Katika mitandao ya
kijamii kumesambazwa habari zikimnukuu msemaji wa CCM kutoa madai mbalimbali ya
uzushi katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu CHADEMA baada ya CHADEMA
kuendelea kutekeleza mikakati na mipango yake ya kuwaunganisha watanzania
kupitia falsafa ya ‘nguvu ya umma’ katika kuchangia vuguvugu la mabadiliko
(M4C) katika maeneo mbalimbali nchini.
Nitatoa tamko kamili na
kueleza hatua za ziada baada ya kupata taarifa iliyotolewa kwa ukamilifu, hata
hivyo kuhusu madai yaliyokwisha sambazwa kwenye mitandao ya kijamii na CCM
nachukua fursa hii kutoa kauli ya awali kama ifuatavyo: Kuibuka huku kwa CCM na
kufanya propaganda chafu ni ishara ya kwamba CCM inaumizwa na namna ambavyo
watanzania wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA kwa hali na mali hivyo CCM sasa
inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la mabadiliko kwa kutumia siasa chafu.
Mwenyekiti wa CCM Rais
Jakaya Kikwete anapaswa kueleza watanzania iwapo mikakati hiyo michafu ina
baraka zake na za serikali anayoiongoza kwa kurejea pia madai yaliyotolewa na
Waziri wa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Steven Wassira kuwa CHADEMA
itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa mbinu mbalimbali. CCM kwa
kuwa imekuwa na kawaida ya kufanya usanii kuhalalisha fedha haramu kama
ilivyofanya kwenye chaguzi zilizopita baada ya viongozi waandamizi wa CCM na
makada wake kuchota fedha za chafu kifisadi kama zile za kutoka kwenye Akaunti
ya Madeni ya Nje (EPA) na vyanzo vingine vichafu na kuzisafisha kupitia
harambee za hadaa zilizofanywa na CCM kwa nyakati mbalimbali; inataka kuichafua
CHADEMA inayopata fedha kutoka vyanzo halali kwa njia za wazi ili kukatisha
tamaa umma wa watanzania unaochangia vuguvugu la mabadiliko. Viongozi wa CCM
wameamua kujidanganya, kuidanganya Serikali yao na kujaribu kuwapotosha
watanzania lakini CHADEMA inatambua kwamba watu wachache wanaweza kudanganyika
kwa muda mchache lakini si watu wote wakati wote; na kwamba watanzania wa leo
kwa uwingi wao hawawezi kudanganyika na uzushi wa kijinga wa CCM.Ni ukweli ulio
wazi kwamba CHADEMA imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali
katika kumbi na katika mikutano ya hadhara ikiwemo ya vijijini ambapo michango
hutolewa kwa uwazi, aidha michango kwa njia ya simu inaweza kufuatiliwa na
kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba watanzania wameamua kuchangia mabadiliko
ya kweli.Madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni ya shilingi
kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na narudia kwa mara nyingine tena kuitaka
CCM itaje majina ya serikali, taasisi ama makampuni ya nje ambayo CCM inadai
kwamba CHADEMA imepokea mabilioni ya shilingi katika siku za karibuni au
inatarajia kupokea.
Badala ya CCM
kuisingizia CHADEMA ilipaswa CCM ieleze watanzania orodha ya vigogo wa Serikali
inayoongozwa na wanachama waandamizi wa CCM ambao wanaelezwa kuwa na akaunti
nchini Uswisi na nchi zingine wakituhumiwa kupewa fedha za kifisadi kutoka kwa
makampuni ya utafutaji wa mafuta, gesi asili pamoja na uchimbaji wa madini.
CCM ilipaswa ieleze watanzania
sababu za kuendelea kusuasua kujivua magamba ya ufisadi kinyume na maazimio ya
CCM yaliyofikiwa baada ya msukumo wa CHADEMA kutaja orodha ya mafisadi kwa kuwa
kati ya mafisadi hao ni pamoja na viongozi wa CCM walioiingiza nchi katika
mikataba mibovu.
Ikumbukwe kwamba madai
haya si mapya kutolewa na CCM, yaliwahi kutolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa
Wanawake wa CCM (UWT) Sophia Simba mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 akidai
kuwa CHADEMA imepokea fedha kutoka mataifa ya ulaya kwa ajili ya kufanya maandamano
ya kuiondoa CCM madarakani.
Itakumbukwa kwamba
wakati huo nilimtaka ataje nchi hizo na kueleza kusudio la kumchukulia hatua
zaidi na kwa upande mwingine niliyataka mataifa hayo ya Ulaya yatoe kauli
kuhusu madai hayo. Izingatiwe kwamba mataifa hayo yalikanusha madai hayo ya CCM
na Sophia Simba mwenyewe alikana kuwa hakuna madai hayo dhidi ya CHADEMA.
Nimeelezwa kuwa CCM
imetoa madai mengine ya uzushi kuwa CHADEMA inapewa mabilioni toka nje kwa kuwa
nchi imegundua rasilimali za mafuta na gesi na kudai kuwa fedha hizo ni kwa
ajili ya kuiweka nchi rehani. Madai haya yaliwahi kutolewa pia na Katibu wa CCM
wa Fedha na Uchumi Mwigulu Nchemba na nikamtaka Waziri wa Mambo ya Nje Benard
Membe kutaja nchi hizo na mikataba hiyo hata hivyo mpaka sasa hakuna kiongozi
yoyote wa CCM na Serikali aliyejitokeza kutaja CHADEMA imepokea au itapokea
mabilioni kutoka nchi gani na kwa mikataba gani.
CCM inatoa madai hayo
kuhamisha mjadala baada ya CHADEMA wa uongozi bora, sera makini, mikakati
sahihi na oganizesheni thabiti kuwa mstari wa mbele katika kutetea rasilimali
za taifa na watanzania kutambua kwamba taifa letu litaepushwa kutumbukia kwenye
laana ya rasilimali kwa kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi za mwaka 2014 na
2015 na kuichagua CHADEMA.CCM na Serikali yake ndiyo imekuwa kinara wa kupokea
fedha kutoka nje kwa kisingizio cha misaada na kuingia mikataba mibovu na
mataifa ya nje pamoja na makampuni ya kigeni na kuachia mianya ya uporaji wa
rasilimali za nchi na CHADEMA imeanika hali hii kwenye orodha ya mafisadi kwa
kutaja majina ya viongozi waliohusika kwenye mikataba ya madini na tutaendelea
kufanya hivyo hata katika masuala ya mafuta na gesi ambayo tayari vigogo wa
Serikali inayoongozwa na CCM wameshaanza kuingia mikataba mibovu na kuingiziwa
fedha katika akaunti zao za nje ya nchi.
Hivyo, badala ya CCM
kutoa madai ya uzushi kuhusu CHADEMA kuingia mikataba na serikali au makampuni
ya nje, CCM ieleze watanzania imechukua hatua gani mpaka sasa juu ya viongozi
na wanachama wake waliongia mikataba mibovu kwenye rasilimali muhimu nchini
ikiwemo madini, mafuta, gesi na maliasili zingine za taifa letu na kutoa mikataba
hiyo hadharani ili watanzania waweze kuchukua hatua za kufanya mabadiliko ya
kweli.
Hivi karibuni Rais
Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema kwamba serikali inayoongozwa na
CCM haitarudia makosa ya kuachia mianya ya ufisadi kwenye gesi; hivyo CCM
ilipaswa wakati huu kuwaomba radhi watanzania kwa ufisadi uliofanyika kwenye
madini na rasilimali nyingine na kuishukuru CHADEMA kwa kuendelea kuwaunganisha
watanzania wakati wote kusimamia mabadiliko ya kweli.CCM badala ya kutishia
kuwa ina mikataba inayoihusu CHADEMA ingetoa mikataba hiyo na hali hii ya CCM
inayoongoza Serikali kudai CHADEMA kufanya mikakati, mipango na shughuli iliyo
kinyume cha sheria bila vyombo vya dola kuchukua hatua ni ishara ya CCM kukiri
wazi kuwa chama legelege chenye serikali legelege kimeshindwa kuongoza nchi na
badala yake kimejikita katika propaganda chafu.
CHADEMA tangu kuanzishwa
kwake imekuwa na makubaliano ya ushirikiano (MOU) bila masharti yoyote na vyama
rafiki vya ndani ya Afrika na duniani na makubaliano hayo yamekuwa yakifikiwa
kwa uwazi ikiwa ni sehemu ya CHADEMA kuwa na mtandao wa kimataifa na hayajawahi
kuhusisha wala hayatawahi kuhusisha CHADEMA kusaidiwa mabilioni ya shilingi kwa
ajili ya kufanya kazi zake kama inavyodaiwa na CCM. CHADEMA kimekuwa chama kiongozi
kwa nyakati mbalimbali kueleza viwango cha matumizi yake ya fedha na vyanzo vya
fedha husika huku kikitegemea kwa kiwango kikubwa michango ya wanachama na
wapenzi wa chama hapa nchini pamoja na kutumia kwa ufanisi ruzuku inayotolewa
kwa vyama vya siasa.
CCM imekuwa na kawaida
ya kutoa madai ya uzushi wakati mwingine yakiambatana na kutoa nyaraka za
kughushi inazodai kuwa ni za CHADEMA. Ikumbukwe kwamba wakati wa uchaguzi wa
mdogo wa Igunga, CCM ilitoa madai ya uzushi kuwa CHADEMA inafadhiliwa na nchi
za nje ikiwemo kupewa mafunzo ya ugaidi na kudai kuwa tayari magaidi
wameingizwa na CHADEMA toka nje katika uchaguzi huo; hata hivyo katika mwenendo
wa kesi ya uchaguzi ya Igunga Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama aliyetoa madai
hayo alitoa ushahidi mahakamani kwamba CHADEMA haijawahi kuleta magaidi bali
kauli hizo za CCM zilikuwa ni za siasa za uchaguzi. Hivi karibuni, CCM
imeghushi waraka mwingine na kuusambaza kile ilichodai kuwa ni maazimio ya
kamati kuu ya CHADEMA ya kupanga migomo ya walimu, madaktari na mipango mingine
ya kuhujumu serikali; hata hivyo waraka huo ulidhihirika wazi kuwa ni wa
kughushi.
Mikakati yote hiyo
michafu hupangwa na CCM mara kwa mara wakati ambapo CHADEMA inaanza operesheni
Sangara na mikakati mingine ya kuleta mabadiliko nchini na kujipanga kuiondoa
CCM madarakani kama ilivyo sasa ambapo CHADEMA inaendelea na operesheni katika
mkoa wa Morogoro hivyo watanzania wanapaswa kuipuuza CCM na kuendelea kujiunga
CHADEMA na kuchangia mabadiliko kwa hali na mali mpaka kieleweke.
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi
12/08/2012- Dodoma
No comments:
Post a Comment