Katibu mkuu wa Wizara ya nishati na madini ndugu Eliakim maswi, akizungumza na waandishi wa habari asubuhi hii..
Na Hafidh Kido
Katibu mkuu mpya wa wizara ya
nishati na madini Tanzania Eliakim Maswi, ameanza kuonyesha cheche zake kwa
kutoa mpango kazi wake utakaoihakikishia nchi kuwa na umeme mpaka mwezi Desemba.
Akitoa tamko hilo
la wizara leo asubuhi jijini Dar es salaam ,
Maswi alisema kiasi cha umeme kinachozalishwa kwa sasa kinakidhi mahitaji na hilo linamfanya kuwa na
kiburi cha kukanusha maneno yanayozungumzwa katika vyombo vya habari kuwa nchi
itaingia gizani.
“Mahitaji ya umeme kwa sasa
ni wastani wa kati ya megawati 650 hadi 720, na hiyo inatokana na mchanganuo wa
uwezo wa ufuaji umeme utokanao na maji, gesi asilia, na mafuta,” alisema Maswi.
Akitoa mchanganuo huo Maswi alieleza
kuwa kwa mitambo inayozalisha nishati hiyo kwa kutumia maji itazalisha megawati
120 hadi 151. Ambapo kituo cha Mtera kitazalisha megawati 22, Kidatu 54,
Kihansi 60, nyumba ya Mungu 3, Hale 3 na Pangani itazalisha megawati 9.
Aidha kwa upande wa mitambo
itakayozalisha nishati hiyo kwa njia ya gesi asilia inayopatikana hapahapa
nchini ni megawati 348, ambapo mitambo ya Songas itazalisha megawati 180,
Ubungo Gas Plant I megawati 77, Ubungo Gas Plant II 50, na Tegeta Gas Plant
megawati 41.
Kwa upande wa mitambo
inayotumia mafuta ya Diesel kwa kipindi hicho cha miezi mitano watazalisha megawati
240 kwa mchanganuo ufuatao, IPTL megawati 100, Symbion Dodoma 40, Symbion
Arusha 40 na Symbion Ubungo megawati 60.
Hata hivyo katika hatua
nyingine katibu mkuu huyo wa wizara yenye misukosuko tangu kuingia awamu ya
Rais Kikwete, alieleza kuwa suala la kampuni ya kununua na kusambaza umeme
nchini TANESCO ambayo ipo chini ya wizara hiyo haiwezi kukosa umeme wa kutosha
kwa kukosa mkopo wa bilioni 408, kwani serikali imeshaingilia kati na kutoa
ruzuku ya kutosha kuiendesha kampuni hiyo kwa miezi kadhaa bila tatizo la umeme
kujirudia.
“Wapo baadhi wanaodhani
kwamba suala la mkopo wa shilingi bilioni 408 kwa TANESCO ndiyo njia pekee ya
kuhakikisha upatikanaji wa umeme. Hata hivyo kati ya Agosti, 2011 na Juni 2012,
Serikali ilishatoa jumla ya Shilingi bilioni 222.4, ambazo ni ruziku na si
mkopo.
“Hivi karibuni Serikali
imetoa Shilingi bilioni 25 nyingine ili kuhakikisha mafuta ya kutosha
yanapatikana ili umeme wa uhakika uwepo. Ni wazi kuwa Serikali inachukua hatua
za makusudi kuhakikisha kuwa umeme wa kutosha unapatikana na ndiyo maana mpaka
sasa imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 247.4 kuhakikisha TANESCO inajiendesha
bila matatizo” alisisitiza Maswi.
No comments:
Post a Comment