Wednesday, July 11, 2012

Operesheni Sangara inakuja tena...





Na Hafidh Kido
Chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) wiki ijayo kitaanza rasmi awamu ya pili ya ‘operesheni sangara’ ambapo itawawezesha kuvifikia vijiji 4000 katika mikoa mitano ya Tanzania bara.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki hii katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, katibu mkuu wa CHADEMA Dk Wilbrod Slaa, alisema waliafikiana katika kikao cha dharura cha kamati kuu kuwa wazunguke mikoani ili kuweza kuwaamsha watanzania ambao kimsingi wana uelewa mdogo katika masuala ya kitaifa.

Akitoa mrejesho wa awamu ya kwanza ya operesheni sangara ambapo chama hicho kilifanikiwa kuzunguka robo tatu ya nchi wamejifunza vitu vingi katika ziara hiyo hasa ukandamizwaji wa haki kwa wananchi wa vijijini ambao ndiwo wanaobeba asilimia kubwa ya watanzania.

“Operesheni iliyopita tuliweza kufikia robo tatu ya nchi na mara hii tutahakikisha tunatembea mikoa mitano ambayo ni Tabora, Iringa, Dodoma, Singida na Morogoro. Pia tutahakikisha tunayafikia majimbo 44, kata 806 na vijiji 4000 katika mikoa hiyo ndani ya siku 44,” alisema Dk Slaa.

Akisisitiza malengo ya operesheni hiyo Dk Slaa alisema CHADEMA kimedhamiria kuzama ndani na kuangalia misingi na mizizi ya matatizo ya kiuchumi nchini hivyo wameamua kutumia wabunge wao, maafisa na viongozi wa chama kuhakikisha wanasikiliza matatizo ya wananchi wa vijijini.

“CHADEMA si chama cha msimu kama vingine, hatusubiri uchaguzi wala matukio yanayogusa taifa ndiyo tujitokeze, badala yake tutakuwa hai wakati wote tunapohitajika. Tutapigia kelele haki za watanzania wote na hii ndiyo kazi ya chama cha siasa,” aliongeza.

Aidha kiongozi huyo alisisitiza kuwa kauli mbiu ya operesheni hiyo itakuwa mpya na ya kusisimua kwani kwa pamoja wanasema ‘hakuna kulala, hakuna kula, hakuna kunywa mpaka kieleweke,’ na wataendelea kupinga upotoshwaji wa aina yoyote unaofanywa na viongozi wa Serikali. Vilevile hawatonyamaza kuendelea kudai ‘chenji’ yao ya rada, meremete, tangold, deep green na mikataba yote iliyoingiwa kifisadi nchini.

Katika hatua nyingine Dk Slaa, amesema katika kikao hicho kilichofanyika eneo la Mbezi Garden Dar es Salaam, walikubaliana katika ziara hiyo wahakikishe wanawaamsha wananchi wa vijijini juu ya suala la kutoa maoni ya kuundwa kwa katiba mpya, kwani wamegundua ‘faulo’ nyingi katika zoezi hilo hali ambayo itafanya taarifa zitakazokusanywa kutokuwa sahihi.

“Tumefuatilia kila hatua ya zoezi hili la kukusanya maoni ya katiba mpya na tumegundua kuna upotoshwaji mkubwa ambao utafanya taarifa zitakazokusanywa zisiwe sahihi, maana tumebaini baadhi ya wakuu wa wilaya wanaenda siku moja kabla katika eneo litakalofanyika mkutano wa kukusanya maoni.

“Wakishafika pale wanakutana na viongozi wa vijji na kata kisha wanawatisha na kuamua kupanga watu watakaozungumza katika mkutano na aina ya maswali yatakayoulizwa. Huu ni upotoshwaji wa hali ya juu tutahakikisha tunatoa elimu ya kutosha na kukemea upotoshaji huu,” alizungumza kwa hasira Dk Slaa.

Katika hali hiyo imebainika wananchi wengi walio vijijini wanaoonekana kuwa na uelewa wa katiba wanazuiwa kutoa maoni yao kwani waliopewa kazi ya kuchagua wananchi watakaouliza maswali ni viongozi wa kata na vijiji ambao huamua kuwatanguliza watu waliowapanga na ikifika zamu ya wengine mkutano hufungwa kwa madai kuwa wakati umekwisha.

Kikao cha dharura cha kamati kuu chadema, kilifanyika siku ya jumatatu wiki hii ikiwa ni siku moja baada ya viongozi wa juu wa chama hicho wakiongozwa na mwenyekiti Freeman Mbowe, kuzungumza na waandishi wa habari juu ya suala la katibu mkuu wa chama hicho Dk Slaa, mbunge wa jimbo la Ubungo John Mnyika na mjumbe wa kamati kuu Godbless Lema, kufuatiliwa na watu waliodai ni wana usalama wa taifa kufuatilia nyendo zao kwa lengo la kuwadhuru.

Hata hivyo kauli tofauti kutoka serikalini zilidai viongozi wa chama hicho wanatafuta umaarufu wa kisiasa tu na si kweli kuwa wanafuatiliwa nyendo zao na watu wa usalama.
Katibu mkuu kiongozi Balozi Ombeni Sefue, aliita ni mbinu ya kisiasa na kuitetea idara ya usalama haiwezi kufanya mambo hayo. Naye Waziri wa mambo ya ndani Dk Emmanuel Nchimbi, alitoa agizo la polisi kufanya mahojiano na viongozi hao wa chadema lakini Dk Slaa alikataa kuhojiwa kwa madai kama wanataka wafanye uchunguzi wao kwani yeye kama mwananchi kazi yake ni kutoa taarifa tu.

HAFIDH KIDO
0713 593894/ 0752 593894
DAR ES SALAAM, TANZANIA


 Pia habari hii leo imetoka katika toleo maalum la Raia Mwema..



        

No comments:

Post a Comment