Na Hafidh Kido
Shirika la umeme nchini
(Tanesco) limeanza kutekeleza maagizo ya waziri mpya wa nishati na madini
Profesa Sospiter Muhongo, la kuwashughulikia vigogo wanaolihujumu shirika hilo na kulisababishia
hasara ya mabilioni ya fedha.
Akizungumza na Raia Mwema
ofisini kwake jana meneja habari na mawasiliano wa shirika hilo Badra Masoud
alikiri kuwa kwa muda mrefu Tanesco imehujumiwa na wafanyakazi wasio waaminifu
kwa kushirikiana na wafanyabiashara wakubwa kuiba umeme na kutoa siri za
shirika.
“Ni kweli Tanesco inahujumiwa
shirika limepoteza pesa nyingi ambazo laiti zingeliingia katika mfuko wetu basi
Serikali ingepata pato kubwa sana
kutoka kwetu; lakini tangu aingie Waziri Muhongo mambo sasa yamebadilika na
hatukai ofisini kila siku tupo mitaani kusaka watu wanaolihujumu shirika.
“Waziri Muhongo alishasema
bungeni kuwa wapo watu wanalihujumu shirika hili, na akatoa ahadi ya
kuwashughulikia wote mpaka kufikia mwisho wa mwaka huu. Ili
itakapofika Januari mwakani shirika liweze kufanya kazi kwa faida na kutoa
gawio (dividend) kwa Serikali, ambapo ni kinyume na awali ambapo Serikali
ilikuwa ikitoa pesa nyingi kuiendesha Tanesco,” alisema Badra.
Aidha akionyesha namna
shirika hilo linavyohujumiwa Badra, alisema
katika Tanzania hakuna
shirika linalofikia Tanesco kwa mapato ikiwa shirika hilo litasimamiwa kwa makini na kuwadhibiti
vishoka wanaoliibia.
Hata hivyo afisa habari huyo
wa Tanesco alikiri kuwa ongezeko la vishoka kunasababishwa na ucheleweshwaji wa
makusudi wa huduma za kuunganisha umeme kama nguzo na meta mpya kwani wapo
wafanyakazi wa Tanesco wasio waaminifu ambao hutengeneza matatizo ili waweze
kujinufaisha.
“Ni kweli sababu kubwa ya
kuongeza vishoka ni kutokana na ucheleweshwaji wa huduma, lakini nikiri kuwa
Tanesco hatuna tatizo la nyaya, masanduku ya luku, nguzo wala vifaa vyovyote.
Tatizo linakuja pale wafanyakazi wasio waaminifu wa shirika hili
wanapowadanganya wateja wetu kuwa kuna uhaba wa vifaa hivyo ili waweze kupata
rushwa ndiyo maana wateja wetu wanaamua kutumia njia za panya kuunganisha
umeme,” Badra.
Aidha Tanesco kutokana na
tukio la kukamatwa mmiliki wa kampuni ya ‘low voltage distribution contractors’
inayomilikiwa na Mussa Mtavaz iliyo Mwananyamala A mtaa wa Mwinjuma juzi
jumatatu, wameahidi kufanya uchunguzi ndani ya shirika hilo ili kubaini wafanyakazi wasio waaminifu
wanaoihujumu Tanesco wakisaidiana na wezi aina ya kina Mtavaz.
“Pesa nyingi zimepotea tazama
zile ‘token’ tulizozikamata jana (juzi), zina thamani ya mamilioni ya pesa,
itatuchukua siku kadhaa kuweza kupata thamani halisi ya ‘token’ zile ni nyingi
mno. Tena alikuwa akiuza kwa bei ya chini maana umeme ule hana hasara nao
hajauzalisha wala hajui unapatikana vipi, anawatumia wafanyakazi wetu wasio
waaminifu kuupata na wanauuza.
“Idara ya teknohama (ICT)
ndiyo inacyohusika na upotevu huu wa umeme, hatumtaji mtu ila tutafanya
uchunguzi na atakaebainika mbali ya kumfuta kazi pia tutamshitaki kwa
kulihujumu shirika,” alisisitiza Badra.
Akifafanua namna umeme huo
unavyotoka ndani ya shirika hilo alieleza kuwa Tanesco wana mfumo wa usambazaji
umeme kuenda kwa wateja hivyo kuna kitu kinaitwa ‘group supply code’ ambayo
ndiyo inayotoa ‘token’ za umeme hakuna mtu yeyote anaezijua ‘code’ hizo
isipokuwa watu wa (ICT).
“Tumegundua tatizo lipo huko
(ICT), maana wao ndiwo wanaosimamia hizi ‘code’ zinazotumika kutoa umeme ndani
ya shirika kuenda kwa wateja. Sasa sisi tutahakikisha tunazibadilisha hizo
‘code’ ili hata umeme ukiibiwa usiweze kufanya kazi kwa wateja. Mteja akinunua
umeme kwa hawa wezi hata akiuingiza katika mita zao hautofanya kazi. Si hivyo
tu hata wale watu ambao walishanunua umeme kwa hawa wezi huko nyuma tutawasaka
na tukiwakamata tutawafungulia mashitaka,” aliongeza Badra.
Siku ya jumatatu wiki hii
majira ya saa tisa alasiri maeneo ya Mwananyamala A mtaa wa Mwinjuma nyumba
namba 182, Tanesco wakishirikiana na jeshi la Polisi lililoongozana na
wanahabari walimnasa mfanyabiashara mmoja Said Ibrahim, akiendesha kampuni ya
uuzaji umeme iliyopewa jina la utani ‘Tanesco ndogo’ ambapo Ibrahim alimtaja Mussa
Mtavaz, ambae alikimbia baada ya kusikia Tanesco watafika eneo hilo kuwa ndie
mmiliki wa kampuni hiyo.
Kampuni hiyo iliyosajiliwa
kwa jina la ‘Low Voltage Distributors Contractors’ inayojishughulisha na
kutandaza umeme majumbani, ilikutwa na mavazi yenye nembo za Tanesco, vyuma
maalum vya kupandia nguzo za umeme, nyaraka za wateja wanaotaka kuunganishiwa
umeme, lakiri (seal) za meta za luku pamoja na masanduku ya luku, ‘token’ za
kuuzia umeme na vifaa vingi ambavyo kwa maelezo yake Said Ibrahim, wamevipata
vifaa hivyo kutoka kwa vijana wanaowatumia katika kazi zao.
Kwa maelezo ya majirani wa
mtaa huo hakuna mtu aliekuwa akijua shughuli za ofisi hiyo kwa muda wa miaka
ipatayo kumi mpaka siku hiyo ukweli ulipobainika.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
07/08/2012
0713 593894/ 0752 593894
No comments:
Post a Comment