Monday, July 9, 2012

Ujamaa wa Tanzania umegeuka ubepari.

Ndugu zangu

leo wakati nikitoka nyumbani nikakutana na huyu rafiki yangu mtaani, anaitwa Mgosi kwani ni msambaa. Mtani wangu huyu na ni mchapa kazi kweli. Kazi yake ni kuuza duka jirani na nyumbani kwetu.

Nikashangazwa kwa kumuona akifanya kazi ya ujenzi (ufundi mchundu), nikamuuliza ikiwa ameachana na shughuli yake ya kuuza duka, akanijibu hapana ni katika njia za kujiongezea kipato.

Nakumbuka miaka ya sabini wakati ujamaa umekolea nchini mtu hakutakiwa kufanya kazi zaidi ya moja, mtu alitakiwa kuhakikisha kazi anayofanya inampa kipato kitakachomwezesha kupata mahitaji yake ya siku tu ili kuweza kuwapa nafasi wengine nao wazalishe mali.

Baada ya Azimio la Zanzibar mwaka 1992, mambo yakabadilika na ubepari ukashika kani. Sasa watanzania ni mabepari wazuri na wanafanya kazi zaidi ya tatu si mbili tu. Nchi ya China inaanza kupambana na suala hili la kufanya kazi kupita kiasi kwani kunasababisha msongo wa mawazo na kuchosha mwili kabla ya kuzeeka.

Naam watu hawafanyi haya kwa mapenzi bali ni kutokana na hali ya kiuchumi, viongozi siku hizi wanalalamikia kupata kisungura kidogo yaani kipato hakitoshelezi kwa Taifa zima. Tupambane na umaskini.

HAFIDH KIDO

0713 593894/ 0752 593894
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment