Sunday, July 8, 2012

Viongozi wa CHADEMA walalamikia kutafutwa na watu wa usalama wa Taifa, leo makao makuu ya chama hicho kinondoni.

Wadau,

Leo wakati nikiangalia taarifa ya kurasa katika east Africa TV nimeona taarifa juu ya viongozi wakuu wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA wakilalamika kutishiwa maisha na watu wanaodaiwa kuwa ni usalama wa taifa.

Hili linakera kidogo, hizi taarifa za watu wa kitengo cha usalama wa taifa kutishia maisha ya watanzania wapigania haki ni kilio cha muda mrefu. Sasa sijajua matatizo haya ni uvumi, kasumba ama kuna ukweli wowote.

Wiki chache zilizopita tumeshuhudia kutekwa, kudhalilishwa na kushambuliwa mwili kwa kiongozi wa madaktari nchini Dr Steven Ulimboka, na lawama zote zikakimbilia kwa watu wa usalama wa taifa.

Kawaida watu hawa wanatakiwa kuwa marafiki wa wananchi lakini imekuwa kinyume chake, ni watu hatari na hawafai hata kujulikana. Mtu wa kawaida akisikia anatafutwa na wajamaa hawa kichwani mwake kunajengeka picha ya mijitu mikatili, isiyo na huruma wala utu.

Tufanye nini ili kuondoa kasumba hii ya hatari itakayorithisha woga na hofu kwa vizazi vyetu ambavyo vimekuwa vikiimbishwa kuwa watanzania ni watu wakarimu. Maana hata Rais wetu wakati wa hotuba yake ya mwezi uliopita wakati akizungumzia suala la Dr Ulimboka, alisema mambo haya ya kutekana ni aibu na mapya katika taifa letu la watu wakaribu.

Mimi sjui na nina hakika hata wewe hujui nini cha kufanya ili kurudisha matumaini na kulisafisha jeshi letu la polisi kupitia kitengo hiki cha usalama wa taifa. Natamani kuwasaidia ili kujenga imani tena kwa watanzania, maana elimu niliyosomea inahusiana moja kwa moja na kujenga taswira za watu fulani (Image building).

Naam hili la kujenga taswira mpya kwa watu wa uslama wa taifa ndicho kinachohitajika kwa sasa, hakuna jingine....

HAFIDH KIDO
0713 593894/ 0752 593894
DAR ES SALAAM, TANZANIA  

No comments:

Post a Comment