya kukimbia ‘jogging;’ niliandika kumuonea ngowa
au wivu juu ya kufanya kwake mazoezi muda wa asubuhi.
Kwa maana kama unachelewa kulala, lazima utachelewa kuamka; hivyo
kwa sisi tulio vyuoni na wengine walio makazini muda wa asubuhi huwa ni wa
kujiandaa kutoka. Na mara nyingi huwa umechelewa. Sasa ikiwa kuna watu walio na
shughuli nyingi kama kina Mjengwa, wanapata
wasaa wa kufanya mazoezi, inastaajabisha kidogo.
Nilionyesha kuyatamani
maisha yake, naye kwa busara alinijibu neno moja tu ambalo lilininyima raha
siku nzima mpaka nilipopata wasaa wa kukaa chini na kuliandikia kurasa hizi
kutoka katika neno hilo
moja.
Alinambia bwana Hafidh,
unaweza kuwa kama mimi unachotakiwa ni
‘nidhamu,’ lile neno nidhamu ndilo lililonisisimua. Nikakaa na kujiuliza neno
dogo kama hili mbona limeushtua sana
moyo wangu na kukosa raha siku nzima? Lina nini ndani yake mpaka likanipa mzigo
mkuu namna hii.
Naam, nidhamu ni chachu
ya maendeleo. Na ndiyo maana Mungu amehubiri nidhamu katika matendo yake,
huchukia sana
watu wasio na nidhamu.
Nilijaribu kutafuta
kamusi ya Kiswahili kwa Kiswahili ili kujua maana ya neno nidhamu limeelezwaji
kwa kirefu. Sikubahatika kuipata, ila kwa ufahamu wangu mdogo wa lugha ya
Kiswahili nidhamu ni adabu, maadili au mfumo wa maisha ambao unamfanya mtu
afuate taratibu zilizopangwa bila ya kukengeuka.
Wanajeshi somo la kwanza
baada ya kujiunga na jeshi ni nidhamu, huwezi kuwa mwanajeshi , mwanausalama au
polisi kama huna nidhamu. Ni amri moja tu
mdogo kwa mkubwa; Nidhamu.
Ukiamua unaamka saa kumi
na moja ya asubuhi, unasali, unafanya mazoezi, unasoma magazeti, unaoga na
kuelekea kazini, chuoni ama shuleni; utaratibu huo wa maisha unahitaji nidhamu
kuweza kuufuata. Kama huna nidhamu lazima
utakuwa mvivu wa kuamka na kutekeleza yote hayo.
Nidhamu hukufanya
kukumbuka wajibu, hukulazimisha kutenda kitakiwacho wakati huo bila
kuchelewa wala kukosa. Kifupi hukujengea kufuata utaratibu na kuepuka njia za
mkato ama uzembe.
Kutokana na neno hili
moja ‘nidhamu’ lililotoka katika kinywa cha mwanajamii Mjengwa, nimegundua
jamii inakosa maendeleo kwa kupungua nidhamu ya uwajibikaji; watu wanaanguka
mitihani darasani kwa kukosa nidhamu ya kuzingatia wanachofunzwa, biashara
hazileti faida kwa kukosa nidhamu ya mapato na matumizi, mashirika yanafilisika
kwa kukosa nidhamu ya kazi. Hata ndoa zinavunjika kwa kukosa nidhamu.
Cha ajabu jeshi
linaheshimika na kuogopewa katika jamii, unadhani ni nini kinawatisha?
kwasababu jeshini kuna nidhamu. Mtu asie na nidhamu hafai kuwa mstari wa mbele.
Hivyo nimegundua hakuna
kinachoshindikana katika uso wa dunia ikiwa kutakuwa na utaratibu wa kuwa na
nidhamu, mtu yeyote duniani akitaka kuwa sawa katika maamuzi na jamii
imuheshimu hana budi kuwa na nidhamu.
Nimejifunza kitu kipya
kutoka kwa mzee wa neno la leo mwenzangu, nacho ni nidhamu.
HAFIDH KIDO
0713 593894/ 0752 593894
DAR ES SALAAM, TANZANIA
hafidhkido@yahoo.com
Siri ya mafanikio ipo kwenye nidhamu
ReplyDelete