Huyu ni Katibu wa CWT Ezekiel Oluoch akijibu swali lililoulizwa na mwanahabari leo asubuhi.
Wanahabari wakiwa kazini makao makuu CWT
Na Hafidh Kido
Chama cha waalimu Tanzania kimeamua kutii uamuzi wa Mahakama wa kusitisha mgomo na kurudi katika meza ya majadiliano na Serikali kwani mgomo wao haukufuata taratibu. Ingawa Rais huyo wa CWT alionyesha kutoridhishwa na maamuzi hayo ya mahakama yaliyotolewa jana na jaji wa mahakama kuu kitengo cha kazi jaji Wambura.
Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Rais wa CWT Gratian Mukoba alisema, walimu wanarudi kazini wakiwa wanyonge na hawana imani na waajiri wao (Serikali) kwani haina nia njema ya kuwaongezea posho na mishahara yao.
'Nataka kuwaeleza watanzania kuwa walimu tunarudi kazini lakini hatuna imani na waajiri wetu ambao ni Serikali, maana wanazungumza maneno ya upotoshaji yakilenga kutuchonganisha na watanzania" alisema Mukoba.
Aidha kiongozi huyo wa walimu alipinga madai ya vyombo vya habari vilivyoandika kuwa wakati wa mgomo yeye alikwenda kuripoti kazini katika shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, ambapo yeye ni mwalimu mkuu huku akiwachuuza walimu wengine wasiripoti ofisini kwao.
"Napenda kuwaeleza kuwa sijafurahishwa kwa taarifa za uongo zilizoandikwa na gazeti moja hapa nchini sitolijtaja, lakini waliandika kuwa siku ya jumatatu mgomo ulipoanza nilisaini daftari la mahudhurio shule ya Benjamin Mkapa, si kweli na nitahakikisha naenda kulipeleka mahakamani gazeti hilo ili likathibitishe taarifa ilizoziandika maana hazina ukweli na zililenga kunichonganisha na wanachama wenzangu," Mukoba.
Mukoba ameitangazia Serikali kuwa hawatokuwa tayari kufidia hasara iliyopatikana kutokana na mgomo huo,badala yake Serikali ndiyo inayotakiwa kukaa chini na kutoa ripoti ya hasara iliyopatikana na wao watakuwa tayari kuwajibika.
hata hivyo CWT imepanga kukata rufaa ya hukumu yao kwa madai kuwa yapo mambo ambayo hawajaridhishwa nayo. watakaa na wanasheria wao na kujadili namna ya hatua watakayochukua kukata rufaa.
No comments:
Post a Comment