Orly Ilemba, akiwa nje ya nyumba aliyokuwa akiishi na
marehemu kaka yake, Patrick Mafisango baada ya mwenye nyumba kutoa nje vyombo
vya ndani kutokana na deni la pango.
Na: Andrew Chale
FAMILIA ya aliyekuwa
kiungo mahiri wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, marehemu Patrick Mutesa
Mafisango iko katika wakati mgumu baada ya kutimuliwa katika nyumba waliyokuwa
wakiishi, Keko Bora jijini Dar es
Salaam .
Familia hiyo, ilitolewa
nje vifaa katika nyumba hiyo na mmiliki wake, kutokana na kudaiwa kodi ya pango
aliyokuwa akiudai kwa muda mrefu uongozi wa Simba.
Akizungumza kwa
masikitiko makubwa jana, mdogo wa marehemu Mafisango, Orly Ilemba, alisema,
mwenye nyumba huyo, Chingweni Mtoro, aliwafuata asubuhi na kutaka chumba chake
kabla ya kutoa vitu hivyo nje ya chumba na kuweka kufuli jipya.
“Nipo nje tokea asubuhi,
hatujafanya lolote, zaidi nalinda vitu vya marehemu, viongozi wa Simba kila
nikijaribu kuwapigia simu hawapokei mpaka sasa sina la kufanya,” alisema
Ilemba.
Alifafanua kuwa,
viongozi hao wa Simba walijua mwisho wa kukaa humo, lakini wameshindwa
kushughulikia suala hilo
mapema mpaka wanakutwa na aibu hiyo.
“Lakini mwenye nyumba
huyu, alisema mkataba huo ulitakiwa kufika mwisho Agosti 8, kama
walivyokubaliana na viongozi wa Simba, lakini mpaka jana viongozi hao
hawakuweza kumalizana naye ndio maana kaamua kufikia hatua hii,” alisema kwa
masikitiko.
Mdogo huyo wa marehemu
Mafisango, yupo nchini kwa ajili ya kusubiria rambirambi, ambazo klabu ya Simba
iliahidi kuzitoa.
Juhudi za kuupata
uongozi wa klabu ya Simba, kujua wana taarifa na wanachukua hatua gani,
zilishindwa kuzaa matunda kwani wahusika, hawakupatikana.
Mafisango kati ya nyota
mahiri waliochangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu
msimu uliopita iliyofikia tamati Mei 6, alifariki dunia Mei 17, 2012 kwa ajali
ya gari, eneo la Keko, jijini Dar es
Salaam .
Juhudi za kuupata
uongozi wa Simba kuzungumzia hali hiyo ilishindikana baada ya baada ya simu
msemaji wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga kutopatikana kwa siku ya jana.
No comments:
Post a Comment