SERIKALI imesema eneo
linalogombewa na Malawi
katika Ziwa Nyasa ni mali ya
Tanzania na sasa imeziamuru
kampuni za nchi hiyo zinazofanya utafiti wa mafuta kuondoka eneo hilo kuanzia jana.
Onyo hilo
dhidi ya Malawi lilitolewa
jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
ambaye pia amesisitiza kuwa Tanzania
itakuwa tayari dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama.
Hii ni mara ya pili
Serikali kuionya Malawi
katika mgogoro huo. Wiki iliyopita aliyekuwa Kaimu Kiongozi wa Shughuli za
Serikali Bungeni Samuel Sitta alisema: “Tuko tayari kwa lolote dhidi ya Malawi .”
Sitta alitoa kauli hiyo
alipokuwa akijibu Swali la Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi aliyetaka
kujua kauli ya Serikali kuhusu mgogoro huo.
Jana, akiwasilisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2012/13, bungeni mjini
Dodoma , Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe alisisitiza kwamba eneo linalobishaniwa katika ziwa hilo lipo Tanzania .
Alisema pamoja na Jeshi
la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuzipiga marufuku ndege za utafiti za
kampuni hizo, bado zilikaidi na ndege tano zilitua katika eneo la Ziwa Nyasa.
“Serikali ya Tanzania
inapenda kuzionya na kuzitaka kampuni zote zinazoendelea na shughuli za utafiti
katika eneo hilo zisitishe mara moja kuanzia leo (jana),” alisema Membe.Alisema
Serikali ya Tanzania iko tayari kulinda mipaka yake kwa gharama yoyote na
haitaruhusu utafiti huo wa uchimbaji wa gesi na mafuta uendelee.
Alisema chini ya
Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wananchi wa Tanzania watakuwa salama dhidi ya
tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama.
Kiini cha Mgogoro
Kuhusu kiini cha
mgogoro, Waziri Membe huku akirejea historia ya mipaka tangu ukoloni, alisema
ni hatua ya Serikali ya Malawi
kushikilia msimamo kuwa eneo lote la Ziwa Nyasa lipo Malawi
wakati Tanzania
inashikilia kuwa mpaka upo katikati ya Ziwa.
“Wenzetu wanadai ziwa
lote lipo Malawi lakini,
nyaraka zilizotengenezwa na wakoloni wa Kiingereza mwaka 1928 na 1938
zinaonyesha kuwa mpaka wa ziwa hilo
upo katikati,” alisema. Alisema hoja ya Tanzania
ina nguvu kulingana na sheria za kimataifa kwa vile tatizo kama hilo linafanana na mgogoro uliokuwepo baina ya Cameroon na Nigeria .
No comments:
Post a Comment