Na Mwandishi Maalum
Ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,
imekabidhiwa rasmi Ujumbe wa Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa (UNBOA)
Makabidhiano hayo
yamefanyika siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, katika hafla
iliyofanyika mwishoni mwa mkutano wa 66 wa Bodi ya Wakaguzi ya UM.
Katika hafla hiyo Afrika
ya Kusini ndiyo iliyoikabidhi Tanzania
kijiti hicho. Makabidhiano ambayo yalishuhudiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe.
Balozi Ombeni Sefue ambaye ameiwakilisha Serikali katika makabidhiano hayo.
Afrika ya Kusini imekuwa
mjumbe wa Bodi kwa miaka 12 na Tanzania
itamaliza ngwe yake mwaka 2018
Aidha hafla hiyo pia
ilihudhuriwa na Bi Suzan Malcora ambaye ni Msimamizi Mkuu wa Ofisi ya Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa (Chief de Cabinet). Akimwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa, Mhe. Ban Ki Moon.
Akizungumza wakati wa
hafla hiyo iliyowashirikisha pia wajumbe wengine wa bodi ambao ni Bw. Dong
Dasheng akimwakilishi Mkaguzi Mkuu kutoka Uchina na Bw. Amyas Morse Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu kutoka Uingereza. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu , Bw. Ludovick Utouh
amewahakikisha wajumbe wenzie pamoja na sekretariati ya Umoja wa Mataifa kwamba
Ofisi yake imejipanga vema kulibeba jukumu hilo .
“ Hafla hii ya leo
inahitimisha rasmi mchakato mrefu wa makabidhiano ya jukumu hili, mchakato
ulioanza tangu uteuzi wangu ulipofanyika mwezi Novemba mwaka jana. Ni mchakato
unaofungua ukurasa wa kubadilishana mawazo, uzoefu na utaalamu. Kwa niaba ya
Nchi yangu, Ofisi yangu na mimi mwenyewe binafsi naomba nitoe shukrani zangu za
dhati kwa wajumbe wa Bodi ya UM na Kamati ya Operesheni za Ukaguzi” akasema Bw.
Otouh.
Akabainisha kwamba Tanzania inachukua jukumu hilo
la kuwa mjumbe wa UNBOA katika kipindi muhimu, kipindi ambacho UM unapita
katika mageuzi makubwa ya kubadili mifumo yake ya kiutendaji ikiwamo kutoka
utumiaji wa mfumo ujulikanao kama UNSAS kwenda
mfumo wa IPSAS.
“ Tunaingia katika bodi
hii katika kipindi ambacho UM inapitia mageuzi makubwa yakiwamo yale ya kutoka
ukaguzi uliokuwa ukifanyika kila baada ya miaka miwili na kuingia katika
ukaguzi wa kila mwaka”. Akasisitiza Otuoh
Na kuongeza. “ Matokeo
ya mageuzi haya maana yake ni kuongezeka kwa ukubwa wa kazi kwa upande wa
wakaguzi, ogezeko ambalo litatupasa si tu kufanya kazi kwa umakini mkubwa
lakini pia kutekeleza majukumu mengi na katika muda mfupi”.
Na kwa sababu hiyo,
akasema, kwa kutambua uzito na unyeti wa kazi kubwa iliyombele, ndiyo maana
baada ya kuteuliwa kwake yeye na maafisa wake walianza jukumu la kujianda kwa
kila hali ili waweze kulitekeleza jukumu hilo kwa ukamilifu na weledi mkubwa.
Akatumia fursa hiyo
kuishukuru Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Afrika ya Kusini kwa namna
ambavyo imetoa ushiriano mkubwa na wa karibu sana, kuanzia siku ile Ofisi ya
NAOT ilipopitishwa kwa kauli moja na Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa
kushika wadhifa huo.
Aidha akasema ingawa
Afrika ya Kusini imemaliza ujumbe wake, Tanzania
itaendelea kushirikiana nayo kwa karibu hasa kwa kuzingatia kwamba kukabidhiwa
kwa jukumu hilo
hakuhitimishi mchakato mzima wa kuendelea kubadilishana uzoefu na utaalamu.
Naye Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza kwa niaba ya serikali, pamoja na
kuwashukuru wajumbe wa bodi ya UNBOA na sekretarieti yake. Amesema Serikali
inauchukulia ujumbe huo kwa uzito wa aina yake.
“Nimefurahi sana kuwapo hapa na kuiwakilisha serikali, ninapenda
ninawakikishie kwamba, serikali yangu inalipa jambo hilo
uzito wa kipekee sana .
Heshima na mchango wa Tanzania
katika Umoja wa Mataifa unafamika na sasa tunapoingia katika jukumu hili ni
dhahiri kwamba tunataka kufanya kazi nzuri hata katika maeneo mengine na uwezo
huo tunao” akasisitiza.
Naye Naibu Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu kutoka Afrika ya Kusini Bw. Thembekile Makwetu akizungumza wakati
wa makabidhiano hayo, amemhakikisha Bw. Utouh na ofisi yake ushirikiano wa
karibu na usiotereka. Huku wajumbe wengine wa Bodi nao wakielezea kutoa
ushirikiano kwa Tanzani na kuikaribisha kwa moyo mkunjufu.
Kwa upande wake, Bi
Susan Malcora akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, yeye
amesema anaikaribisha Tanzania katika ujumbe wa bodi hiyo kwa mikono miwili na
kusisitiza kwamba ujumbe wa Tanzania katika Bodi hiyo utasaidi sana katika
kusukuma mbele ajenda ya uwajibikaji na udhibiti wa fedha na mali
zinazomilikiwa na Umoja wa Mataifa.
Akasema Umoja wa
Mataifa, unatambua umuhimu na mchango mkubwa wa Bodi hiyo na kuongeza kwamba
itafanya kazi kwa karibu wa wajumbe wa bodi ili kuhakikisha kwamba mageuzi
yanayoendelea hivi sasa ndani ya UM yanafanyika kwa ukamilifu na kwamba
watazingatia ushauri na maelekezo watakayopewa na Bodi.
Chanzo: Mjengwa blog.
No comments:
Post a Comment