Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na viongozi wa CUF kwa ngazi ya majimbo na Wilaya nne za Pemba katika ukumbi wa Chuo cha Benjamin Mkapa Wete Pemba.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad,
ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika sensa ya watu na makazi,
ili kuirahishia serikali kupanga mipango yake ya maendeleo kwa uhakika.
Maalim Seif ametoa wito
huo leo katika ukumbi wa chuo cha Benjamin Mkapa Wete Pemba alipokuwa
akizungumza na viongozi wa CUF kwa ngazi za Wilaya na Majimbo.
Amesema Sensa ya watu na
Makazi ni muhimu kwa wananchi na serikali kwa ujumla katika kutathmini na
kuandaa mipango yake ya maendeleo kwa wananchi, na kuwataka kuachana na mtazamo
kuwa suala hilo linaihusu serikali pekee.
Seif ametoa msimamo huo
kufuatia wananchi wengi wa Kisiwa cha Pemba kuwa na mtazamo wa kutaka kususia
suala la sensa kwa madai kuwa hawakushirikishwa ipasavyo katika suala hilo .
Aidha wananchi wa Pemba wanadai kuwa hawawezi kushiriki suala la sensa,
huku wakiwa bado hawajatekelezewa haki zao za kisheria ikiwemo kutopewa
vitambulisho vya ukaazi.
Hata hivyo Seif amewataka
wananchi kupima faida na hasara za kushiriki kwenye zoezi hilo la sensa, na hatimaye waweze kushiriki
kikamilifu kwa maslahi ya maendeleo ya nchi.
Akizungumzia kuhusu
mchakato wa ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya mabadiliko ya katiba, Maalim Seif
amewataka wananchi kuwa huru kutoa maoni yao ,
na kwamba hakuna atakayeadhibiwa kwa sababu ya kutoa maoni. “Mimi najua wapo
wanaotaka serikali moja, wengine mbili, tatu, nne, na muungano wa mkataba,
lakini wengine wanataka waachiwe wapumuwe.
Yote hayo ni maoni na
kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake bila ya kulazimishwa, kwa hivyo wakati
wenu ukifika nendeni mkatowe maoni hayo kwa uwazi”, alisisitiza Maalim Seif.
Amesema lengo la
serikali ya Tanzania
ni kuwa na katiba mpya ifikapo April mwaka 2014, na kufahamisha kuwa kwa
Wazanzibari suala kubwa linalowagusa kwenye mabadiliko hayo ni suala la
Muungano. “Zanzibar tunayo katiba yetu ambayo
imejitosheleza kwa mambo yetu ya Zanzibar ,
lakini suala kubwa kwenye mabadiliko hayo kwetu sisi litakuwa ni la Muungano,
na hili haliwezi kuepukwa”, alibainisha.
Amesema Zanzibar kabla
ya Muungano ilikuwa nchi huru iliyokuwa na kiti chake katika Umoja wa Mataifa,
na kuelezea haja ya kuwepo kwa Mamlaka kamili ya Zanzibar ili iweze kurejesha kiti chake
kwenye umoja huo.
Amewataka wananchi
kuangalia maslahi ya nchi yao
kwanza katika mchakato wa kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba, na kuachana
na misimamo ya vyama katika suala hili linalohusu maslahi ya nchi. “Katiba ya
nchi ni mali
ya wananchi sio ya chama chochote, lakini najua kila chama kina katiba yake na
hiyo ndio itabakia kuwa katiba na muongozo wa chama husika, kwa hivyo ndugu
zangu naomba tulifahamu hili na tuangalie maslahi ya nchi yetu kwanza”,
alifahamisha.
Na: Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment