Wachezaji wa Azam FC wakishangilia bao la kusawazisha lililoingizwa kimiani na Jabir Aziz......
Na Mahmoud Zubeiry, Kinshasa
WAWAKILISHI wa Tanzania katika
Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, (CAF), Azam FC wameanza na sare ya 1-1
dhidi ya Dragons ya hapa katika mchezo wa Kundi B kuwania Kombe la Hisani
kwenye Martyrs mjini hapa.
Hadi mapumziko, wenyeji
walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na mshambuliaji wao hatari, Nkate
Jason dakika ya 24.
Nkate alifunga bao hilo baada ya kuwazidi
ujanja mabeki wa Azam, ambao walichanganyana na kipa wao, Mwadini Ally. Pamoja
na kufungwa, Azam walicheza vizuri katika dakika 45 za kwanza na zaidi walikosa
mipango tu ya kumalizia.
Hata hivyo,
mashambulizi ya pembeni ya wapinzani wao yalilitia misukosuko ya kutosha lango
la Azam katika ngwe hiyo.
Kipindi cha pili Azam
walirudi na kikosi kile kile, lakini walibadilika kiuchezaji na iliwachukua
dakika nne tu kukomboa bao, kupitia kwa Nahodha mpya, Jabir Aziz aliyeunganisha
pasi ya Abdi Kassim ‘Babbi’.
Baada ya bao hilo , Azam waliendelea
kushambulia lango la wapinzani wao, lakini safu ya ulinzi ya Dragons ilisimama
imara kudhibiti mashmbulizi hayo.
Katika dakika ya 76,
kipa Mwadini alipangua kwa uhodari mkubwa mkwaju wa penalti wa Mukinzi Mawesi,
baaada ya mchezaji huyo huyo kuangushwa kwenye eneo la hatari na Ibrahim
Mwaipopo.
Baada ya hapo Azam
walihamia langoni mwa Dragons, ambao safu yao
imara ya ulinzi iliwanusuru adhabu hii leo.
Azam ilicheza mechi ya
leo bila makocha wake wote wawili, Waingereza Stewart Hall na Msaidizi wake,
Kali Ongala ambao wamebaki Nairobi, Kenya pamoja na Daktari Mjerumani Paulo
Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche kutokana na kukosa viza za
kuingia DRC.
Azam ambao ni washindi
wa pili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na Ligi Kuu,
wamepangwa katika Kundi B pamoja na Dragons na Shark FC, ambayo watacheza nayo
Desemba 17.
Ikifuzu kwenye kundi
lake, Azam itaingia Nusu Fainali moja kwa moja, ambazo zitachezwa Desemba 25 na
Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu.
Kundi B, lina timu za
DC Motema Pembe, Diables Noirs, FC MK na Real De Kinshasa.
Kikosi cha Azam leo
kilikuwa; Mwadini Ally, Himidi Mao, Waziri Salum, Luckson Kakolaki, David
Mwantika, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Abdi Kassim, Gaudence Mwaikimba,
Abdallah Seif/Humphrey Mieno na Uhuru Suleiman/Zahor Pazi.
picha na habari vyote kwa hisani ya blog ya Bin Zubeiry aliekuwepo Kinshansa...
No comments:
Post a Comment