WANASAYANSI mbalimbali
wanaoendesha tafiti mbalimbali za kutafuta tiba na chanjo ya Ukimwi,
wameitangazia dunia kuwa hatua waliyofikia sasa wanauona ugonjwa huo ‘siyo
hatari tena’ kwa sababu wanazo silaha zote za kuweza kukabiliana nao.
Ila wakasema, kinachowakwamisha
ni ukosefu wa fedha ambazo zinahitajika katika kuendeleza tafiti na kuweka sera
mpya za kukabili Virusi Vya Ukimwi (VVU) duniani.
Hayo yalibainika kwenye
siku ya pili ya Mkutano wa 19 wa Kimataifa wa Ukimwi unaofanyika mjini Washington DC ,
Marekani na unahudhuriwa na watu zaidi 22,000 miongoni mwao wakiwamo wataalamu
wa afya, watunga sera na wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo toka karibu
kila kona ya dunia.
Kwa mujibu wa taarifa
kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari cha Mkutano huo na
gazeti hili kufanikiwa kupata nakala yake, ilieleza kwamba jopo la wanasayansi
nguli duniani walikiri kuwa wamefanyia VVU utafiti wa kutosha ndiyo maana
wanatamba kuwa wamefanikiwa katika kuvidhibiti.
“Kwa sasa tunazo silaha
zote za kisayansi kumalizia mbali gonjwa hili la Ukimwi. Kilichobaki ni kutumia
kikamilifu utaalamu huu katika fursa hii tuliyo nayo,” alisema Rais wa Taasisi
ya Kijamii ya Kimataifa ya Mapambano dhidi ya VVU (IAS), Dk Elly Katabira.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment