Na Hafidh Kido
Leo bunge
limeahirishwa mpaka mwezi octoba mwaka huu, utakumbuka kikao cha bajeti ambacho
ndicho kikao kirefu kuliko vikao vyote kilianza tarehe 12 June mwaka huu mpaka
leo tarehe 16 August leo.
Shilingi trilioni
15.19 zimepitishwa kuwa bajeti ya mwaka mzima kwa mwaka wa fedha 2012-2013
ambapo kwa mujibu wa waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda, alisema shilingi
trilioni 10.60 zitatumika kwa matumizi ya kawaida kama mishahara na kulipa
madeni, halafu shilingi trilioni 4.59 zitatumika kwa shughuli za maendeleo.
Aidha Waziri mkuu
Pinda alitaja vipaumbele vya Serikali katika matumizi ya fedha hizo kwa mwaka
huu wa fedha kuwa ni miundombinu,
kilimo, viwanda, maendeleo ya rasilimali watu na huduma za utalii biashara na
uchumi.
“Katika mwaka huu wa
fedha serikali imeainisha vipaumbele vitano ambavyo ni sekta ya miundombinu kama barabara, madaraja na mawasiliano, kipaumbele cha
pili ni kilimo ambapo itahusisha mifugo na uvuvi, kipaumbele cha tatu ni
maendeleo ya viwanda hasa tukiangalia vile viwanda vinavyozalisha bidhaa zake
kwa kutumia bidhaa za ndani.
“Aidha Kipaumbele cha
nne ni maendeleo ya rasilimali watu
tukiangalia sana
ajira na maendeleo ya mtu mmoja mmoja, na kipaumbele cha tano ni huduma za
utalii, biashara na uchumi. Tumehakikisha ndani ya mwaka huu wa fedha
vipaumbele vyote hivyo vimepata mafungu ya kutosha kuweza kutimiza malengo ya
Serikali,” alisema Pinda.
Hata hivyo katika
hotuba yake hiyo ya majumuisho ya kikao cha bajeti Pinda alisema Serikali
itahakikisha hakutakuwepo matumizi mabaya ya fedha ili kuweka nidhamu ya
matumizi.
Waziri mkuu aliongeza
kuwa ili kulinda matumizi mabaya ya fedha Serikali itapima uwajibikaji kwa
watendaji wake na kuhakikisha inapunguza matumizi ya anasa kama
kununua magari ya gharama, posho za vikao, warsha na safari za nje zisizo na
tija.
Aidha katika
kuhakikisha Serikali inapunguza baa la njaa Waziri Mkuu pinda alisema watatoa
tani laki moja katika ghala ya chakula ya taifa ili kupeleka katika mikoa
ambayo imekumbwa na baa la njaa kwa kipindi cha hivi karibu.
Katika suala la
miundombinu Pinda alisema kuwa wakala wa barabara nchini (Tanroads) wamepewa
bil 580 ili kuhakikisha wanakamilisha miradi 14 ya barabara katika mikoa yenye
matatizo ya msongamano wa magari na miundombinu inayoleta usumbufu kwa maendeleo.
Pesa hizo zitatumika kujenga madaraja kama la
kigamboni, barabara za kuzunguka na barabara za juu (fly overs).
Aidha katika mambo ya
msingi ambayo Serikali imeyafanya kwa bajeti hii ni kukaribia lengo la
kufikisha asilimia 15 ya bajeti katika wizara ya afya. Kwani kwa mujibu wa
Waziri Mkuu Pinda, jumuiya ya Afrika ilikutana kujadili suala la kutoa
kipaumbele kwa wizara za afya kwa kuhakikisha bajeti za wizara hizo katika nchi
za Afrika zinafika asilimia 15 ya bajeti ya jumla ili kujenga taifa lenye afya.
“Katika vitu ambavyo
tunajivunia kwa najeti ya mwaka huu wa fedha ni kukaribia lengo la kuwa na
asilimia 15 ya bajeti katika wizara ya afya, ambapo kwa mwaka huu asilimia 10
ya bajeti tumeipeleka katika wizara ya afya, hivyo tumebakisha asilimia tano tu
tufikie lengo,” alisema.
Nae spika wa bunge la Tanzania
Anne Makinda alihitimisha kikao cha leo kwa kuwataka wabunge kuwa watulivu na
kuacha kuingilia kazi ya kamati ya bunge iliyoundwa ili kuchunguza kashfa ya
rushwa inayowakabili wabunge ambao inadaiwa walichukua rushwa katika shirika la
umeme nchini Tanesco ili kupitisha tenda ya uuzaji mafuta kutoka kampuni ya
mafuta ya puma energy.
“Kamati hii inafanya
kazi zake kama mahakama, hivyo kuanza kuzungumza mambo yanayohusu sakata hilo mkiwa majimboni ni
sawa na kuingilia mwenendo wa shauri hili nayo ni makosa. Hivyo nawaomba
wabunge muwe watulivu na kuacha ushabiki,” alisema Spika Makinda na kuahirisha
bunge mpaka mwezi Oktoba mwaka huu.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM , TANZANIA
0713 593894/ 0752
593894
16/08/2012
kidojembe@gmail.com
No comments:
Post a Comment