Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzíbar 23/07/2012
Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuunda Tume ya uchunguzi
wa ajali ya Mv. Skagit iliyozama July 18 mwaka huu ambapo
jumla ya abiria 290 walikuwemo katika meli hiyo.
Balozi Seif
ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi
wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni kuhusiana na kuzama kwa meli hiyo.
Amesema Tume
hiyo itaweza kuishauri Serikali nini cha kufanya katika kuhakikisha kuwa vyombo
ambavyo vinachukuwa abiria vinakuwa vya aina gani na kuweka utaratibu mzuri
utakaoweza kufanikisha usafiri wa baharini.
Ameongeza
kuwa kutokana na hali ya ajali zinazotokea mbali na Tume hiyo,Serikali imeona
kuwa ipo haja ya kupitia
sheria zinazohusu usafiri wa baharini na kuweka aina ya viwango vya meli
zitakazoruhusiwa kuingizwa nchini na kuchukua abiria.
Makamu wa
Pili wa Rais amesema kuwa nia ya Serikali juu ya ununuzi wa Meli kwa ajili ya
usafiri ipo pale pale na kwamba juhudi zinaendelea katika kufanikisha suala
hilo.
Akizungumzia
kuhusu ajali hiyo Balozi amefahamisha kuwa jumla ya watu 146 mpaka sasa
wameokolewa wakiwa hai ambapo Maiti 78 zilipatikana wakiwemo wanaume,wanawake
na watoto.
Aidha amesema
kuwa Chombo hicho kilikuwa na Raia wa kigeni 17 na waliookolewa wakiwa hai ni
15 mmoja amepatikana akiwa amefariki ambaye ni Raia wa Uholanzi na mmoja mpaka
sasa hajapatikana.
Wageni hao
kutoka nchi za nje ni wa Ubelgiji,Marekani,Ujerumani, Uholanzi pamoja na
Israel na Serikali imetoa huduma kwa wageni hao na tayari wameondoka kurudi
makwao kwa salama.
Makamo wa
Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi alieleza kuwa kati ya majeruhi 138
waliopelekwa Hospitali kuu ya Mnazimmoja iliyopo mjini Zanzibar kwa uchunguzi
hadi kufikia leo wagonjwa wote hao walikwisharuhusiwa baada ya kupata matibabu.
Amewataka
wananchi popote pale ambapo wataiona maiti wapeleke taarifa kwa Jeshi la
Polisi,Wakuu wa Wilaya,Mikoa na Masheha ili taratibu za kuihifadhi maiti hiyo
ziweze kuchukuliwa.
Amesema kuwa
zoezi la uokoji linaendelea na kuwashukuru wananchi Vikosi vya ulinzi vya
Tanzania na vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na vyombo binafsi na
wazamiaji kutoka nchi za nje kwa ushirikiano walioutoa uliofanikisha kazi ya
uokoji wakiwemo pia waandishi wa habari na wafanyabiashara.
No comments:
Post a Comment